Wednesday, October 15, 2008

Mwalimu Nyerere na Elimu


Mwalimu Julius Nyerere alikuwa mwalimu. Naamini ni sahihi kusema kuwa silika ya ualimu iliathiri siasa na matendo ya Mwalimu Nyerere kama kiongozi wa Tanganyika na hatimaye Tanzania. Aliiona nchi yake kama darasa, na daima alikuwa anafundisha.

Ninachotaka kuongelea hapa ni mchango wa Mwalimu Nyerere katika uwanja wa elimu. Elimu ni suala mojawapo ambalo Mwalimu Nyerere alilishughulikia sana. Katika kuelezea suala la elimu, Mwalimu aliweka na kufuata misingi kadhaa muhimu.

Tanganyika ilipopata Uhuru, Mwalimu Nyerere alikuwa ameshajizatiti kubadilisha mfumo wa elimu uliokuwepo wakati wa ukoloni, ambao ulikuwa mfumo wa kibaguzi. Kulikuwa na shule za wazungu, za Wahindi, na za watu weusi. Mara tulipopata Uhuru, Nyerere alifuta ubaguzi na kuwachanganya wanafunzi mashuleni. Tangu mwanzo, Mwalimu Nyerere aliamini dhana ya usawa wa binadamu.

Mwalimu Nyerere aliamini kuwa elimu ni haki ya kila mtu. Alifanya kila juhudi kutoa elimu kwa watu wote, kuanzia watoto hadi watu wazima. Mwalimu alijitahidi kujenga mfumo wa elimu ambao ulitoa nafasi kwa yeyote kutokana na uwezo wa akili yake, bila kujali kama alikuwa maskini au tajiri. Kwa msingi huu, watu wengi ambao hawangeweza kulipia masomo walisoma hadi vyuo vikuu.

Mwalimu Nyerere alitaka elimu iwe inamjenga mwanafunzi kuwa mdadisi wa mambo na mwenye kiu ya kutafuta elimu. Yeye mwenyewe alikuwa mwanafalsafa, mtu wa kutafakari mambo. Na hivyo ndivyo alivyotaka elimu iwe. Mwalimu alitaka elimu iwe nyenzo ya kumkomboa mwanadamu, tofauti na elimu ya kikoloni, ambayo ilikuwa inaendeleza fikra tegemezi, fikra za kujidhalilisha, fikra za kitumwa. Alitaka elimu ijenge tabia ya kuheshimiana, sio kiburi cha usomi.

Mwalimu Nyerere alitaka elimu ijumlishe nadharia na vitendo, na ijenge tabia ya kushirikiana, si kushindana na ubinafsi. Vijana mashuleni alitaka wawe pia wanajishughulisha na kazi za mikono, kama vile kulima au kufuga na useremala. Hii nayo ni elimu, na ni fursa ya kufahamu mengi ambayo hayapatikani darasani. Kazi za mikono aliziona ni njia moja ya shule kujenga msingi wa kujitegemea kwa mahitaji yake.

Mwalimu Nyerere alifundisha kuwa elimu haina mwisho. Aliwahimiza watu kujibidisha katika kutafuta elimu. Mbali ya kushughulikia elimu ya watoto na vijana mashuleni, alianzisha mpango wa elimu ya watu wazima. Vijijini na mijini watu walihimizwa na walipata fursa ya kujiongezea elimu, kuanzia kujifunza kusoma na kuandika hadi kujipatia ujuzi na maarifa katika fani na taaluma mbali mbali.

Kwa utaratibu ulioitwa kisomo chenye manufaa, wavuvi, wakulima, seremala, wafugaji, na wengine katika shughuli mbali mbali, walihimizwa kujiongezea ujuzi kwenye fani na shughuli zao. Vitabu vilichapishwa katika fani za aina aina, ambavyo viliwapa watu fursa ya kujifunza kusoma na pia kujiongezea maarifa na ujuzi.

Kama Watanzania tungefuata mawazo ya Mwalimu, leo tungekuwa mbali kimaendeleo, na tungekuwa na mategemeo ya kufanikiwa zaidi. Katika dunia ya leo ya utandawazi, elimu, ujuzi na maarifa ndio msingi wa mafanikio. Lakini, Tanzania tuna matatizo makubwa, kwani ari ya kujielimisha imepungua sana, na watu wanatafuta vyeti badala ya elimu. Wengi wanaamini kuwa njia ya mafanikio ni kutumia mambo ya ushirikina, badala ya kujiongezea maarifa katika fani na shughuli mbali mbali, iwe ni kilimo, uvuvi, au biashara.

