Tuesday, October 16, 2018

Vitabu Nilivyonunua Leo

Leo niliamua kutembelea maduka ya vitabu kwenye miji ya Apple Valley na Burrnsville hapa Minnesota. Apple Valley, kwenye duka la Half Price Books,  nilinunua vitabu vitatu bila kutegemea. Nilipita sehemu ya vitabu vya Hemingway, ambapo sikuona kitabu kigeni kwangu. Nilienda sehemu ya bei nafuu, nikanunua vitabu vitatu.

Kimoja ni Essays and Poems cha Ralph Waldo Emerson, kilichohaririwa na Tony Tanner. Kwa miaka mingi nimefahamu jina la Emerson. Nilifahamu kuhusu insha yake "Self Reliance," ingawa sikuwa nimewahi kuisoma. Nilifahamu pia kuwa ameathiri sana falsafa na uandishi, sio tu Marekani, bali kwingineko. Kwa hali hiyo, sikusita kununua kitabu hiki, hasa baada ya kuona kuwa kina mashairi ya Emerson. Sikujua kuwa alitunga mashairi.

Kitabu kingine nilichonunua ni Collected Poems cha Edna St. Vincent Millay. Huyu ni mwandishi ambaye sidhani kama niliwahi kusikia hata jina lake. Lakini nilipoona hiki kitabu kikubwa sana chenye kurasa 757 na nyongeza ya kurasa 32, na halafu nikasoma taarifa za huyu mwandishi, kwamba alikuwa mwanamke mwenye kujiamini na uthubutu katika utunzi wa ma shairi, na mwanaharakati ambaye katika mazingira ya miaka ya 1920 kuelekea 1930 alikuwa akitetea uhuru wa mtu binafsi na hasa wanawake, na halafu nikaona alipata tuzo maarufu ya uandishi iitwayo Pulitzer Prize mwaka 1923, niliona lazima ninunue kitabu hiki, ili nifaidi utunzi wa mama huyu.

Si kawaida kukutana na tungo za wanawake wa zamani namna hiyo hapa Marekani. Tungo ya mwanzo kabisa ambayo nimewahi kusoma na kuifundisha ni The Awakening, ya Kate Chopin. Hiyo ni riwaya ya mwanzo mwanzo inayotambulika kama ya kifeministi. Kutokana na kufahamu kiasi fulani harakati za wakati ule, nilivutiwa na kitabu hiki cha mashairi ya Edna St. Vincent Millay, ambaye alikuja baada ya Kate Chopin.

Kitabu cha tatu nilichonunua ni The Mother, cha Maxim Gorky, kilichotafsiriwa na Hugh Aplin. Maxim Gorky ni mwandishi wa zamani wa Urusi. Nilipoona kitabu hiki, nilikumbuka enzi zangu kama mwanafunzi katika idara ya "Literature" ya chuo kikuu cha Dar es Salaam, ambapo mwalimu wetu Mofolo Bulane alitufundisha nadharia ya fasihi kwa mtazamo wa ki-Marxisti.

Katika mafundisho yale alituwezesha kufahamu kuhusu waandishi wengi, wakiwemo wa Urusi, kama vile Leo Tolstoy, Fyodor Dostoyevsky, Maxim Gorky, Vladimir Mayakovsky, Anna Akhmatova, na Mikhail Sholokhov. Tulijifunza kuwa Gorky ni moja wa waandishi waanzilishi wa mkondo wa "Socialist Realism," ambao ulifuatwa baadaye na akina Mayakovsky na Ana Akhmatova na wengine. Kutokana na kumbukumbu hizi za ujana wangu, niliamua kununua kitabu hiki ili niweze kukisoma nitakapopata wasaa. Baada ya kununua vitabu hivyo, nilielekea kwenye mji jirani wa Burnsville, kwenye duka la vitabu la Barnes Noble. Nitaandika juu ya safari hiyo wakati mwingine.

