Wednesday, November 13, 2013

Kitabu Kinapendwa

Tangu nichapishe vitabu vyangu mtandaoni, ninaweza kufuatilia mauzo kila siku. Nimefungua duka mtandaoni, na nimetoa ushauri kwa waandishi wengine, hasa wa-Tanzania, kuhusu uzuri na ubora wa tekinolojia hii.

Ushauri wangu nimeutoa katika kitabu kiitwacho CHANGAMOTO: Insha za Jamii. Lakini inaeleweka kuwa ukiwa na wazo ukaliweka kitabuni, usitegemee kama wa-Tanzania wataliona. Huu ni ukweli ambao umesemwa tena na tena. Nami sidhani kama nina la kuongeza. Papo hapo, falsafa yangu ni kuwa ukiwa na jambo la manufaa, waeleze wengine.

Kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences ndicho chenye mauzo kuliko vingine vyote. Kila ninapoona kimenunuliwa, najiuliza ni nani huyu aliyenunua. Pengine inakuwa ni nakala moja, lakini pengine ni nakala za kutosheleza darasa. Nami sijui ni nani kaagiza. Hiki kitendawili kinanifanya niwe na dukuduku, na nafahamu kuwa sitapata jawabu.

Kuna wakati zinapita siku nyingi kidogo bila mtu kukinunua, lakini wakati mwingine hali hubadilika ghafla. Kwa mfano, Oktoba 31, niliona mtu kanunua nakala 51. Laiti ningemfahamu. Ningempelekea barua ya shukrani na pia nakala ya bure kama kifuta jasho. Lakini simjui. Ni kitendawili.

Namshukuru Mungu kwa jinsi alivyoniwezesha kuandika na kuwagusa walimwengu kiasi hicho. Yote ni uwezo wake.


3 comments:

emu-three said...

Sijui utanisaidiaje na mimi niweze kufika huko

Yasinta Ngonyani said...

Ni kizuri kweli binafsi nshasoma mara kadhaa,,,HONGERA SANA!!

Anonymous said...

Sijui kama ni kweli kitabu kinapendwa. Kitapendwaje au tutajuaje kinapendwa wakati anayekipigia debe ni mtunzi? Yaani prof ina maana hicho ndicho kitabu chako unachojivunia kwenye muda wote wa kufundisha? Je unacho kitabu chochote cha kiada?

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...