Monday, May 25, 2009

Jiwe la Mmbuji

Hili ni Jiwe la Mmbuji. Liko mahali paitwapo Ngwambo, katika nchi ya Umatengo, wilayani Mbinga, mashariki ya Ziwa Nyasa. Jiwe hili kubwa linasemekana lina maajabu. Wamatengo tangu zamani wanasimulia mambo ya ajabu yanayotokea hapa.

Wamatengo wanaamini kuna viumbe viitwavyo ibuuta. Ni kama binadamu, ila wadogo sana, na wa ajabu, na katika mataifa mengine wanajulikana pia, kwa majina mbali mbali. Wamatengo wanasema kuwa ibuuta wanakuwepo kwenye jiwe hili usiku wakifanya mambo yao.

Nyumbani kwangu sio mbali na hapo, na jiwe hili tulikuwa tunalisikia tangu tukiwa wadogo. Tukipanda mlimani kijijini kwetu, tulikuwa tunaliona. Mwaka jana nilipita karibu na eneo hili, nikapiga picha ya jiwe hili kama inavyoonekana hapa. Hii ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kulikaribia jiwe hili namna hii.

Nilishangaa kuona watu wamelima mashamba karibu yake, na wanaishi sio mbali na hapo. Habari nilizozisikia tangu utoto wangu kuhusu jiwe hili zilinifanya niamini kuwa hakuna mtu anaweza kusogea hapo, achilia mbali kuishi karibu na hapo.

Mawe ya ajabu yako sehemu mbali mbali Tanzania, Afrika na sehemu zingine za dunia. Baadhi nimeshayaona sehemu kadhaa Tanzania, katika safari zangu za utafiti juu ya masimulizi na imani za jadi. Mawe hayo, pamoja maajabu mengine, kama vile miti mikubwa, maporomoko ya maji, na mapango, ni urithi mkubwa katika nchi yetu.

Utafiti juu ya mambo hayo unatufungua macho kuhusu mila, desturi, imani, na maisha ya binadamu. Tunagundua jinsi wanadamu tunavyofanana. Ni muhimu tuyajumlishe hayo katika mambo tunayofundisha mashuleni, pamoja na mengine, kama vile hadithi. Mtu wa mbali, kama vile mtalii, akija kuangalia jiwe la Mmbuji, kwa mfano, na kusikia habari zake, atakuwa amepiga hatua katika kuwaelewa waMatengo, na atawaelewa zaidi akijifunza pia historia yao, na hadithi zao, kwa mfano kama zilivyo katika kitabu hiki.

Tuesday, May 19, 2009

Maprofesa Hatuvunji Msitu, ni Mwalimu wa Shule ya Msingi

Makala hii imechapishwa katika Kwanza Jamii, Mei 19, 2009
*********************************************************************************

Maprofesa Hatuvunji Msitu, ni Mwalimu wa Shule ya Msingi

Na Profesa Joseph L. Mbele

TUNAONGELEA sana mfumo wa elimu. Kitu kimoja ninachoona hatukizungumzii ipasavyo ni wadhifa wa mwalimu wa shule ya msingi. Jamii haimwoni mwalimu wa shule ya msingi kama mtu wa pekee sana. Lakini, akitokeza mwalimu wa chuo kikuu, kama mimi, jamii inafungua macho na kutega masikio. Jamii inamwona mwalimu wa chuo kikuu, profesa, kuwa mtu wa pekee sana, kumzidi mwalimu wa shule ya msingi.

Kwa miaka kadhaa sasa, nimejjijengea mtazamo tofauti kuhusu suala hilo. Hii ndio mada ya makala yangu hii. Hoja yangu ni kuwa, mwalimu wa shule ya msingi anastahili heshima ya pekee. Tunaposema shule ya msingi, tuzingatie neno msingi.

Neno msingi tunalitumia sana tunapoongelea ujenzi wa nyumba. Basi, tuchukulie mfumo wa elimu kama nyumba. Tunapowazia kujenga nyumba, tunazingatia sana msingi, kuhakikisha kuwa ni imara. Kila mtu anajua kuwa ukishafanya hivyo, nyumba yako itakuwa imara. Basi, na elimu ni hivyo hivyo. Ili iwe imara, ni lazima tuanzie kwenye msingi. Na hapo ndipo tunamkuta mwalimu wa shule ya msingi. Yeye ni kama yule fundi mjenzi tunayemtegemea kutujengea msingi imara. Hapo tunaanza kuelewa maana halisi ya dhana ya shule ya msingi.