Nimeona jinsi Wamarekani wanavyojali elimu. Wanatumia fedha kununua vitabu, kulipia semina, na fursa nyingine kadha wa kadha za kujiongezea elimu, ujuzi na maarifa, ili wapate mafanikio katika shughuli zao, kama vile biashara. Watanzania tungekuwa tumefuata nyayo za Mwalimu Nyerere tungefanya hivyo hivyo: tungeona umuhimu wa kutumia fedha kununulia vitabu na kulipia warsha za kujiongezea ujuzi na maarifa katika shughuli mbali mbali. Imani ya kuwa maendeleo na mafanikio yanatokana na mambo ya kishirikina ni dalili za kuanguka kwa ule msingi aliokuwa anaujenga Mwalimu Nyerere. Je, Watanzania tutaweza kushindana katika dunia ya leo na kufanikiwa bila elimu, ujuzi na maarifa? Hilo wimbi la ushindani wa kimataifa tutaliweza au litatuzamisha? Hilo ni suala la kulitafakari.

Kuufahamu mchango wa Mwalimu Nyerere katika elimu ni sherti kuyapitia maandishi yake na hotuba zake. Baadhi ya maandisho hayo na hotuba hizo zilihusu elimu moja kwa moja, na baadhi ya kazi zake hizo ni hazina ambayo inatuwezesha kukusanya dondoo mbali mbali za kutuwezesha kuielewa falsafa na sera ya Mwalimu Nyerere kuhusu elimu. Kwa bahati nzuri, kuna kitabu kimechapishwa, kinachokusanya maandishi muhimu ya Mwalimu Nyerere kuhusu elimu. Kinaitwa Nyerere on Education/ Nyerere Kuhusu Elimu. Ni kitabu muhimu sana ambacho kinapatikana hapa: http://msupress.msu.edu/bookTemplate.php?bookID=3032

6 comments:

kamuzo said...

Hakika, bila utamaduni wa kusaka maarifa kwa njia mbalimbali hasa kujisomea, taifa letu tutazidi kubaki nyuma. Kwa vile pande nyingine za dunia wanatumia muda na rasrimali nyingine kujielimisha kwa muda wote, jamii ambazo hazifanyi hivyo ziko mashakani kuendelea.

Kwa vile sasa uchumi unatawaliwa na maarifa zaidi kuliko rasrimali nyingine kama ardhi, madini, misitu, nk, haishangazi jinsi jamii zetu tunavyozidi kutegemea watu wengine watutengenezee vifaa vilivyojaa maarifa. Katika jamii zetu karibu kila kitu cha kutegemea maarifa sana kimetengenezwa njee. Hii ni hatari kwa usalama na maendeleo.

Ili tuendelee tunabidi na sisi tuuze bidhaa zilizotengenezwa kwa kuongezewa thamani ya maarifa na tuagize bidhaa kama hizo kutegemea na mahitaji ya walaji (product differentiation). Mfano mzuri ni kwamba hata nchi zinazotengeneza tuseme magari bado zinaagiza magari toka nchi nyingine. Utaratibu huu unaitwa "intra-industry trade" katika Uchumi.

Katika kuyasaka maarifa inapaswa kufika kipindi cha kutakiwa kuachia ("unlearn") baadhi ya vitu tunavyovifahamu kwa sasa. Hii inatokana na ukweli kwamba kadri mtu anavyopata ukweli sahihi, mambo mengine aliyodhani hapo zamani kuwa ni kweli inabidi aachane nayo. Labda hii ya kuutafuta ukweli sahihi inaweza ikawatisha baadhi ya watu kujisomea zaidi. Maana inasemekana kuwa "ujinga una raha zake" yaani ignorance is bliss! Kwa uhakika hakuna raha yeyote kwenye "ujinga" kwa vile dunia haibadiriki eti mtu anaiangalia kwa mtazamo usio sahihi.

Ka-mchango kangu katika uzi (thread) huu wa maana sana.

Mbele said...

