Sunday, December 21, 2008

Kuku kwa Mrija

Watanzania wana uwezo mkubwa wa kubuni misemo na kudumisha uhai na utamu wa lugha ya kiSwahili. "Kuku kwa mrija" ni usemi moja ambao umepata hadhi ya pekee katika kiSwahili cha mazungumzo.

Naamini kuwa wengi wanaweza kueleza maana ya usemi huu na matumizi yake, lakini napenda kuelezea machache, kwa kuchambua mantiki yake.

Kuku kwa mrija ni usemi unaobeba dhana ya maisha ya raha, starehe, na vyakula tele. Kwa vile kuku ni nyama inayothaminiwa sana katika utamaduni wetu, kula kuku sana ni dalili ya kuishi maisha ya raha na mafanikio.

Kwa ujumla, Watanzania wanaamini kuwa maisha hayo yanapatikana nchi za nje, hasa Ulaya na Marekani. Mtanzania anayeishi huko anahesabiwa na Watanzania walioko nyumbani kuwa anakula kuku kwa mrija. Maisha yake ni ya starehe na kuku ndio chakula chake kikuu.

Mimi mwenyewe nilikuja Marekani mara ya kwanza mwezi Agosti 1980, kusoma katika chuo kikuu cha Wisconsin-Madison, nikitokea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambapo nilikuwa nafundisha. Wakati ule, ninavyokumbuka, dhana ya kuku kwa mrija haikuweko katika kiSwahili. Lakini utamaduni wa kuthamini kuku kuliko nyama zote ulikuwepo, kwani ni utamaduni wa tangu enzi za mababu na mabibi.

Kwa hivyo, nilipofika Marekani, nilikuwa na tabia ya kununua sana kuku. Nina hakika kuwa Watanzania wanaofika huku wanafanya hivyo hivyo, kutokana na utamaduni wetu.

Kitu ambacho sikujua, na Watanzania kwa ujumla hawajui, ni kuwa kuku wa kijijini Tanzania si sawa na kuku wa hapa Marekani. Kuku wa kijijini anakua katika mazingira muafaka kwa afya yake na afya ya wale wanaomla. Anakula punje, mabaki ya ugali au wali, na vidudu mbali mbali ambavyo havina madhara kwa afya yake, na nyama yake haina madhara kwa binadamu.

Kwa ujumla, kuku wa huku Marekani hawako hivyo. Makampuni ya kibepari ndio yameshika hatamu katika kuzalisha kuku na vyakula vingine. Lengo la hao mabepari ni kupata fedha, si kuangalia afya za binadamu. Kuku wao wanakuzwa katika mazingira ya aina yake na kulishwa vyakula na madawa ili wakue upesi, wakauzwe. Baada ya muda mfupi tu wanakuwa wakubwa na tayari kuchinjwa na kuliwa. Madawa wanayolishwa ni hatari kwa afya ya binadamu. Lakini mabepari wakipata mwanya, bila kubanwa, hawaangalii hayo. Naafikiana na Mwalimu Nyerere alivyosema kuwa ubepari ni unyama.

Kwa hivi, Mtanzania anayekuja Marekani au Ulaya na mawazo ya kuku kwa mrija anajitakia matatizo. Hapa Marekani penyewe, na Ulaya pia, baadhi ya watu wameshaanza kampeni ya kuelimishana kuhusu madhara ya ufugaji huu wa kisasa, iwe ni wa kuku au wanyama mbali mbali tunaowala.

Kampeni hii inahusu pia mboga za aina mbali, matunda, mayai, na vyakula vingine. Hofu ya madawa yanayotumika katika kilimo na ufugaji inazidi kuwahamasisha watu waingie kwenye mkondo wa kutafuta vyakula ambayo vimetokana na kilimo kisichotumia madawa, au mifugo isiyotumia madawa.

Watanzania hawaonekani kufahamu suala hilo. Wakati huu, ambapo nchi yetu imefungua milango na kuwaruhusu wawekezaji kuingiza vitu vyao vya kila namna, hata sekta ya vyakula imeathirika. Vyakula vinavyotoka nchi za nje vimejaa madukani, hata vile ambavyo vimetokana na kilimo au ufugaji wa kutumia madawa. Kuku kwa mrija sio tena kitu cha kukiwazia tu, kwamba kinapatikana Ulaya na Marekani. Yeyote mwenye hela Tanzania anakula kuku kwa mrija kutoka nje. Katika hali hii, wale mabepari wanaotafuta hela wanazidi kuneemeka nchini kwetu, na kwa vile sisi inaonekana hatutambui ujinga wetu, wao wataendelea kuchuma, kama methali inavyosema: wajinga ndio waliwao.

Mambo haya yanasikitisha. Jambo linalosikitisha zaidi ni kuwa Tanzania kuna vyakula vya kila aina ambavyo wakulima wanalima bila madawa, kama vile matunda, mboga, viazi, na maharagwe. Kuna mifugo ambayo ni salama kabisa kwa afya ya binadamu, kama vile kuku, mbuzi, na ng'ombe.