Tunaweza kutoa mfano mwingine. Tukichukulia ualimu kama kazi ya ukulima, basi mwalimu wa shule ya msingi ni sawa na yule mkulima anayevunja msitu. Sisi walimu tunaokuja baadaye kwa mfano chuo kikuu, tunakuta shamba limeshatayarishwa. Kazi yetu ni nyepesi tukiichukulia kwa mtazamo huu wa kumkumbuka aliyevunja msitu. Ni lazima tumwenzi mvunja msitu, ambaye ni mwalimu wa shule ya msingi. Ni msitu gani huo anaovunja?

Mwalimu wa darasa la kwanza ana jukumu la kuleta mapinduzi katika akili ya mtoto. Anamtoa katika fikra na mazoea ya kucheza siku nzima na kuwinda ndege na kumwingiza katika ulimwengu wa ukurasa wa daftari na kitabu. Huu ni ulimwengu mwingine kabisa, na mapinduzi yanayofanyika hapa ni makubwa. Mtoto alikotoka anajua lugha ya kuongea na kusikia. Lakini mwalimu wa darasa la kwanza anambadilisha na kumfanya aifahamu lugha andishi. Maneno ambayo mtoto alizoea kuyasema tu na kuyasikia, sasa anapaswa ayaone na ayaelewe yanakuwaje kimaandishi. Ajifunze kuandika na kusoma, sio kusema tu na kusikia. Ajifunze namna ya kupanga kila herufi, neno, na sentensi kwenye mstari ulionyooka. Afahamu ukurasa unapangwaje: aanzie juu kwenda chini, si vinginevyo. Maneno ayaandike vipi, nukta na mkato aziweke wapi, na alama za kuuliza na kushangaa aziweke wapi. Haya ni mapinduzi makubwa ya akilini.

Katika mapinduzi hayo, mtoto anaanza kukiona kila kitu kwa mtazamo wa maandishi. Akiona kiti, anajua namna ya kuandika neno kiti. Akiona mnyama au mdudu, anajua namna ya kuandika mnyama au mdudu. Akili ya kuielewa lugha kama kitu cha kusema na kusikia tu inapanuliwa. Akili hiyo inakutana na lugha kwa kutumia macho. Hii ni lugha andishi.

Baada ya mwalimu wa shule ya msingi kufanya hayo mapinduzi akilini mwa mtoto, ndipo sisi walimu wa madarasa yanayofuata tunaletewa huyu mtoto. Sisi hatuleti mapinduzi. Hatuvunji msitu, wala kujenga msingi. Tunaingia darasani na kuongea sana, na wanafunzi wanaandika wanachosikia. Tunawaambia waende maktabani wakasome. Lakini hayo yanawezekana tu kwa vile mwalimu wa shule ya msingi alishawafundisha hao wanafunzi kuandika na kusoma. Bila hivyo, sisi tungekwama. Kwa bahati mbaya, tunasahau jambo hilo. Tunamsahau aliyevunja msitu na tunadhani kusoma na kuandika kuliwezekana au kulijitokeza kiurahisi tu.

Huwa najiuliza, je, nikiambiwa nikafundishe darasa la kwanza, nitaweza? Nina hakika nitaumia kichwa. Bahati nzuri, kwa miaka kadhaa nimekuwa nawatafuta walimu wa shule za msingi sehemu mbali mbali za Tanzania na kuongea nao. Wamenifungua macho kuhusu mambo kadhaa, kama vile saikolojia na tabia ya watoto. Wamenielimisha kuwa watoto wana saikolojia tofauti kufuatana na umri: watoto wa darasa la kwanza wana tabia hii na hii, na unapaswa unapowafundisha ufanye hivi au hivi. Ukifanya vile au vile, hutafanikiwa katika kuwafundisha. Mimi sikujua hayo, lakini walimu wa shule ya msingi wamenifundisha.

