Wednesday, March 17, 2010

Naishangilia Zanzibar

Siku kadhaa zilizopita nilipata fursa ya kusikiliza hotuba aliyotoa Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Shariff, kule Uingereza, akielezea makubaliano yaliyofikiwa baina yake na Rais wa Zanzibar, Mheshimiwa Amani Karume. Bofya hapa.

Nimeipenda sana hotuba ile, kwa jinsi ilivyojaa kumbukumbu, mawazo, tathmini na mawaidha kuhusu siasa Zanzibar. Nimevutiwa na jinsi Zanzibar ilivyofikia hatua ya kutathmini maana ya mfumo wa siasa ambao umetumika kwa yapata nusu karne na wakauona kuwa una dosari na ni chanzo cha matatizo. Mfumo huo ni wa vyama vya siasa.

Mimi mwenyewe nimehoji sana mantiki ya dhana nzima ya chama au vyama vya siasa. Mwaka jana niliandika makala nikihoji kama chama cha siasa au vyama vya siasa ni kitu cha lazima katika kujenga demokrasia. Nilisema kuwa tumeiga hii dhana kikasuku, na tunashinikizwa na mataifa mengine. Nilitamka kuwa labda kuna umuhimu wa kuangalia uwezekano wa kujenga demokrasia bila chama au bila vyama. Bofya hapa. Mawazo yangu, ambayo yanahoji mambo tuliyozoea, katika siasa, uchumi, utamaduni, elimu na kadhalika, yamo katika kitabu cha Changamoto.

Nimefurahi kusikia maelezo ya Maalim Seif kuhusu tathmini waliyoifanya Zanzibar, hadi wakafikia hatua ya kujenga ushirikiano baina ya CUF na CCM, na kuondokana na historia ya uhasama, kwa ajili ya maslahi ya Zanzibar. Wamefanya uamuzi wa maana, na nimefurahi kuona jinsi wanavyojipanga kuunganisha nguvu za wa-Zanzibar wote, walioko nchini na nje ya nchi, ili wajenge Zanzibar, ambayo zamani ilikuwa na historia na heshima kubwa duniani.

Naamini kuwa kwa Zanzibar kuchukua uamuzi huu, sote tutafaidika. Kuimarika kwa Zanzibar ni neema kwa Muungano. Wale waliokuwa wanaitumia Zanzibar kwa manufaa yao, wakawa wanaendekeza siasa za mfarakano, ndio pekee watakaoambulia patupu. Wale waliokuwa wanaendekeza ubabe wa kutumia nguvu ya chama au vyama, wamepewa somo kubwa. Nategemea watajifunza.

Hotuba hii ya Maalim Seif nimeona ni muhimu kuliko zote ambazo nimewahi kuzisikia kutoka kwa wanasiasa wetu tangu aondoke Mwalimu Nyerere.

5 comments:

bibi Alesha said...

Kaka Mbele,

Ingawa mimi sijasikiliza hiyo hotuba, naungana na wewe kwa kila neno. Mtu ukijiuliza chama kinawezaje kuleta maendeleo ya nchi kama si watu wenyewe na mawazo yao ya kuangalia mbele. Huwezi kutumia chama kama biblia kuleta maendeleo kwa watu. Hata biblia yenyewe ukiisoma sana unaona kwamba mambo mengi ni tungo tu wala haziingii akilini. Neno SERA za vyama ndo ubabe ambao umetufikisha katika hali tuliyo nayo nchini.

Niliangalia video ambayo ilipostiwa na mtu kwenye blog ya Kaka Michuzi, nilitaka kulia. Niliangalia chinsi watu walivyochinjwa kama kuku Pemba wakati wa mapinduzi. Ukiiangalia huwezi kushiriki siku ya Mapinduzi! Aibu sana hasa ukizingatia nchi kama Tanganyika iliyopata uhuru bila kumwaga damu.

Tusubiri hili la mgombea binafsi tuone kama anaweza kutokea mtu wa kutuvusha kwenye hili lindi la kashfa na wizi.

Lulu, NY

Mbele said...

Shukrani kwa ujumbe huo. Kutafuta njia au namna mpya za kufikiri, namna mpya ya kuangalia mambo, ni jambo linalonivutia sana, na ndio msingi wa maendeleo. Nami nina mawazo kama yako, kuhusu suala la mgombea binafsi. Ni mtazamo mpya katika siasa, tofauti na ilivyozoeleka.

