Friday, August 18, 2017

Tumesoma "Confession of the Lioness"

Tumo katika wiki ya mwisho ya kozi ya "African Literature," ambayo ni kwa kipindi hiki cha kiangazi. Kati ya vitabu ambavyo tumesoma ni Confession of the Lioness, riwaya ya Mia Couto wa Msumbiji. Couto ni mmoja wa waandishi maarufu kabisa Afrika na ulimwenguni, ambaye amepata tuzo za kimataifa kwa uandishi wake, ikiwamo tuzo ya Neustadt.

Mia Couto anaandika kwa ki-Reno. Ninasoma na kufundisha tafsiri za ki-Ingereza. Kwanza nilifundisha riwaya yake The Tuner of Silences hapa chuoni St. Olaf nikaipenda sana. Niliifundisha tena katika muhula mwingine. Kutokana na hilo, niliamua kufundisha riwaya yake nyingine. Ndipo nikachagua Confession of the Lioness, baada ya kusoma taarifa zake mtandaoni.

Riwaya hii inasimulia habari za eneo la kaskazini mwa Msumbiji, katika jamii ya wa-Makonde. Jamii inaishi kwa hofu na wasi wasi kutokana na kuwepo kwa simba ambao huzunguka na hushambulia watu na mifugo. Wasi wasi umechanganyika na imani za kishirikina kuhusu simba hao. Je, ni simba kweli, au ni simba wa kutengenezwa kiuchawi? Hilo ni moja ya maswali yanayosumbua jamii hii.

Kwetu wa-Tanzania, tumekuwa tukishuhudia hali hiyo hiyo katika wilaya ya Tunduru, ambayo inapakana na Msumbiji. Mimi ni mwenyeji wa mkoa wa Ruvuma, ambao unapakana na Msumbiji. Confession of the Lioness ilinigusa kwa namna ya pekee, kwa jinsi utamaduni unaoelezwa humo unavyofanana na ule wangu wa ki-Matengo. Kuna hata maneno kadhaa ya kilugha, ambayo yanafanana na yetu. Sijawahi kusoma riwaya maarufu kama hii ambayo mazingira yake ni ya karibu namna hii na mahali nilipozaliwa na kukulia.

Kama ilivyo katika The Tuner of Silences, katika Confession of the Lioness, Couto anasisimua akili, kwa namna ya pekee. Analeta maajabu katika mtazamo na maelezo ya mambo. Hiyo dhana ya simba, anaipeleka mbali kwa kutufanya tuitafakari kifalsafa. Wakati tunahangaika na simba wazururao porini, labda simba wamo katika nafsi zetu binadamu. Tusijiziuke kuogopa simba wa porini tukashindwa kutambua simba ndani yetu. Binadamu huenda ndio simba wa kuogopwa zaidi.

Mbinu moja mahsusi ya uandishi anayotumia Couto ni ile ambayo inajulikana kwa ki-Ingereza kama "defamiliarization." Kwa mfano, ni jambo la kawaida kwa wawindaji kujipiga picha wakiwa na mnyama waliyemwua, Couto analielezea jambo hili kwa namna ya kutufanya tulione kwa mtazamo mpya.

Take a photo of me next to the trophy, the administrator insists, cutting a vain pose, one foot on the animal. It's an illusion I don't bother to dismantle: What is there is no longer a lion. It is empty plunder. It isn't anything more than a useless shell, a piece of skin stuffed with nothingness (uk. 189).

Nilipojadili kifungu hiki darasani, pamoja na kukielezea kama mfano wa "defamiliarization," niliingia pia katika falsafa, kwa kunukuu kauli ya Macbeth, anapoelezea maisha na harakati za binadamu kama si chochote bali

...It is a tale
Told by an idiot, full of sound and fury
Signifying nothing.

(Shakespeare, Macbeth, Act 5, Scene 5).

Suala la watu kujigeuza simba nililielezea darasani kama sehemu ya jadi yenye historia ndefu katika masimulizi na fasihi ya ulimwengu. Humo, watu hugeuka wanyama, au kitu kingine. Mifano ni Metamorphoses, ya Ovid, The Golden Ass, ya Apuleius, Metamorphosis, ya Kafka.

Confession of the Lioness inatufanya tufikirie maana ya simba. Simba sio tu wale wanyama wanaoishi porini. Simba pia ni dhana ya kifalsafa ku yamwelezea binadamu, kwani tabia ya binadamu inaweza kufanana na ya simba. Kwa mfano, katika riwaya hii kuna suala la wanaume kuwanyanyasa wanawake, kiasi kwamba wanaume hao wanakuwa kama simba. Confession of the Lioness, ni utungo wa aina inayoitwa "allegory" kwa ki-Ingereza.

Ninaipendekeza riwaya hii kwa dhati kwa wasomaji. Couto ana kipaji cha pekee cha kuandika hadithi ya kugusa hisia na kuamsha fikra. Haishangazi kuwa amejipatia tuzo na sifa kubwa ulimwenguni.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...