Lakini, Watanzania wengi wenye hela wanaona ni fahari kununua vyakula kwenye haya maduka ya kisasa, ambavyo vimetoka nje ya nchi na vimefungwa vizuri kwenye vifurushi, kuliko kwenda sokoni kununua viazi, mchele, na mboga zinazotoka kijijini.

Watanzania wengi wanaona fahari kununua vikopo vya juisi ya machungwa au maembe ambavyo vimeagizwa kutoka nchi za nje, kuliko kununua maembe au machungwa yanayotoka kijijini hapo hapo Tanzania. Akili ya kuelewa kwamba kadiri vyakula hivi vinavyokaa dukani, ndivyo vinavyopoteza lishe haiko vichwani. Ingawa tunda likikaa dukani wiki nzima baada ya kuchumwa linabaki tunda, thamani yake kama lishe haifanani na thamani ya tunda lililochumwa leo hii kijijini na kuletwa sokoni.

Elimu ni nguzo na kinga ambayo tumeendelea kuipuuzia katika nchi yetu. Matokeo yake ni kuwa tunashabikia kuku kwa mrija na vyakula ambavyo wenzetu Marekani na Ulaya wameanza kuviogopa kwa vile vina madhara kwa afya. Madhara ya vyakula vibovu yanaonekana sana katika nchi zinazosemekana zimeendelea, kama zile za Ulaya na Marekani. Tatizo la watu kunenepa kupita kiasi, kwa mfano, ni tishio, na watu wa huku wanaendelea kutambua hilo. Lakini, Watanzania ndio wanaanza kuvishabikia vyakula vinavyoleta madhara haya, na ambayo huku Marekani vinaitwa "junk food" (vyakula takataka), kwani tunaviona ni vyakula vya kisasa.

Tulipopata Uhuru, mwaka 1961, kiongozi wetu wa kwanza, Julius Nyerere, alitangaza kuwa nchi yetu ina maadui wakuu watatu, ambao itakuwa kazi yetu kuwapiga vita. Maadui hao ni ujinga, maradhi na umaskini. Kwa miaka yote ya maisha yake, Nyerere alijitahidi na kuongoza vita hivi na kutuelimisha kwa kila namna. Leo, inaonekana tunaukaribisha ujinga na hivi kujihumu sisi wenyewe.

2 comments:

Bennet said...

Mdau nashukuru sana kwa mada hii, na pia nakupa pole kwa kuwa sehemu ambayo hupati vitamu vya huku nyumbani mara kwa mara.

Mimi najitahidi sana kutumia vitu vya asili kuanzia madawa, chakula na maji. mfano mafuta ya kupikia huwa naagiza Singida ambako kuna mtu namjua anakamua mwenyewe alizeti anaichemsha na kuichuja na kuweka kwenye madumu, Upande wa nyama najitahidi sana kula nyama ya kienyeji na kamwe siweki kwenye freezer labda nyama ya porini tu, kuku nakula wa kienyeji tu na vitu kama nyanya, vitunguu, biringanya n.k najitahidi kununua ambavyo sio high breeds (inahitaji utaalam kidogo) situmii sukari ila natumia asali, sinywi soda mara kwa mara bali natengeneza juice kutokana na matunda yetu (bila sukari)

maji huwa nakinga yale ya mvua kwa ajili ya kunywa na pia nina kisima cha kuchimbwa (bore hole well) kwa hiyo nakwepa sana chlorine ya kwenye maji.

pamoja na dawa za hospital lakini pia mara kwa mara natumia dawa za asili kama majani ya mpera, muarobaini, aloe vera, miembe, matango, mkwaju na magome na mizizi ya miti mbalimbali

pia naendelea kujifunza dawa mbali mbali za asili ambazo naona zinafaa zaidi ya zile za kisasa ambazo huwa na madhara fulani kwa baadhi ya dawa kwa hiyo kama kuna dawa za asili ambazo unazijua naomba utudokezee kidogo. NAWASILISHA HOJA

Mbele said...

Shukrani sana kwa mchango wako, Mdau Bennet. Nilianzisha hii mada ili kuwavuta wanaojua zaidi watuelimishe. Mimi mwenyewe najitahidi kusoma kadiri niwezavyo, na nafahamu kuwa tabia zinazoenea Tanzania, kama nilivyodokeza, ni hujuma kwa kizazi cha leo na kesho. Naamini kabisa kuwa mfano unaoonyesha, wa kutumia vyakula, vinywaji na vitu vingine asilia ni muhimu sana. Mbali ya kuchangia ubora wa afya zetu, vile vile tunapotumia mazao na vitu vingine vya aina hiyo, kama vile kuku za kienyeji na matunda kutoka vijijini kwetu, tunaleta manufaa kwa uchumi kwa wazalishaji wetu. Kama wewe, nami hamu ya kuwasikia wadau wenye ufahamu zaidi wa masuala hayo. Binafsi, ningependa kuwasikia wadau wanaoweza kuelezea madhara ya vyakula hivi vinavyoitwa "fast food" au "junk food," huku Marekani, na ambavyo vinashabikiwa katika Tanzania ya leo.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...