Saturday, October 13, 2018

Nimeshiriki Tamasha la Vitabu la Deep Valley

Leo nilienda Mankato, Minnesota, kushiriki tamasha la vitabu liitwalo Deep Valley Book Festival. Hii ilikuwa mara yangu ya nne kushiriki tamasha hilo. Ilikuwa fursa ya kuongea na watu kwa undani kuhusu mambo mbali mbali.

Kuna watu kadhaa ambao nawakumbuka zaidi. Mmoja aliniambia kuwa ana binti yake ambaye anafundisha ki-Ingereza kama lugha ya kigeni. Hapa Marekani somo hilo linajulikana kama English as a Foreign Language. Hufundishwa kwa wahamiaji ambao wanahijtaji kujia lugha hiyo, ambayo ndio lugha rasmi ya hapa Marekani. Nilichangia mada hiyo kwa kuelezea jinsi sgughuli ya kufundisha ESL inavyofungamana na suala la tamaduni. Hufundishi tu muuno, sarufi, istilahi, bali pia utamaduni wa mazungumzo.

Mama mmoja mzee, mwandishi, ambaye meza yake ilikuwa mbele yangu, alifika kunisalimia na kuongea. Nilimwuliza ameandika kuhusu nini, akaniambia kitabu chake kinahusu changamoto aliyopitita kufuatia binti yake kujitokeza kama mwenye silika ya mapenzi ya jinsia yake. Nilivyomwelewa huyu mama, ilikuwa ni changamoto kubwa kwake, na ndiyo aliyoandika kitabuni. Nilimwambia kuwa nami nilianza kuelewa suala hili la mapenzi ya jinsia moja nilipokuwa masomoni katika chuo kikuu cha Wisconsin-Madison, ambapo palikuwa na wana harakati wa aina mbali mbali. Nina nia ya dhati ya kukipata ta kiabu chake.

Kijana mmoja alikuja mezani pangu akaniambia kuwa anafuatilia habari za mwandishi Sinclair Lewis. Anamwigiza, yaani kujifanya yeye ndiye mwandishi huyo. Akaniuliza iwapo ataweza kupata wapi habari zaidi. Nikamwambia kuwa kwa bahati nzuri, Marekani ni Makini kwa kutunza taarifa za watu mashuhuri kama hao waandishi. Nilimwabia kuhus nyumba ya makumbusho ya Carl Sandburg, ambayo niliwahi kuitembelea, mjini, Galesburg, Illinois, na nyumba za makumbusho ya Ernest Hemingway ambayo niliwahi kutembelea mjini Oak Park, Illinois, na sehemu zingine, kama vile maktaba ya JF Kennedy ambayo niliwahi kuitembelea Boston.

Watu wamenieleza uzoefu wao wa kuishi na waAfrika hapa Marekani na kujione tofauti za tamaduni, kwa maana ya mienendo, namna ya kufikiri na kutenda. Mzee moja aliniambia kuwa ana jirani mSomali. Alinunua kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, nami nikamhimiza asikose kumwazimisha huyu mSomali asome.

Nami nimepata fursa ya kuwaeleza wat hao kuhu mialiko ninayopata kwenda sehemu mbali mbali kuelezea athari za tofauuti za tamaduni. Wakati wa kuongelea kitabu changu, nimeelezea mtindo wa uandishi niliotumia. Nimepata fursa ya kuongelea kitabu cha Matengo Folktales, pia, nilivyokiandaa kwa miaka mingi, tangu kurekodi hadithi hadi kuzitafsiri na kuzichambua, na hatimaye kuchapishwa. Sikukosa kuelezea kilivyotajwa mwezi November tarehe 23 katika kipindi cha TV ch Jeopardy. Nilikuwa nimechukua karatasi yenye tamko la Jeopardy a, ambao  hawakuweza kujibu/.

Mbali ya vitabu vyangu, nilichukua vitabu vya Bukola Oriola na kitabu cha mwanae Samuel Jacobs, mwenye umri wa miaka kumi na moja. Bukola Oriola niliwahi kumzungumzia katika blogu hii. Tangu nilipomwelekeza namna ya kuchapisha kitabu chake cha kwanza, amefika mbali. kwani aliteuliwa na Rais Obama kuwa katika United States Advisory Council on Human Trafficking.