Walimu hao wameniambia kuwa unapowafundisha watoto wadogo, uangalie unatumia muda gani kwa kitu kimoja, ili ubadili na kufanya kitu kingine. Usijaribu kuwafundisha kitu kimoja kwa muda mrefu. Ukitoa maelezo kwa dakika kadhaa, unabadili; labda uwaimbishe wimbo. Baada ya dakika kadhaa, labda wachukue daftari na kuchora; baadaye wasome, na kadhalika. Usijaribu kutoa mhadhara kwa muda mrefu, kama tunavyofanya chuo kikuu. Elimu hii nimeipata kutoka kwa walimu wa shule za msingi. Kwa maana nyingine, ningekurupuka tu na kwenda kufundisha kule, ningeharibu mambo. Sijui maprofesa wangapi wanajua hayo.

Kitu kimoja tunachohitaji ni kumtambua mwalimu wa shule ya msingi kwa kazi anayofanya na kumpa fursa kamili ya kufanya kazi yake. Katika Tanzania, tangu miaka ya mwanzo ya Uhuru, tuna jadi ya kuwatwisha walimu majukumu ambayo si ya lazima. Kwa mfano, kwenye sherehe za kitaifa au mapokezi ya viongozi, walimu wametegemewa kuwaandaa watoto wa shule katika gwaride, nyimbo, ngoma, au halaiki. Maofisa kilimo, wahasibu na watumishi wengine ambao wangeweza kabisa kufanya shughuli hizo, hawaguswi. Kwa nini hao wasifanye hizo shughuli za magwaride, ngoma, na halaiki, kama ni shughuli muhimu? Walimu wametumika katika shughuli nyingine pia, kama vile kusimamia kura na hata kuwapikia viongozi. Hizi ni kero zisizo na sababu. Walimu wana kazi nyingi: kuandaa masomo, kufundisha, na kusahihisha daftari za wanafunzi au mitihani..

Baadhi ya matatizo yanayoendelea kuwepo kutokana na walimu wa ngazi mbali mbali kutokuwa na mshikamano. Ingekuwa bora iwapo walimu wa shule za msingi na wale wa sekondari, hadi wa vyuo vikuu, wawe na mshikamano thabiti, na mawasiliano ya daima. Kama nilivyogusia hapo juu, mwalimu wa shule ya msingi ana mengi ya kutufundisha sisi wengine. Anao uwezo wa kutupa mwanga kuhusu njia waliyosafiri wanafunzi tunaowafundisha vyuoni.

Naamini, ingekuwa bora pia kwa walimu wa vyuo vikuu kujaribu kufundisha shule ya msingi. Ingekuwa njia nzuri ya kujielimisha. Ninafahamu kuwa profesa akienda kufundisha shule ya msingi, waTanzania watamshangaa, na huenda wakadhani amechanganyikiwa. Lakini kuna mengi muhimu ambayo profesa anaweza kujifunza kwa kufundisha shule ya msingi, angalau mara moja moja.

Podikasti ya Kwanza Jamii

Waweza kujipatia picha ya hali ya maisha ya sehemu fulani za vijijini Tanzania katika podikasti ya Kwanza Jamii, kama ilivyorekodiwa na ndugu Maggid Mjengwa. Isikilize hapa




Monday, May 18, 2009

Watoto na Matatizo ya Mtindio wa Ubongo

Makala hii ya Dada Yasinta aliiandika katika blogu yake ya Ruhuwiko nami niliipenda na naiweka hapa kwa ruhusa yake.
*****************************************************************************
Friday, May 15, 2009
WATOTO NA MATATIZO YA MTINDIO WA UBONGO
Ngoja tuendelee na mada hii lakini samahanini imekuwa kinyume.

Wapo watoto wengi wanaozaliwa wakiwa na matatizo mbali mbali, lakini mojawapo nitatizo la mtindio ya ubongo ambalo leo nimeona nilizungumzia kwa undani zaidi.
Matatizo ya mtindio wa ubongo yanatokana au kusababishwa na kizalia (Genetic), dawa alizotumia mama wakati wa ujauzito, matumizi ya madawa ya kulevya, pombe, hali ya hewa, au hata ajali. Mojawapo ya sababu hizo nilizozitaja zinaweza kusababisha kuzaliwa kwa mtoto mwenye mtindio wa ubongo au mtu kupata mtindio wa ubongo.

