Sunday, July 10, 2011

Nimeingia Tena Duka la Half Price Books

Jana, nikitokea mkutanoni Minneapolis, nilipita mjini Apple Valley, nikaingia duka la Half Price Books, kama kawaida. Ilikuwa siku nzuri, jua linawaka na hali ya hewa ya joto la kupendeza. Kama kawaida, niliwaona watu wengi dukani, watoto hadi wazee, wake kwa waume, wakiwa katika kuangalia vitabu, kusoma, na kununua.


Wakati wote, watu wanaingia na kutoka. Kwa utaratibu wa maduka ya Half Price Books, ukiwa na vitabu unavyotaka kuviuza, unavileta, na Half Price Books wananunua. Ndio maana daima utawaona watu wanaingia na mizigo ya vitabu, wakati wengine wanatoka na vitabu walivyonunua.

Kama kawaida, ninapokuwa katika duka la vitabu namna hii, ninajiwa na mawazo mengi. Jana, wakati nawaangalia watoto waliokuwemo katika duka hili, nilikumbuka habari niliyoisoma wiki hii kuhusu fiesta mjini Iringa.

Taarifa ilisema kuwa katika fiesta hiyo, kulikuwa na watoto hadi usiku wa manane. Nilihuzunika. Wakati wenzetu wanawalea watoto wao katika usomaji wa vitabu, sisi watoto wetu tunawalea katika fiesta hadi usiku wa manane. Huku Marekani watoto wanaenda kulala kwa wakati unaofaa; hawaonekani kwenye shughuli za usiku namna hiyo.

5 comments:

emu-three said...

Profesa, labda vitabu vingegeuzwa kuwa `mziki' au `mikanda ya filamu' hapo Watoto wa Kitanzania wangesoma sana...huamini hili, watu wengi hapa nchini, ukiwaambia kusoma kitabu, wanasema `sina muda, nipo busy kweli...'
Hongeara sana Profesa kwa juhudi zako hizo, labda ipo siku jamii yetu itaamuka!

Mbele said...

Shukrani, emu-three, kwa ujumbe. Kweli, wa-Tanzania hawaishiwi visingizio kwenye masuala haya na mengine. Ukiwauliza kwa nini hawanunui vitabu watasema hawana hela. Lakini hela za bia wanazo sana.

Ukiwauliza kwa nini hawana ajira, wako wa-Tanzania ambao watakuambia wa-Kenya wanatuonea. Hizo hoja nilizosoma katika blogu ya Michuzi miezi mingi kidogo iliyopita, na hao wa-Tanzania walikuwa hata wanaiomba serikali ilinde ajira kwa wa-Tanzania.

Wengine watakuambia kuwa hawajasoma kwa sababu ya mfumo Kristo. Ninapita sana katika maktaba, lakini sioni kama kuna utaratibu wa kuwazuia baadhi ya watu kuingia humo. Tangu zamani imekuwa hivyo.

Wengine ndio hao unaoongelea, wanaosema hawana muda wa kusoma vitabu, wana shughuli nyingi mno. Lakini ukiwaalika baa ukawanunulie ulabu, hakuna atakayekuambia hana muda.

Wiki hii nitatua Tanzania. Nina hakika kuwa natawaona maelfu ya wa-Tanzania vijiweni katika miji yote nitakayopita. Lakini kwenye suala la kusoma vitabu watasema hawana muda, wana shughuli nyingi mno.

Nilihudhuria warsha kadhaa huku Marekani kwa ajili ya wajasiriamali, na huko nilijifunza kuwa kumbe muda tunao sana, ila tu hatujatathmini suala hilo. Kwa mfano, mtu anakaa nyumbani akiangalia televisheni masaa, mambo ambayo hayana tija. Lakini hatambui kuwa akiacha kuangalia vipindi hivyo, tayari anakuwa ameshaokoa masaa mengi ya kujifanyia shughuli za maendeleo.

Miaka hii mimi huwa naangalia televisheni mara moja moja tu, na baa siendi kabisa. Tatizo ni pale ninapokuwa Tanzania, maana hapo hata kama hupendi, washikaji wanakuswaga na kukufikisha baa ukajumuike nao :-)

tz biashara said...

Profesa nipo nje kidogo ya mada kwa sababu nimeisoma ishu ya kujiandaa kwa kutengeneza vitambulisho.Ishu ni kwamba vitambulisho ni muhimu lakini je ni wakati muafaka kwa kutumia mamilioni ya dola kutengeneza hivyo vitambulisho.Hapa uingereza waliikataa kutokana na gharama ambayo ingeweza kusaidia secta muhimu.Na ukiangalia kwetu hatuna umeme na maji na hata watoto wetu waliobahatika kwenda shule hawana vitabu wala madawati na wanakaa sakafuni.Hii ishu unaionaje au imekaaje na isijekuwa yale ya rada sasa yanaangukia ktk ID card.

Mbele said...

tz biashara, naafikiana nawe. Angalau kwa wakati huu, ambapo nchi inakabiliwa na uwezekano wa njaa, vitambulisho haviwezi kuwa kipaumbele kikubwa namna hii. Na masuala ya elimu, afya, umeme, bado yanatukabili.

Anonymous said...

Sad watoto wetu tumewaharibu wenyewe...Wazazi ndio wakulaumiwa kumwacha mtoto mpaka usiku wa manane...

Mimi nina nieces na nephew nawaambia hata wasome blogs tu hawataki wako radhi waingie kwa Facebook siku nzima kucheck status za wenzao. Mimi nawaambia social comparison zitawaua. Mtu una rafiki 600 hardly unawafahamu 40 sasa ukiona hao watu wengine ambao hata huwajui wanasema kitu fulani kinakuhusu nini? Na wengine wanaweka status za uongo. It is just so sad...

lakini yote haya ni wazazi wanachangi...wakitoka kazini wako baa wakirudi nyumbani watoto wamelala kesho siku inaenda hivyo hivyo ...Angalia wazazi wa huku jinsi wanavyotumia muda wao mwingi kwa watoto wao. Na pia wakiona mzazi anasoma ktabu nao wanakua na hamu ya kusoma sasa wazazi hawataki hata kusoma..Wengine toka wamemaliza shahada zao na kitabu wakasahau...Kumbe hawajui elimu haina mwisho...

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...