Nimekutana na rafiki yangu Becky Fjelland Brooks, mwalimu wa South Central College, ambaye ni mpenzi mkubwa wa kitabu changu cha Africans and Americans, amewahi kunikalika mara kadhaa nikaongee na wanachuo wake. Akaandika taarifakadhaa, kama hii hapa na hii hapa.


Thursday, October 11, 2018

Mchakato wa Kwenda Kuongelea Kitabu

Leo nimepata ujumbe kutoka kwa Dan, ambaye hivi majuzi alikipigia debe kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, katika duka la Barnes and Noble, kama nilivyoelezea katika blogu hii. Anaendelea na juhudi yake. Ameandika:

Happy to spread the word about your book. Let me know if you are ever interested in doing a talk at our store. I can connect you with our manager.

Tafsiri yangu:

Ninafurahi kukitangaza kitabu chako. Nijulishe iwapo utapenda kuja kukiongelea katika duka letu. Nitaweza kukuunganisha na meneja wetu.

Kuwaalika waandishi kuongelea vitabu vyao ni utamaduni wa kawaida hapa Marekani. Ni fursa ya mwandishi kukutana na watu wanaotaka kujua mambo kama  historia ya mwandishi, changamoto za uandishi, falsafa na mawaidha yake kuhusu uandishi, na kadhalika. Vinakuwepo vitabu vya mwandishi, kwa watu kuvinunua na yeye kuvisaini. Wa-Marekani wanapenda kusainiwa vitabu, kama nilivyowahi kusema katika blogu hii.

Wednesday, October 10, 2018

Naambiwa Niongeze Bei ya Kitabu

Katika matamasha ya vitabu ninayoshiriki, ninakutana na mambo mengi, zikiwemo tabia na mitazamo ya wateja. Moja ambalo linanigusa zaidi ni pale mteja anaposhauri niongeze bei ya kitabu changu. Hiyo imetokea mara kadhaa, kuhusiana na vitabu vyangu viwili: Africans and Americans: Embracing Cultual Differences na Matengo Folktales.

Vitabu hivi ninaviuza kwenye matamasha kwa dola 14 kila kimoja. Kwa kujua kwamba watu wengine wanatoa  noti ya dola 20 au noti mbili za dola kumi kumi, ninajitahidi kuwa na chenji. Ajabu ni kwamba watu wengine hawasubiri chenji, na wengine wanakataa. Wanachotaka ni kitabu waende zao. Ninakumbuka watu waliowahi kutoa noti ya dola 20 bila kutaka chenji. Mmoja wa hao, nilipojiandaa kumpa chenji, alisema hiyo chenji ni shukrani yake kwangu kwa kuandika kitabu.

Tarehe 4 mwezi huu nilikutana na jambo jingine kabisa. Mama moja, Jackie, ambaye nimemfahamu miezi michache iliyopita na akasoma hivi vitabu vyangu viwili, alinialika kwenye mhadhara wa rafiki yake Maria kuhusu vitabu na maisha yake. Alikuwa ameniambi nije na nakala za vitabu vyangu, ili aweze kuvipeleka katika tamasha la vitabu. Baada ya mhadhara, wakati tulipokuwa tunajumuika kwa viburudisho na maongezi, Jackie akanulizia bei ya vitabu vyangu, nami nikamwambia kuwa ni dola 14. Alisema nipandishe iwe 15, kwa ulinganisho na kitabu cha dola 10 na pia kwa urahisi wa chenji.

Alinitambulisha kwa rafiki yake, akamwambia kuhusu hivi vitabu vyangu. Alivyokuwa akielezea hayo, akaniambia nivitoe kwenye begi, nikampa. Huyu rafiki alichagua Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, akapanda ngazi kwenda kuchukua hela akaja akanipa na kitabu akachukua. Dakika chache baadaye, mama huyu alinitambulisha kwa mama mwingine, na akamwambia kuhusu vitabu. Naye akanunua Matengo Folktales.

