Friday, June 8, 2012

Mama Shakila, Mwimbaji Maarufu

Mama Shakila ni mwimbaji maarufu wa taarab. Imepita miaka yapata 22 tangu nilipobahatika kumtembelea na kuongea naye kuhusu maisha yake na masuala ya sanaa na jamii. Laiti ningekuwa nimepata fursa zaidi ya kuongea naye hadi kuandika makala za kiwango cha juu kitaaluma, au hata kitabu  cha aina hiyo. Mama Shakila, sawa na wasanii wetu wengi, ametoa mchango mkubwa kwa jamii yetu na ulimwengu kwa ujumla. Lakini, jamii yetu ina tatizo la kutowaenzi watu hao ipasavyo. Kufanya utafiti na kuandika habari zao na tathmini ya mchango wao ingekuwa namna moja ya kuwaenzi, pia kuhakikisha kuwa wanapata kipato wanachostahili kutokana na kazi zao. Ingebidi wasomi wawe wanaandika makala na vitabu kuchambua kazi za wasanii hao; wanafunzi vyuoni wawe wanaandika tasnifu, na pawe na mijadala, makongamano, ya kuchambua mchango wa watu hao. Lakini jamii yetu, pamoja na kufaidika kutokana na juhudi za watu hao, ina jadi ya kutowajali kimaslahi, na kisha kuwasahau.

4 comments:

Emmanuel said...

Professa umesema ukweli ambao watu wanaujua lakini wanakaa nao kimya. Ni wakati watanzania tukaenzi kazi za wenzetu hata kwa kiwango kinachostahili.

Huu mtindo ndio unaotufanya tuendelee kuwepo kuwepo tu hapa duniani maana hamna motisha wala nini

Mbele said...

Ndugu Emanuel, shukrani kwa mawaidha yako. Tukiwaorodhesha wasanii wetu maarufu wa zamani hadi leo, tutaona jinsi tulivyopotoka.

Tippu Tip, hatumkumbuki. Shaaban Robert, mwandishi wa riwaya, mashairi, tenzi, na insha, hatumkumbuki. Matias Mnyampala na Akilimali Snow White hatuwakumbuki. Saadani Abdi Kandoro hatumkumbuki. Kadhalika Mbunda Msokile ambaye aliandika vitabu vingi.

Tukienda kwa waimbaji na wanamuziki, ni hivyo hivyo. Siti binti Saad, Mbaraka Mwinshehe, Patrick Balisidya ni mifano michache.

Angalau kumekuwa na juhudi kidogo za kumwenzi mtunzi na mwigizaji wa filamu Steve Kanumba. Lakini tungekuwa makini, tungeanzia nyuma zaidi. Nani anayekumbuka kwamba Rashidi Kawawa (Simba wa Vita) alikuwa kati ya waigizaji maarufu wa filamu wa mwanzo hapa nchini?

Nani anawazia kumwenzi Mzee Morris Nyunyusa, mpiga ngoma nyingi kwa mpigo?

Tunaweza kuandaa orodha ndefu, na tukaona tatizo ni kubwa.

tz biashara said...

Profesa Mbele leo umenikumbusha mbali sana na huezi amini kama huyu mama kama sikosei nimemzungumzia wiki iliopita.

Kwa hakika hakuna tunachokijali vya zamani ila vilivo sasa ndio vinaonekana vizuri bila kukumbuka waliopita na utunzi wao au mchango wao.

Huyu mama alikuwa anaimba na sauti ya kumtoa nyoka pangoni.Aliimba kwa fani alioichagua yeye bila kujali nani anamthamini.Nadhani humuijia siku akisikia wasanii wanapokea tuzo na kujiuliza maswali kwamba kuimba kwake kote hakuna aliejitokeza na kumthamini japo kwa zawadi.

Nadhani ifike siku hao watayarishaji wa mambo kama haya wangejaribu kuwakumbuka watu wa zamani kwa michango yao ya zamani kwa kuwapa tuzo na kuwasaidia kimaisha.

Ili kuwapa changamoto wengine vizazi vijavo na kuwajengea maisha yenye kuwapa mtazamo mpya.Tunao waimbaji,watungaji vitabu,waigizaji na wachoraji na wengine wengi wenye fani mbalimbali.

emuthree said...

Huo ni ukweli, na nimeshangaa kuna waigizaji wanapenda kuigiza watu waliokuwa mashuhuri, ama waimbajii au wacheji mpira, ambao walikuwa wakifanya vizuri, sasahali zao ni mbaya,....wanaigiza kwa kejeli!
Tuwaenzi watu kama hao,....na tuwasaidie kila inavyowezekana,

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...