Lile tamasha maarufu kabisa la vitabu ambalo limefanyika mjini Minneapolis kwa miaka mingi, mara moja kwa mwaka, limekaribia kabisa. Kuanzia mwaka jana, tamasha limehamia mjii St. Paul, kwenye viwanja vya State Fairgrounds.
Hakuna tamasha kubwa zaidi ya hili katika eneo hili la Minnesota na majimbo ya jirani. Wanahudhuria watu yapata 7,000, wapenzi wa vitabu. Wanakuwepo waandishi, wachapishaji, wahariri, wachora picha za vitabuni, wahakiki, wauzaji wa vitabu na majarida. Wanahudhuria wazee, watu wazima, vijana, na watoto.
Nimeshiriki tamasha hili kwa miaka mingi, kama mwandishi wa vitabu na mwelimishaji katika chuo kikuu na jamii. Kila mara nimepata fursa ya kuongea na wasomaji wa maandishi yangu na watu ambao sijawahi kuwafahamu kabla. Wanakuja na maoni, taarifa, na uzoefu mbali mbali. Tunabadilishana mawazo. Inakuwa ni kama shule muhimu sana. Tamasha linapoisha, jioni, najiona nimeelimika sana.
Namshukuru Mungu kwa kuniwezesha kuandika vitabu na maandishi mengine. Namshukuru kwa namna ya pekee kwa kuniwezesha kuandika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambacho najua kimesomwa na bado kinasomwa na maelfu ya watu hapa Marekani, ambao huguswa na mawazo na ushauri niliotoa katika kitabu hiki.
Kwenye kila tamasha, ambamo kunakuweko vitabu maelfu kwa maelfu, unawajibika kushangaa wadau wanafikiaje uamuzi wa kununua kitabu fulani au vitabu fulani. Nina bahati kuwa kitabu changu, ingawa kimekuwepo sokoni kwa miaka mingi kiasi, hakijachujuka bali kinawavutia wateja. Ninachoweza kusema ni kimoja, kwamba yote ni mipango ya Mungu.
Baadhi ya watu ninaokutana nao ni waandishi chipukizi. Huniulizia namna ya kuchapisha kitabu. Nami huwahamasisha kufuatilia hali ya uchapishaji wa leo, unaotumia tekinolojia tofauti na zile tulizozizoea. Kwa taarifa, na kwa manufaa ya watu wanaoongea ki-Swahili, nimetoa maelezo na uzoefu wangu kuhusu uchapishaji huo na mikakati mingine inayohusika, katika kitabu changu cha CHANGAMOTO: Insha za Jamii.
Nimeshajiandaa vizuri kwa tamasha la tarehe 12. Nakala za vitabu vyangu ninazo, pamoja na matangazo na machapisho mengine. Nangojea kwa hamu kukutana na kuongea na watu wengi. Kwa namna ya pekee, nangojea kuongea na watoto. Insh'Allah, nitaandika ripoti ya tamasha, kama ilivyo jadi yangu.
Kwenye tamasha hili, nimejisajili kwa jina la kampuni yangu ndogo iitwayo Africonexion: Cultural Consultants, ambayo nimekuwa nikijitahidi kuitambulisha Tanzania. Unaweza kuona jina hilo katika orodha ya wauza vitabu, ambayo hi hii hapa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
No comments:
Post a Comment