
Ushauri wangu nimeutoa katika kitabu kiitwacho CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Lakini inaeleweka kuwa ukiwa na wazo ukaliweka kitabuni, usitegemee kama wa-Tanzania wataliona. Huu ni ukweli ambao umesemwa tena na tena. Nami sidhani kama nina la kuongeza. Papo hapo, falsafa yangu ni kuwa ukiwa na jambo la manufaa, waeleze wengine.
Kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences ndicho chenye mauzo kuliko vingine vyote. Kila ninapoona kimenunuliwa, najiuliza ni nani huyu aliyenunua. Pengine inakuwa ni nakala moja, lakini pengine ni nakala za kutosheleza darasa. Nami sijui ni nani kaagiza. Hiki kitendawili kinanifanya niwe na dukuduku, na nafahamu kuwa sitapata jawabu.
Kuna wakati zinapita siku nyingi kidogo bila mtu kukinunua, lakini wakati mwingine hali hubadilika ghafla. Kwa mfano, Oktoba 31, niliona mtu kanunua nakala 51. Laiti ningemfahamu. Ningempelekea barua ya shukrani na pia nakala ya bure kama kifuta jasho. Lakini simjui. Ni kitendawili.
Namshukuru Mungu kwa jinsi alivyoniwezesha kuandika na kuwagusa walimwengu kiasi hicho. Yote ni uwezo wake.