Shukrani sana kwa mchango wako. Ni kweli usemavyo, kuhusu maarifa. Sehemu mbali mbali duniani watu wanatambua kuwa uchumi wa dunia ya leo unatawaliwa na maarifa kuliko kitu kingine chochote. Fundisho hili bado halijaingia vichwani mwa Watanzania wengi, na hivyo tunajichimbia kaburi. Lazima tujenge utamaduni wa kutafuta elimu na maarifa, utamaduni wa kusoma vitabu, kuhudhuria mafunzo ya aina mbali mbali. Tunatakiwa tuamke kimawazo na kutambua kuwa kununua vitabu na kuvisoma, au kulipia semina ni sawa na kugharamia pembejeo katika kilimo au kitendea kazi chochote. Kama tunafanya biashara, kwa mfano, tutambue kuwa kuna vitabu ambavyo vina nadharia, mbinu, na mawaidha muhimu. Kuna mambo madogo kama kumjali mteja. Siri moja ya mafanikio katika biashara ni kumjali na kumhudumia vizuri mteja. Inasikitisha kuwa hata jambo dogo kama hili wengi hawalitambui. Matokeo yake ni kuwa biashara yao ikizorota, wanasema wamelogwa. Narudia, shukrani kwa mchango wako. Katika kufuatilia habari zako mtandaoni leo, nimeona kuwa umeandika kitabu, _E-Commerce for Development: eTourism as a Showcase_. Nitakitafuta.

Mbilinyi mwinama said...

Nashukuru kwa naelezo haya Ninauhitaji na kitabu hicho nimeshindwa kukipata hapo

Mbele said...

Ndugu Aginiwe Mbilinyi, shukrani kwa ujumbe. Kitabu hiki, "Nyerere on Education/Nyerere Kuhusu Elimu," kilichapishwa na kampuni iitwayo E & D Ltd iliyoko Da es Salaam. Ninaamini kinapatikana katika maduka ya vitabu nchini Tanzania. Vitabu vya makampuni ya uchapishaji mengi ya Afrika vinasambazwa huku ughaibuni na African Books Collective iliyoko Uingereza na Michigan State University Press iliyoko hapa Marekani.

Nashawishika kuongeza jambo. Hii kampuni ya E & D Ltd ilianzishwa na inaendeshwa na akina mama wawili: Elieshi Lema na Demere Kitunga, ambao walikuwa wanafunzi wangu wa "Literature," Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Wana mtazamo wa kimaendeleo kuhusu uchapishaji, vitabu, na elimu kwa ujumla, na wanahamasisha usomaji wa vitabu kwa rika zote. Fuatilia shughuli zao, utajionea mwenyewe. Nakutakia kila la heri.

kwetutz24 said...

ni kweli uliyo yasema hapo juu.... Nina swali kwako Mr. Mbele kama Mwalimu wa Chuo Kikuu, unazungumiaje elimu ya sasa inayotolewa mashuleni na kwenye vyuo vikuu kulingana na sera ya Elimu bure naa ukilinganisha na elimu iliyotolewa na Mw. Nyerere zamani hizo.

Mbele said...

Ndugu Davis Kiwelu, shukrani kwa suali lako. Sina hakika kama nina jawabu, bali nina mtazamo. Ninaona kuwa mbali na suala la kutoa elimu bure, jambo ambalo Mwalimu Nyerere alifanikisha vizuri, tukiangalia suala la elimu ni nini, tutaona kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa na upeo sahihi, lakini leo tunakwamisha. Ninamaanisha nini?

Ni kwamba Mwalimu Nyerere alitaka elimu iwe inamfanya mwanafunziv asiwe mtu wa kuitikia au kukariri mambo, bali awe na tabia ya kudadisi mambo, na awe anajitambua na kujiamini. Leo ninaona kuwa tunapotea njia. Watu wanazungumzia miundo mbinu, madawati, na vitu vingine, bila kuangalia suala la elimu ni nini.

Leo, katika Tanzania ya awamu ya tano, utamaduni wa kuhoji unadidimizwa katika jamii na hii inaathiri malezi ya vijana pia. Siamini kama mazingira ya leo yanajenga ujasiri na uthubutu alioongelea Mwalimu Nyerere. Miaka ya Mwalimu Nyerere tulikuwa tunatafakari nadharia za wanafalsafa wa elimu kama Paulo Freire, ambao walihusisha elimu na ukombozi, kuanzia na ukombozi wa fikra hadi ukombozi kwa maana pana ya mapinduzi ya jamii.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...