Tarehe 8 Agosti, nilikwenda Rochester, Minnesota, kuhudhuria mkutano wa bodi ya Rochester International Association (RIA). Tunakutana mara moja kwa mwezi. Katika ajenda ya tarehe 8, yalikuwepo mambo yanayonihusu moja kwa moja, ambayo ninapenda kuyaelezea hapa.
Moja ni kuwa wanabodi tuliohudhuria tuliulizwa na rais wa bodi, Brian Faloon, iwapo tutapenda kuendelea kuwa wajumbe mwaka ujao. Wote tulikubali. Mimi kama mwanabodi mpya kuliko wote, nilivutiwa na jinsi wajumbe walivyo na moyo wa kujitolea. Nilikubali kwa sababu ninathamini mchango wa RIA katika jamii. Kwa upande wangu, kutumikia RIA kumeniwezesha kufahamika katika mji wa Rochester. Kwa mfano, kupitia RIA niliweza kutoa mhadhara chuo kikuu cha Minnesota Rochester.
Pili ni kuwa RIA imesisitiza kuafiki pendekezo nililotoa siku zilizopita la kuonyesha filamu ya Papa's Shadow mjini Rochester. Bodi ilipendekeza kwamba onesho lifanyike kupitia maktaba ya Rochester. Tutafuatilia, ili filamu ionyeshwe hivi karibuni.
Jambo jingine ni kuwa mwanabodi Kristin Faloon aliwaeleza wanabodi kuhusu mhadhara niliotoa katika kikuu cha Winona, ambao yeye na mumewe Brian walihudhuria. Sikutegemea Kristin angeongelea tukio lile, lakini ilionekana wazi kuwa walifurahishwa na mhadhara ule, akasema kuwa walijifunza mengi. Kwa kuzingatia hadhi ya Brian na Kristin katika jamii, maoni yao yana uzito mkubwa. Nimewaandikia ujumbe kwamba sitawaangusha katika mihadhara ya baadaye.
Zaidi ya hayo, mkutano wa RIA umenifungua macho kuhusu taasisi zinazofanya shughuli zinazofanana na zangu katika kuendeleza maelewano baina ya watu wa tamaduni mbali mbali. Mbali ya Diversity Council-Rochester, ambayo niliifahamu, niligundua pia kuwa kuna kitengo katika Mayo Clinic kinachoshughulika na masuala ya kujenda na kustawisha mahusiano baina ya watu wa tamaduni mbali mbali. Ninatarajia kuwa tutakuwa na fursa ya kushirikiana kwa namna moja au nyingine.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
1 comment:
Hongera sana!
Post a Comment