Nikianza na tatizo la pombe, ni kwamba pombe ina athari kubwa na mbaya kwa akina mama wajawazito. Lipo tatizo linalofahamika kitaalamu kama Fetal Alcoholic Syndrome (FAS) ambalo huwapata watoto ambao wazazi wao walikuwa wanatumia kiwango kikubwa cha pombe wakati wa ujauzito.

Watoto wanozaliwa na tatizo hili wanakuwa na nyuso ambazo sio za kawaida (FacialDeformities), kwa mfano watoto hawa wanweza kuwa na pua bapa na macho yaliyoingia ndani au kuwa na mtindio wa ubongo (Mental Retardations), matatizo ya kusikia na kutokuwa na uwezo wa kusoma.

Kwa hiyo unywaji wa pombe hata kwa kiwango kidogo katika kipindi cha mwezi mmoja hadi mitatu ya mwanzo kwa mama mjamzito huchangia kwa kiasi kikubwa kuzaliwa kwa watoto wenye matatizo haya.

Watot wote wenye matatizo haya ya mtindio wa ubongo wanaweza pia kujifunza kusoma iwapo watapewa msaada maalum na kuandaliwa mazingira mazuri yatakayowashawishi kujifunza kusoma. Malezi kwa watoto wenye matatizo haya, yanatakiwa yawe tofauti na yale ya watoto wa kawaida.

Watoto hawa wanahitaji kuoneshwa upendo, kusikilizwa na mengineyo ya aina hiyo. Hata hivyo swali la msingi tunalopaswa kujiuliza ni kwamba, tutawatambuaje watoto wenye tatizo hili la mtindio wa ubongo wakingali wadogo?

Ukweli ni kwamba ni vigumu sana kwa wazazi kuwatambua watoto wao wenye tatizo hili, kabla watoto hao hawajatimiza umri wa miaka mitatu au minne. Kwa kawaida inashauriwa kwamba mtoto yeyote ambaye anfanya mambo yake pole pole ukilinganisha na watoto wengine wa umri wake, inapaswa kupelekwa haraka hospitalini kwa daktari bingwa wa watoto ili afanyiwe uchunguzi wa kina.

Hata hivyo dalili zifuatazo zinaashiria kuwa mtoto ana tatizo hili Kwanza haoneshi dalili yoyote ya kulia au anaweza kulia kidogo sana. Pili huchelewa sana kutembea na hata kuongea. Tatu haoneshi kuvutiwa nna mazingira yanayomzunguka, kwa maana kwamba hata kama kuna vitu vya kuchezea hawezi kujishughulisha navyo. Nne ni vigumu sana kufundishika na hata kujifunza kusoma huwa ni kazi ngumu ukilinganisha na watoto wa rika lake.

Tano hawezi kula mwenyewe, kuvaa mwenyewe au kujifunza kutumia choo. Hata hivyo zipo dalili nyingi zinazoweza kujitokeza na mara nyingi zinatambuliwa na madaktari maalum wa watoto.

Jinsi wazazi wanavyoweza kuwasaidia watoto wenye tatizo hili:

Watoto wenye mtindio wa ubongo wanafundishika, iwapo tu watafundishwa kwa makini, utulivu na uvumilivu mkubwa, yaani mtu anayemfundisha mtoto wa aina hii hatakiwi kamwe kuwa na hasira, na pia inashauriwa sana kuwapongeza wanapofanya vizuri japo kidogo.

Mwalimu anatakiwa awe mpole na ufundishaji wake usiwe wa haraka haraka, aoneshe mapenzi kwa mtoto, hapaswi kumkemea hata kama anakaosea .

Watoto wa aina hii inashauriwa wapewe nafasi ya kujenga urafiki na watoto wenzao warika lao. Huko nyuma watoto wenye matatizo ya akili walikuwa wantengwa na watoto wenzao katika madarasa, kwa kuwekwa kwenye madarasa maalum.

Lakini siku hizi inashauriwa wachnganywe na wanfunzi wenzao wasio na matatizo ya akili, japo hata kwa nusu siku. Utaratibu huu hujulikana kitaalamu, kama mainstreaming.Itaendelea.....

