Thursday, July 11, 2013

Tumeanza Kusoma "Abyssinian Chronicles"

Baada ya kumaliza kitabu cha Half of a Yellow Sun, darasa langu la fasihi ya Afrika tumekuwa tukisoma Abyssinian Chronicles, riwaya ya Moses Isegawa.

Moses Isegawa ni kijana aliyezaliwa na kukulia Uganda. Lakini mwaka 1990 aliondoka Uganda akaenda kuishi Netherlands, akiwa amechukua uraia wa nchi ile.

Nilikuwa nimesikia habari za kitabu chake hiki kwa miaka kadhaa. Nilinunua nakala, ila sikupata fursa ya kukisoma, ingawa nilikipitia juu juu. Hata hivyo katika kukipitia hivyo, niliona wazi kabisa kuwa ni kitabu murua, kilichoelezea kwa ufasaha na mvuto mkubwa maisha ya leo ya watu wa Uganda, kuanzia kijijini hadi mjini.

Nilipokuwa naandaa kozi yangu hii, miezi michache iliyopita, niliamua kitabu hiki kiwemo katika orodha yangu. Tumesoma karibu kurasa 100 tu,  wakati kitabu kina kurasa 480. Kiasi tulichosoma kimetupa fursa ya kuongelea dhamira mbali mbali zinazojitokeza, kama vile mila na desturi za arusi, masuala ya wahusika, na sanaa.

Kwa upande wangu, nimekuwa nikiwaambia wanafunzi kuwa maelezo ya maisha ya vijijini yamenikumbusha maisha yangu mwenyewe, maana nilizaliwa na kukulia nilikulia kijijini.

Moses Isegawa alikiandika kitabu hiki kwa lugha ya kidachi (Dutch), na jina lake lilikuwa Abessijnse kronieken, ambacho kilichapishwa Amsterdam mwaka 1998. Nakala 100,000 ziliuzwa hima, ingawa idadi ya watu wa nchi ile ni yapata milioni 16 tu.

Mwandishi alikiweka kitabu chake hiki katika lugha ya ki-Ingereza. Kwa kawaida, tunasema alikitafsiri. Lakini kwa mujibu wa falsafa za leo, dhana ya tafsiri ni dhana tata, na kile tunachokiita tafsiri sio tafsiri kwa kweli, bali utungo mpya. Huo ndio mtazamo wangu kuhusu Abyssinian Chronicles.

Muhula wetu umeisha leo, na mategemeo yangu ni kuwa wanafunzi na mimi mwenyewe tutaendelea kukisoma kitabu hiki hadi ukurasa wa mwisho. Sioni kama kuna tatizo kufikia mwisho wa muhula bila kumaliza kusoma kitabu. Dhana ya kumaliza kusoma kitabu nayo ni dhana tata na naweza kusema ni dhana muflisi. Kwa kutafakari kwa undani maana ya kusoma ni nini, na nini kinafanyika tunaposema tunasoma kitabu, nimejionea kuwa huwezi kumaliza kusoma kitabu chochote, hata kama umefika ukurasa wa mwisho na sentensi ya mwisho. Hilo ni suala jingine la falsafa, ambalo nalifafanua wakati wa kufundisha fasihi.

Abyssinian Chronicles ni kitabu kinachoelezea mambo ya miaka ya karibuni, ya sabini na kitu hadi themanini na kitu. Kinavutia sana. Ni ushahidi mwingine wa jinsi wenzetu wa nchi jirani, na wa nchi zingine za Afrika, walivyo katika anga za juu sana katika uandishi kwa lugha hizi za kigeni.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...