Tarehe 31 Mei hadi 4 Juni mwaka huu nilishiriki mkutano mkubwa mtandaoni, "Trade With Africa Business Summit." Mwandaaji, Toyin Umesiri, alikuwa ameniomba nikazungumzie kitebu changu kiitwacho Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Nilifanya hivyo, nikijikita katika kuongelea vipengele vya tamaduni vinavyohitaji kuzingatiwa katika biashara baina ya waAfrika na waMarekani.
Kwenye mkutano ule, nilipata kufahamiana na mtoa mada Joy Wanjiru Zenz, mama mKenya aishiye uJerumani na ni mwanzilishi na mwendeshaji wa jumuia ya wanawake waAfrika waishio Ulaya. Alishuhudia jinsi kitabu changu kilivyokuwa kinatajwa na baadhi ya washiriki wa mkutano.
Siku kadhaa baada ya mkutano, Joy nami tuliwasiliana, akanieleza kuwa wanajumuia wake wamechapisha vitabu kuhusu maisha yao Ulaya. Nilivutiwa na taarifa hii. Ninayafahamu maisha ya waAfrika Marekani, lakini si Ulaya. Ilibidi nimwambie Joy kuwa ninahitaji vitabu hivi. Ninavisubiri kwa hamu.
No comments:
Post a Comment