Kwa hivyo nimejikuta nikiafiki wazo la kuongeza bei ya vitabu vyangu. Hata hivyo, bei hiyo ni ndogo kulingana na bei za mahali pengine za vitabu hivyo. Ninaamini kuwa taarifa hii ina ujumbe kuhusu watu wanaothamini vitabu kuliko fedha. Kama nilivyowahi kusema tena na tena, blogu hii ni sehemu ambapo ninajiwekea mambo yangu binafsi, kama vile kumbukumbu, hisia, na mitazamo. Ikitokea haja, siku zijazo, ya kuandika kitabu kuhusu maisha na kazi zangu, blogu hii itakuwa chanzo muhimu cha taarifa.

Thursday, September 27, 2018

Nimenunua Tena Tungo Zote za Shakespeare

Tarehe 24 Septemba, nimenunua tena kitabu cha tungo zote za William Shakespeare.  Nilikinunua katika duka la Half Price Books mjini Apple Valley nilipotoka Burnsville kuangalia kitabu changu kama nilivyoelezea katika blogu hii.

Ingawa tayari nina vitabu vinne vyenye tungo zote za Shakespeare, sikuona tatizo kununua hiki pia. Kuwa na nakala mbali mbali za kitabu cha tungo za Shakespeare kuna mantiki nzuri kwa sababu tungo hizo zimehaririwa kwa namna mbali mbali. Hii imekuwa ni sehemu ya historia ya uchapishaji wa tungo za Shakespeare.

Mara kwa mara neno linaloonekana kwenye nakala fulani si lile linaloonekana kwenye nakala nyingine au limeandikwa kwa namna tofauti na lilivyo katika nakala nyingine. Hali hiyo ni ile inayoonekana katika miswada ya tungo za zamani, sehemu mbali mbali ulimwenguni, ikiwemo za huku kwetu, kama zile za Liongo Fumo.

Tofauti hazikwepeki, kwa sababu uandishi katika enzi za Shakespeare ulikuwa tofauti na wa leo. Leo kitabu kikichapishwa, tunategemea ni nakala sahihi ya mswada ulivyoridhiwa na mwandishi. Wakati wa Shakespeare, hapakuwa na utaratibu huo. Watu walikuwa wananakili andiko walivyoweza, na tofauti mbali mbali zilijidhihirisha kutoka kwa mnukuzi hadi mwingine.

Kadhalika waigizaji wa tamthilia majukwaani walikuwa wanatamka, pengine bila kujitambua, maneno yaliyofanana sauti, ingawa maneno ya mwandishi yalikuwa tofauti. Hiyo nayo ni sababu ya waandishi kuandika maneno tofauti.

Kwa hali hiyo, ni busara kuwa na nakala tofauti za kitabu hiki cha tungo zote za Shakespeare. Hata mtu ukiwa na kitabu cha tamthilia mojawapo tu, ni busara kuwa na nakala zilizohaririwa na wahariri tofauti wa kitabu hicho.

Faida nyingine ni kwamba baadhi ya nakala hizi zina maelezo ya wahariri juu ya mambo mbali mbali, yakiwemo maana za maneno na semi. Maelezo haya ni msaada mkubwa kwetu, kwani ki-Ingereza cha wakati wa Shakespeare kina tofauti nyingi na kiIngereza cha leo.

Monday, September 24, 2018

Nimekikuta Kitabu Changu Barnes and Noble

Baada ya kusikia kwamba kitabu changu kimewekwa sehemu maalum katika duka la Barnes and Noble, kama nilivyoandika katika blogu hii, leo nimeenda Burnsville kuangalia. Hapa kushoto linaonekana duka hilo, ambalo nimelitembelea mara kadhaa.





