Kadiri siku zinavyopita, neno tekinolojia linazidi kusikika miongoni mwa wa-Tanzania, kama ilivyo duniani kwa ujumla. Tekinolojia ya leo imetuletea mambo mengi, mojawapo likiwa ni mtandao. Ulimwengu unazidi kuunganishwa kwa tekinolojia ya mawasiliano ambayo kifupi tunaiita mtandao.
Lakini kuna hatari kuwa hizi dhana zinabaki kuwa dhana tu miongoni mwa wa-Tanzania wengi. Ukweli ni kuwa, ingawa una dosari za hapa na pale, na athari mbaya za hapa na pale, huu mtandao umekuja kama baraka. Mtandao umepunguza au kuondoa tofauti zilizokuwepo kabla katika uwezo wa watu mbali mbali kusambaza taarifa na maoni, au kutangaza shughuli zao kama vile biashara.
Kwa mfano, kwa kutumia nyenzo kama blogu, tovuti, au Facebook, mfanyabiashara mdogo, auzaye mahindi mjini Songea au Tunduma, au yule auzaye vinyago Mtwara, anaweza kutangaza biashara yake kwa ulimwengu.
Mtandao umeleta urahisi wa aia nyingine pia. Leo hii, umuhimu wa kujenga jengo linaloitwa duka, au kukodi chumba cha kukitumia kama duka, umepungua sana. Mtu unaweza ukawa na bidhaa zako nyumbani mwako au katika ghala yako, na ukafungua duka mtandaoni.
Mimi, kwa mfano, ni mwandishi wa vitabu. Ninauza hivi vitabu. Lakini sina nyumba au chumba kinachoitwa duka. Vitabu ninavichapisha mtandaoni. Bofya hapa. Au, kwa usahihi zaidi, niseme kuwa miswada ya vitabu hii nimeihifadhi mtandaoni, na mtu anapoagiza nakala, ndipo mitambo inachapisha nakala iliyoagizwa au nakala zilizoagizwa tu. Sivioni hivi vitabu wanavyoagiza wateja, lakini nimefungua duka huko huko mtandanoni. Bofya hapa. Wateja wananunua bila mimi kuwaona au kuwafahamu.
Katika maduka ya jadi, mwuzaji na mteja wanakutana, au wanasiliana kwa simu au barua. Mteja wa duka la mtandaoni kama hili langu, hahitaji kuwasiliana na mwenye duka. Yeye anafungua kompyuta, anaingia hapo dukani na kununua anachotaka, kwa kutumia "credit card" na kwenda zake. Wewe mwenye duka unapofungua kompyuta na kuangalia duka lako la mtandaoni, utaona kuwa bidhaa imenunuliwa, bila kumjua aliyenunua. Lakini malipo yako yanakuwa yameshaingia.
Siku hizi, watu wengi wenye maduka ya jadi au biashara za jadi wanaziweka mtandaoni pia. Ni njia ya kuwafikia wateja duniani kote. Mtu akiangalia duka hili la mtandaoni akapenda kununua kitu, anawasiliana na mwenye duka, kwa njia itakayokuwa imetajwa, iwe ni barua pepe, simu, au faksi. Au, kufuatana na utaratibu alioweka mwenye duka, mteja anatoa malipo hapo hapo anapoamua kununua kitu fulani. Jukumu la mwenye duka ni kumfungashia na kumpelekea mteja hicho alicholipia.
Kwa maana hiyo, biashara ya aina hii inahitaji uaminifu. Hili si jambo la kuongelewa. Ni ukweli usiopingika. Mwenye biashara makini anazingatia umuhimu wa kumridhisha mteja daima, kwani hii ndio siri ya mafanikio katika biashara. Mteja aliyeridhika na kufurahia huduma mahali fulani anawaambia wenzake. Huduma bora huzaa wapiga debe na kumneemesha mwenye biashara. Lakini mteja asiyeridhika naye atawaeleza wengine, na kusambaa kwa habari hii ni sumu kwa biashara. Wafanya biashara wetu wengi hawaelewi madhara ya kumnyanyasa mteja. Biashara yao inapoanguka, wanatoa visingizio kama vile kurogwa na washindani wao.
Ni muhimu sana wafanyabiashara wetu Tanzania waangalie suala hili la kuingia mtandaoni. Baadhi, kama vile kwenye sekta ya utalii, wanazo tovuti. Lakini kwa jinsi tekinolojia ya mtandao inavyozidi kupanuka na kusonga mbele, na kwa jinsi ilivyo na manufaa, ni vizuri wengine wajiunge na kuwa nayo sambamba.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
2 comments:
Ahsante sana Prof Mbele kwa somo zuri kama hili. Hakika mtandao una faida chanya nyingi. Ni wajibu wetu Watanzania kuamka sasa na kuchangamkia maendeleo ya teknolojia kwa manufaa.
Ndugu Mtanga
Shukrani kwa ujumbe wako. Hayo mawili matatu ninayoandika ni baadhi ya yale ambayo nayaandaa kwa ajili ya warsha nitakazoendesha hivi karibuni kule Bongo: tarehe 12 Juni Tanga; tarehe 3 Julai Arusha, na kadhalika.
Niko katika maandalizi makali, kwa kusoma na kufanya mihadhara hapa Marekani, ili nitakapotua Bongo, nimwage sera zilizoenda shule :-)
Post a Comment