Kila siku ni ya pekee, lakini kuna siku ambazo ni za pekee zaidi. Leo nilienda Luther Seminary, St. Paul, kuonana na wachungaji wawili, ambao ni Rev. Dr. Falres Ilomo (aliye katikati pichani) na Rev. Dr. Andrea Mwalilino (hapo kulia). Mchungaji Mwalilino, ambaye tumefahamiana kwa miaka kadhaa, alikuwa ameniarifu kuwa kuna huyu mgeni kutoka Tanzania, ambaye yuko kwa kipindi tu hapa Luther Seminary. Tulitafuta fursa ya kuonana, na leo imewezekana.
Mchungaji Mwalilino, ambaye alihitimu shahada ya uzamifu Luther Seminary, tuko wote hapa Minnesota, ingawa miji mbali mbali. Mgeni wetu, ambaye alihitimu shahada ya uzamifu katika Chuo Kikuu cha Augustana, Ujerumani, ni mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Tumaini, Iringa. Mimi mwenye blogu hii nilihitimu shahada ya uzamifu katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison. Mjadala wetu ulikuwa wa kiwango cha juu kitaaluma. Tumeongelea utafiti katika tamaduni na dini za jadi za wa-Afrika, lengo moja muhimu likiwa ni kutafakari namna ya kuziweka dhana na falsafa za jadi za ki-Afrika kwenye uwanja wa mijadala na uchambuzi katika dunia ya leo, tukizingatia kuwa wa-Afrika wa tangu zamani wana mchango ambao unastahili kutambuliwa na kutumiwa.
Katika utafiti huo, tuna wajibu wa kuangalia lugha, kwani lugha ndio chombo kinachobeba na kuwakilisha dhana mbali. Utafiti wa lugha utatuwezesha kujua sio tu dhana za ndani katika falsafa za wa-Afrika, bali pia namna ya kuwasilisha kwa wa-Afrika mafundisho ya dini yetu ya u-Kristo ambayo yalikuja kwetu kutoka kwenye lugha za kigeni. Suala hilo si kwa u-Kristo tu, bali pia kwa u-Islam. Tumebaini kwamba kutokana na tofauti za lugha, dhana nyingi katika dini hizo hazijaelezwa au kueleweka ipasavyo. Tutawezaje kuziwasilisha kwa wa-Afrika, dhana za hizo dini, ambazo huko zilikotoka zilikuwa katika lugha ambazo sio zetu? Hili ndilo suala, na inabidi tuzame katika kulitafakari. Tafakari hii ni lazima ifanyike na iwe endelevu. Mada hii tumeiongelea na kuichambua kwa karibu saa mbili tulizokuwa pamoja, na sote tunakiri tumefanya kazi nzito, ya kufikirisha. Tumekubaliana kuendeleza tafakari na mawasiliano siku za usoni.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
4 comments:
safi sana!!inapendeza kwa kweli.
Dada Yasinta, shukrani.
Ngoja nikupe mfano wa hili tatizo. Sisi wa-Katoliki tuna usemi, "mimi ni mzabibu." Sasa tujiulize, je m-Nyasa wa Lundu na m-Ngoni wa Mgazini wanaujua mzabibu? Kuna uwezekano au umuhimu wa kuwaeleza dhana husika kwa kutumia tamathali zilizomo katika lugha zao ili fundisho la dini lieleweke kwao na liwe na maana kabisa kufuatana na utamaduni wao?
mheshimiwa Profesa Mbele asante sana kwa mada hiyo na hapo umenikumbusha huo mti wa mzabibu ni kweli huyo mnyasa au mhaya mimi ninayeandika hapa huo mzabibu sijui kama mababu zetu huko kwa wahaya wanaujua lakini bado na sisi katika kufanya ibada zetu(matambiko)tulikuwa na miti mfano kama unataka kufanya tambiko ni lazima mbele ya nyumba yako ya ibada yaani"msonge"uweke mti unaoitwa "ORUBUGU/O" YAANI HUU MTIkaramayake ni kwamba unaweza kuutoa ngozi au gambalake na kufanya shuka la kulalia zaidi ya mara sita baada ya hapo ndio mambo mengine yanaendelea yaa huo tunauita mti wa KAZOBA KA NYAMHUNGA,YAANI MTI WA MUNGU MUUMBAJI
Ndugu Anonymous, shukrani kwa mchango wako, mfano hai kutoka katika utamaduni wa wa-Haya. Ni mfano mzuri kabisa.
Hili suala ni zito, nami niliwahi kushiriki katika kulifafanua kwenye mkutano fulani wa wa-Luteri, kama nilivyoelezea hapa.
Post a Comment