Sunday, October 13, 2013

Tamasha la Vitabu Twin Cities, Oktoba 12, Lilifana

Tamasha la vitabu, Twin Cities Book Festival, lililofanyika mjini St. Paul, Minnesota, jana, tarehe 12, lilienda vizuri. Niliondoka mapema asubuhi, yapata saa mbili, nikafika kwenye maaonesho saa tatu. Sikuwa nimechelewa, kwani wakati naandaa vitabu vyangu kwenye meza yangu, wengine nao walikuwa wakiandaaa, ingawa wengi walishapanga vitabu vyangu siku iliyotangulia
Meza niliyopata, baada ya kulipia dola 80, ilikuwa namba 12. Nilikuwa nimejisajili kwa jina la Africonexion, ambayo kampuni yangu ndogo inayohusika na uchapishaji na uuzaji wa vitabu vyangu, na pia kuratibu mihadhara yangu ya kuchangia maelewano baina ya watu wa tamaduni mbali mbali. Tangu nilipoisajili kampuni hii, shughuli zake zimekuwa zikifanyika zaidi hapa Marekani, lakini hatimaye, hasa nitakaporejea Tanzania baada ya kustaafu hapa Marekani, nataka kuijenga kampuni hii Tanzania, Africa Mashariki, na sehemu zingine.







 




Kama kawaida, watu walianza kuingia ukumbini tangu milango ilipofunguliwa. Ukiwaangalia wanavyojishughulisha kuangalia vitabu kwenye meza mbali mbali, unaona kabisa kuwa hao ni watu wanaothamini elimu. Kwa vigezo vyangu, hao ni watu walioelimika.











Inavutia kuona jinsi watu wanavyoacha shughuli zao nyingine ili kuja kwenye tamasha la vitabu. Ingekuwa ni Tanzania, watu hawangehudhuria. Hilo nimeshuhudia tena na tena, na nami, na wengine wengi, tumeandika sana kuhusu suala hilo. Kadiri miaka inavyopita, Tanzania inazidi kuwa taifa la wajinga. Hakuna sababu ya kubembelezana; ukweli lazima usemwe.









Ushahidi wa kuelimika ni kuwa na kiu isiyoisha ya kujifunza mambo. Ni dukuduku ya kutaka kujua, ambayo kwa ki-Ingereza huitwa "intellectual curiosity." Mtu asiye na "intellectual curiosity" hajaelimika, kwa sababu kuridhika na kile ambacho unadhani unajua, ambacho kwa kweli ni kidogo, ni ujinga. Ni wajibu wangu kama mwalimu kupambana na tabia za aina hiyo, bila kumwonea aibu mtu yeyote.








Kama kawaida, ushiriki wangu katika tamasha la Twin Cities Book Festival ulikuwa na mafanikio mazuri. Nilionana na kuzungumza na watu wengi waliofika kwenye meza yangu. Niliuza vitabu kadhaa. Niliitangaza kampuni ya Africonexion kwa kuwagawia watu chapisho la ukurasa moja ambalo linaelezea shughuli zake, na pia niliwapa kadi ya biashara ya Africonexion.

Binti yangu Zawadi alifika baadaye kunisaidia kwenye meza yangu, nami nikapata fursa ya kutembelea meza za wachapishaji na waandishi wengine. Nilielimika sana kwa kuongea na watu mbali mbali, kujionea shughuli za uchapishaji na maelfu ya vitabu vilivyokuwepo kwenye maonesho. Nilipata fursa ya kuwaelimisha wengine, kama mwalimu, mwandishi na mshauri katika masuala ya tofauti za tamaduni na athari zake.

1 comment:

Rachel Siwa said...

Hongera Sana..MUNGU azidi kubariki kazi zako na ndoto zako!!!!!

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...