Anonymous said...

Shikamoo Dr. Mbele!

Nilivutiwa uliposema:"Nilisema kuwa tumeiga hii dhana kikasuku, na tunashinikizwa na mataifa mengine."
Hayo mataifa mengine ni yepi?Inanifurahisha sana kwamba hotuba yenyewe ilitolewa Uingereza ambayo pengine itakua baadhi ya nchi amazo tuliziiga kikasuku.Naam,tena jijini London,kitovu na makao makuu ya mkoloni namabri moja: Malkia wa Uingereza aliyetawala miaka yote ile".Kama haya yote sio ukoloni mambaleo sijui ni nini tena(Maalim nae namnakuu:"Waziri wa mambo ya ndani wa Norway alitoa hongera").

Kuhusu,"Nilitamka kuwa labda kuna umuhimu wa kuangalia uwezekano wa kujenga demokrasia bila chama au bila vyama." kule kijijini kwa maza,Mdunduwalo,Songea nilishawahi kushuhudia jinsi wakina mama na vyama vyao vilivyokuwa vinawajibika kutetea na kubuni mbinu za kuzalisha vijisenti kwao (wao walikua na chama cha kupiga pombe).Saa tuseme kwamba nao waliiga kikasuku sijui?

Binafsi naona lazma tukubali kwamba chanzo cha matatizo yote- iwe ya siasa au pengine -sio "vyama" bali ni watu ndani ya vyama.Mfumo wowote ule,uwe Udikteta,Demokrasia,Umwenye au chama kimoja vyote vina upungufu.Tunachoona hapa ni Maalim akifanya juu,chini kuelezea makubaliano ambayo wanachama wa CUF hawakuyatathmini wala kukubaliana nayo. Nadhani,Tanzania Daima wameibua siri wanaposema kwamba:

"Uchunguzi wa kina uliofanywa na Tanzania Daima Jumatano, umebaini kuwa chanzo cha makubaliano ya ghafla ya viongozi hao imetokana na shinikizo kutoka nchi za Jumuiya ya Ulaya zilizotishia kuwafikisha katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC), The Hague nchini, Uholanzi viongozi hao kama damu itamwagika tena katika uchaguzi mkuu ujao.

Naam, shinikizo lilitoka huko,huko makala hii ilipoandikwa:majuu!!

Mbele said...

Ndugu Wachumi

Katika mada yangu, neno chama au vyama lina maana ya chama au vyama vya siasa. Halijumlishi vitu kama vyama vya kuzikana au vya wagema ulanzi.

Katika makala hii fupi kwenye blogu, nimetoa dokezo tu la fikra na mtazamo wangu. Na nimetaja pia makala ambayo mtu anaweza kufuatilia zaidi. Nimetaja pia kitabu changu, ambacho kinaelezea kwa upana zaidi mawazo yangu. Mwenye kutaka kujua mtazamo wangu kwa upana zaidi, apitie maandishi hayo.

Mtu akipitia maandishi hayo, ataona mtazamo wangu kuhusu suali unalouliza, kama nchi zinazotushinikiza ni zipi. Nimeliongelea hilo suala.

Kuhusu suala la vyama vya siasa na magomvi nimeliongelea zaidi katika maandishi niliyotaja hapo juu, na pia katika makala hii hapa. Humo utaona nimeelezea jinsi vyama vya siasa vinavyohujumu amani nchini.

Kama kuna gazeti limeandika habari fulani, hii ni sawa kabisa. Lakini kuwepo kwa habari kwenye gazeti fulani si ndio mwisho wa mjadala, si mwisho wa utafiti na tafakari.

Kwa maana hiyo, sisi wengine, na sisi wote, tunao uhuru na wajibu wa kuendelea kutafakari suala hili la makubaliano ya Zanzibar na kutoa mawazo yetu bila vipingamizi wala visingizio.

Anonymous said...

Naam Profesa Mbele,ni kweli "sisi wengine, na sisi wote, tunao uhuru na wajibu wa kuendelea kutafakari suala hili".Binafsi nimevutiwa na barua ya Prof.Shivji kuhusu jambo hili (Unaweza kusoma barua hiyo kwenye Blogu la Dr Faustine:http://drfaustine.blogspot.com/2010/01/barua-ya-profshivji-kwa-rais-karume-na.html )

Asante,

Majaliwa
http://wachumi.blogspot.com/

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...