Sunday, August 27, 2017

Vitabu Nilivyonunua Leo

Leo nilienda Mall of America. Nilipitia Apple Valley katika duka la half Price Books. Kama kawaida, niliangalia kwanza sehemu vinapowekwa vitabu vya Ernest Hemingway. Hapo nilinunua The Dangerous Summer, kitabu ambacho nilikifahamu kwa miaka. Nilijua kwamba kinahusu utamaduni wa Hispania wa "bull fighting." Nilijua pia kuwa hiki ni moja ya vitabu vya Hemingway ambamo alielezea utamaduni huu kwa umakini na ufahamu wa hali ya juu.

Kitu kimoja kilichonifanya ninunue kitabu hiki leo ni utangulizi mrefu ulioandikwa na James A. Mitchener, mwandishi ambaye nimemfahamu kwa jina kwa miaka kadhaa na nimeshaona baadhi ya vitabu vyake, ila sijawahi kuvisoma. Nilivyoanza kusoma utangulizi wake katika The Dangerous Summer, nilivutiwa sana na uandishi wake. Vile vile, nilitaka kujua anaeleza nini kuhusu kitabu hiki. Utangulizi wake umenipa hamu ya kusoma vitabu vyake.

Baada ya hapo, nilielekea vinapowekwa vitabu vya bei ndogo zaidi. Niliangalia kijuu juu vitabu vilivyojazana hapo, na ghafla nikaona kitabu kiitwacho Bamboo Among the Oaks, kilichohaririwa na Mai Neng Moua. Nilifurahi kukiona, kwani mwandishi alikuwa mwanafunzi hapa chuoni St. Olaf miaka ya tisini na kitu. Nilikuwa nimesikia habari za kitabu hiki, kwamba ni mkusanyo wa maandishi ya watu wa taifa la Hmong waliohamia Marekani.

Taifa la Hmong asili yake ni kusini mwa China na nchi za Cambodia, Laos, Thailand, na Vietnam. Wakati wa vita baina ya Marekani na Vietnam, jamii ya Hmong ilishirikiana na shirika la kijasusi la CIA la Marekani. Kwa mujibu wa mhariri wa Bamboo Among the Oaks, walifanya hivyo "to defend their own territory and way of life and to rescue American pilots downed along the Ho Chi Minh Trail."

Kwetu sisi wa-Tanzania, kutokana na mwelekeo wetu wa kishoshalisti, tulishikamana na nchi zilizokuwa na mwelekeo huo. Tuliunga mkono Vietnam ya Kaskazini chini ya kiongozi wao Ho Chi Minh. Hatukupendeza na hao waliosaidiana na Marekani, nchi ambayo tuliiona ya kibeberu. Kwa mtazamo huo, suala la jamii ya Hmong ni tata kwetu.

Marekani iliposhindwa, washindi, yaani Pathet Lao, walianza kulipiza kisasi dhidi ya jamii ya Hmong. Hii ndio sababu ya wao kukimbilia nchi zingine, kuanzia Thailand, na kisha nchi za mbali, kama vile Argentina, Australia, Canada, Ufaransa, Ujerumani, na Marekani. Katika jimbo la Minnesota, ambapo ninaishi, watu wa jamii ya Hmong ni wengi. Vijana wao wengi tunawafundisha chuoni St. Olaf.

Nimesikia mambo kadhaa kuhusu jamii hiyo nchini Marekani, hasa kuhusiana na tofauti baina ya utamaduni wao na ule wa Marekani. Kuna changamoto inayotokana na nia ya wazee kudumisha utamaduni wa jadi mwelekeo wa vijana wa kupendelea utamaduni wa Marekani.

Kwa mategemeo kwamba kitabu hiki, ambacho ni mkusanyo wa mashairi, hadithi, tamthilia, na insha, kitanipa mwanga zaidi kuhusu jamii hii, niliamua bila kusita kukinunua. Nilivutiwa na wazo kuwa kitanipa upeo wenye uhusiano na yale niliyoandika katika kitabu changu, Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...