Thursday, May 14, 2009

Kipanya na Usomaji Vitabu

Mimi kama mwalimu na mwandishi ninaliongelea sana suala la usomaji wa vitabu. Katika blogu hii, maandishi yangu mengi yanahusu suala hilo. Hapa kuna katuni ya Kipanya, ambayo nimeiona kwa Profesa Matondo. Inatoa mchango wake kwa mtazamo unaofanana na wangu. Nitatoa mfano mmoja.













Tarehe 21 Juni, 2008, niliendesha warsha Arusha, na katika mazungumzo yangu nililalamikia tabia ya waTanzania kutopenda kusoma vitabu. Nilitoa mfano kama huu wa Kipanya, kwamba waTanzania wanaposafiri katika basi, hutawaona wakisoma vitabu. Hapo mwanawarsha mmoja, mama Mwingereza, alitoa hoja kuwa utamaduni wa waTanzania wa kuongea na wenzao ndani ya basi unaonyesha wanavyojali mahusiano ya mtu na mtu, tofauti na wazungu, ambao kwao ni kila mtu na lwake. Alimaanisha kuwa jamii ya wazungu imekosa mshikamano; badala ya kuongea na binadamu mwenzao, wanashikilia kitabu. Hoja hii ilinifungua macho.

Kipanya ana tovuti yake hapa

Friday, May 1, 2009

Mchango wa Wabeba Boksi

Leo, siku kuu ya wafanyakazi duniani, napenda kuwakumbuka wabeba boksi. Hao ni waTanzania wanaoishi ughaibuni, wakifanya kazi za mikono, kama vile kubeba na kupanga mizigo ya bidhaa madukani, kusafisha maofisi, kusafisha vyombo mahotelini, kuwatunza wazee, na kadhalika. Watanzania wanaposema kubeba boksi, wanamaanisha kazi za aina hiyo. Na jina hilo linatokana na huu kweli kuwa wengi wa wahusika wanabeba na kupanga maboksi.

Wabeba boksi wanataniwa sana katika jamii ya kiTanzania. Wabeba boksi wengi nao wanajitania. Watanzania wengi wanaziona kazi za boksi kuwa ni kazi duni. Napenda kubadili mtazamo huo kwa kuelezea umuhimu wa boksi. Natumia hilo neno boksi kwa sababu linatumika pia kumaanisha kazi ya kubeba boksi.

Jambo moja la msingi ni kuwa wabeba boksi wanatumia nguvu zao kujipatia kipato. Wao ni tofauti na wezi au mafisadi, ambao wanakula jasho la wenzao. Kwa msingi huu, mbeba boksi anastahili heshima.

Kila kazi halali ina umuhimu wake katika jamii, iwe ni kilimo, uvuvi, usafishaji vyoo, ualimu, udaktari, au upigaji muziki. Kila kazi ya aina hiyo inastahili heshima. Mpiga boksi anafanya kazi muhimu. Bila yeye, jamii itakwama. Anastahili heshima.

Wabeba boksi, kama vile walivyo waTanzania wengine wanaoishi ughabuni, wanatoa mchango mkubwa katika kipato cha Taifa, kwa hela wanazotuma nyumbani, iwe ni kwa ndugu, jamaa, marafiki, au taasisi. Nimesoma taarifa kuwa mwaka 2008, kwa mfano, watu hao waliliingizia Taifa dola zaidi ya 100 millioni. Wenzetu waKenya wanaoishi nje waliingiza nchini mwao dola zaidi ya 400 millioni. Ni wazi kuwa mbeba boksi, akiwa ni mmoja wa watu hao, ni mtu muhimu kwa uchumi wa Taifa.

Je, lipi bora zaidi: kukaa vijiweni nchini bila ajira, au kubeba boksi? Hili ni suali la kutafakariwa.

Kuna wabeba boksi ambao, baada ya kukusanya hela, wanaanzisha miradi nyumbani wakiwa bado ughaibuni, na wengine wanarudi nyumbani na kuanzisha hiyo miradi. Kwa njia hiyo, wanatoa ajira kwa wananchi wenzao.

Mpiga boksi, kwa kukaa ughaibuni, anajifunza mengi. Anarudi nchini akiwa na upana wa mawazo kuhusu dunia na uzoefu wa nidhamu ya kazi, vitu ambavyo vinaweza kutoa changamoto kwa wananchi wengine.

Kwa ufupi, boksi lina umuhimu na heshima yake.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...