Hapa kushoto ndio mwonekano wa kabati ambapo huwekwa vitabu vilivyopendekezwa na wahudumu wa duka. Kitabu changu kinaonekana hapo chini. Duka lolote la Barnes and Noble huwa na vitabu vingi sana. Ni kama maktaba. Kwa hiyo, kitabu kuuzwa humo si jambo la ajabu. Hakunaajabu yoyote kwa kitabu changu kuuzwa Barnes and Noble. Kama nilivyoandika juzi, kitab changu hich kimekuwepo kwenye mtandao wa Barnes and Noble kwa muda mrefu.





Kitu cha pekee ni uamuzi wa mhudumu wa duka kukipendekeza kwa wateja, kama inavyooneka hapa chini ya kitabu:

Short and sweet. A wonderful read about the differences between Africans and Americans. I feel wiser to the world after reading it.
Tafsiri yangu:
Kifupi na kitamu. Andiko la kupendeza ajabu kuhusu tofauti za tamaduni baina ya waAfrika na waMarekani. Najiona nimejiongezea werevu mbele ya dunia baada ya kukisoma.

Ninafurahi kwa sababu huyu mhudumu, mwenye uzoefu katika maktaba amesema hivyo. hudumu wa maktaba hapa Marekani ni msomaji wa vitabu. Anapopendekeza kitabu hawezi kupendekeza kiholela. Aanajua kuwa wadau wanaofika humo ni wa kila aina. Wengine ni wasomi waliobobea. Anaweka heshima yake rehani, kwani wadau wakinunua wakaona si kitabu bora, ataaibika yeye kabla ya mwandishi. Hiyo ni sababu ya wazi ya mimi kufurahi.

Friday, September 21, 2018

Kitabu Kimeingia Barnes and Noble

Kwa wasomaji wa vitabu hapa Marekani, jina la Barnes and Noble si geni, kwani ni jina la kampuni inayomiliki maduka mengi ya vitabu yaliyoko nchi nzima. Maduka ya Barnes and Noble ni maarufu kiasi kwamba watu wanapoongelea maduka ya vitabu, huwazia kwanza Amazon na Barnes and Noble.

Leo nimepata ujumbe kutoka kwa mhudumu wa duka la Barnes and Noble Burnsville, mwendo wa nusu saa kutoka hapa ninapoishi. Ameandika:

Hi Joseph. Just letting you know I put your book on the staff recommendation display at the Barnes and Noble Burnsville where I work. The book about cultural differences between Africans and Americans. I really enjoyed it!

Tafsiri yangu:

Jambo Joseph. Nakufahamisha tu kwamba nimeweka kitabu chako sehemu vinapoonyeshwa vitabu vilivyopendekezwa na wahudumu wa duka la Barnes and Noble Burnsville ambapo ninafanya kazi. Kile kitabu juu ya tofauti za tamaduni baina ya wa-Afrika na wa-Marekani. Nilikifurahia sana!


Bwana huyu aliyeniandikia ujumbe alikuwa mhudumu wa duka la vitabu la hapa Chuo cha St. Olaf,  na ndipo alipokisoma kitabu changu. Yeye na wahudumu wenzake tulikuwa tukipenda kuongea. Kwa kuwa walikuwa wamesoma kitabu changu, walipokuwa wanaenda kujisaidia walipenda kusema, "kuchimba dawa," usemi waliouona kitabuni. Tulikuwa tukicheka. Nilikuwa nikivunjika mbavu na kujisikia raha kuwasikia hao wazungu wakiwa wa-Swahili namna hiyo. Niliona kitabu changu kimewagusa.

Nimefurahi kusikia kuwa kitabu changu kimeingia Barnes and Noble namna hiyo. Nasema ”namna hiyo” kwa maana ya kitabu kuwemo dukani, kwani, kwa miaka, kimekuwepo kwenye mtandao wa Barnes and Noble. Sitaki kusema mengi, nisije nikawa nahesabu vifaranga kabla havijaanguliwa, kama isemavyo methali ya ki-Ingereza. Nitasubiri nione.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...