Thursday, December 29, 2016

Vitabu Tulivyosoma Mwaka 2016

Zikiwa zimebaki siku mbili tu kabla ya kwisha mwaka 2016, nimeona wa-Tanzania kadhaa wakijitokeza katika mtandao wa Facebook na kutaja vitabu walivyosoma mwaka huu. Jambo hili limenifurahisha, nikizingatia kuwa nimekuwa nikihamasisha usomaji wa vitabu, kwa kutumia blogu yangu hii, blogu za wengine, na pia katika kitabu changu, CHANGAMOTO: Insha za Jamii.

Ninawapongeza watu hao kwa kuonyesha mfano mzuri. Ninawapongeza pia wasomaji waliojitokeza na kuchangia suala hili kwa namna mbali mbali, kama vile kuvijadili vitabu hivyo, kuulizia upatikanaji wake, au kupendekeza vitabu vingine. Kuhusu upatikanaji wa vitabu, watu wamepeana taarifa za maduka ya vitabu, na pia upatikanaji wa vitabu pepe mtandaoni. Ni jambo la kuvutia kwamba kuna wa-Tanzania wanaotambua matumizi ya manufaa ya tekinolojia ya mtandao.

Mazungumzo haya yameonyesha mambo kadhaa. Jambo moja ni kuwa wako wa-Tanzania wanaojibidisha kusoma vitabu. Jambo jingine ni kuwa wanasoma vitabu vya aina mbali mbali, kama vile vya siasa, ujasiriamali, fasihi, na maendeleo ya jamii au ya mtu binafsi. Vile vile wanasoma vitabu vya waandishi wa mataifa mbali mbali, vya ki-Swahili na vya ki-Ingereza. Jambo jingine ni kuwa wahusika wameonyesha moyo mkubwa wa kusaidiana, kama vile kwa kufahamishana vitabu bora na hata kuazimishana vitabu.

Ninawaenzi watu hao. Huenda wakawa chachu ya kustawisha utamaduni wa kusoma vitabu nchini Tanzania. Laiti watu wengi zaidi wangejumuika katika safari hii. Laiti kama watu maarufu nchini mwetu, kama vile wanasiasa na wasanii, wangejiunga na kuwa wahamasishaji wa usomaji wa vitabu. Kutokana na mvuto wa wasanii wetu, kwa mfano, wangeweza kuwa wahamasishaji wa watoto na vijana katika kupenda kusoma vitabu.

Kwa upande wangu, naona sihitaji kuorodhesha vitabu nilivyosoma mwaka 2016. Mara kwa mara, katika blogu hii au blogu ya ki-Ingereza, ninaandika taarifa za baadhi ya vitabu ninavyosoma. Vingine ni vile ninavyofundisha chuoni St. Olaf, na vingine ni vile ninavyojisomea mwenyewe. Ninapoandika  taarifa, ninajitahidi kuelezea upekee au ubora wa vitabu hivyo.

2 comments:

Ndugu Nkwazi N Mhango said...

Ndugu Mbele,
Acha nitume fursa hii kukutakia mwaka mpya mwema na wenye mafanikio wewe na familia yako, marafiki na ndugu na jamaa. Huwa naguswa na ukereketwa wako wa elimu hasa usomaji vitabu. Kama mtunzi anayeibukia, huwa Napata faraja na nguvu. Sitaki nijisifu, mwaka huu nimesoma vitabu vichache ila machapisho (journals) nyingi. Pia nimekamilisha mswaada mmoja ambao Inshallah unaweza kutoka mwakani juu ya Ugaidi na namna unavyotumika kuikalia Afrika kijeshi. Mwaka unaoisha nilifanikiwa kuchapisha vitabu viwili yaani Africa's Best and Worst Presidents: How Neocolonialism and Imperialism Maintained Venal Rules in Africa na Psalm of the Oppressed (Ushairi wa kiingereza). Pia nilijaliwa kuchapisha Sura (Chapters) tatu kwenye vitabu tofauti vya kiada yaani Chapter One Democracy, Violence and Peace in One House: The Dilemma of Post-colonial Africa, Myths of Peace and Democracy? Towards Building Pillars of Hope, Unity and Transformation in Africa na Chapter Five Violence, Power, Politics and (Anti-) development in Africa na kukamilisha moja ambayo itatoka mwaka ujao. Pia mwaka unaokwisha niliweza kuboresha mswaada wangu juu ya vita ya uchumi, ukaliwaji wa DRC na matatizo ya kijinsia ambao nao Mungu akitujalia huenda nikaumaliza mwakani.
Naungana na ndugu Mbele kuwachakatiza watanzania kujisomea vitabu hata ikiwezekana kuandika. Hakuna zawadi inayodumi milele kama kitabu au chapisho hata barua kama itatunzwa. Nawatakieni wote heri ya mwaka mpya.

Joseph said...

Ndugu Mango

Shukrani kwa ujumbe wako murua, unaothibitisha kujituma kwa hali ya juu. Maisha ni mafupi, na wewe unatuonyesha mfano kuwa maisha tuliyopewa ni dhamana na fursa adimu. Nashukuru umeweka ujumbe wako, ambao pia ni fundisho, hapa kwangu kwa ufasaha kiasi kwamba sina la kuongezea. Nakutakia kila la heri kwa mwaka mpya.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...