Thursday, July 4, 2013

Tumemaliza Kusoma "Half of a Yellow Sun"

Kwa wiki hizi sita, katika kipindi hiki cha "summer," nimekuwa nikifundisha kozi juu ya fasihi ya Afrika. Jana tumemaliza kusoma Half of a Yellow Sun, riwaya ya Chimamanda Ngozi Adichie wa Nigeria.  Huyu ni mwandishi chipukizi, lakini tayari ameshajipatia umaarufu sana na nyota yake inazidi kung'ara.

Amechapisha vitabu kadhaa akianzia na Purple Hibiscus na The Thing Around Your Neck. Ninavyo vitabu hivyo, na nimeshawahi kufundisha Purple Hibiscus.  Hivi karibuni, amechapisha Americanah, kitabu ambacho kinaongelewa sana miongoni mwa wasomaji, walimu, na wahakiki.

Kilipochapishwa kitabu cha Half of a Yellow Sun, nilisoma taarifa zake. Taarifa hizi zilielezea kuwa kitabu hiki kinahusu vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Nigeria, ambapo sehemu ya kusini mashariki ilijitenga na kutangaza kuwa imekuwa taifa huru la Biafra.

Mwaka 2008 Chimamanda Ngozi Adichie alikuwa mmoja wa waandishi walioalikwa kuhudhuria tamasha la vitabu Minneapolis. Alikuja kuzindua kitabu cha Half of a Yellow Sun. Nilihudhuria, nikasikiliza hotuba yake, kisha nikajumuika na umati wa watu waliokuwa wananunua nakala na kusainiwa na mwandishi. Nilipata pia fursa ya kupiga naye picha inayoonekana hapa kushoto.

Pamoja na kuwa nilinunua nakala ya Half of a Yellow Sun siku hiyo, sikupata fursa ya kukisoma. Lakini miaka yote hii nilikuwa na nia ya kufanya hivyo, na nimefanya hivyo katika kufundisha somo la fasihi ya Afrika.

Wote tumependezwa sana na Half of a Yellow Sun. Chimamanda Ngozi Adichie ana kipaji kikubwa sana cha kubuni na kusimulia hadithi. Yeyote anayesoma maandishi yake na anakijua ki-Ingereza vizuri, atakiri kuwa mwandishi huyu anaimudu vizuri sana lugha hiyo. Ni kweli kuwa kwa ujumla Half of a Yellow Sun inahusu vita ya Biafra, 1966-1970, lakini kwanza inaongelea maisha ya kila siku ya watu, hasa katika mazingira ya Chuo Kikuu cha Nsukka. Chimamanda alizaliwa na kukulia hapo, na katika maandishi yake hupenda kuongelea maisha ya wasomi na familia zao chuoni pale.

Hata katika mazingira ya vita, Half of a Yellow Sun inatuonyesha watu wakijitahidi kuendelea na shughuli zao za kawaida, kama vile kuelimisha watoto, hata kama ni chini ya mti. Tunawaona watu wakitafuta riziki za maisha. Na tunawaona watoto wakicheza michezo, pamoja na dhiki kubwa ya magonjwa na njaa. Pamoja na ukatili mkubwa uliojitokeza katika vita ya Biafra, Chimamanda Ngozi Adichie amejiepusha na kishawishi cha kuangalia suala zima kama suala la aina mbili tu ya watu, yaani wabaya na wema. Anaonyesha jinsi binadamu tulivyo na uwezo wa kuwa wabaya, sawa na wale ambao tunawaona ndio wabaya.

Half of a Yellow Sun imefuata vizuri mtiririko wa matukio yaliyotangulia vita na matukio ya vita yenyewe. Kwangu mimi kama m-Tanzania, nimeguswa na jinsi Chimamanda Ngozi Adichie alivyoelezea mchango wa Tanzania katika kuiunga mkono Biafra. Ameelezea furaha ya watu wa Biafra na heshima waliyokuwa nayo kwa Tanzania na Mwalimu Nyerere. Wakati nasoma kitabu hiki na suala hili la Tanzania, nilikumbuka kitabu kipya cha Chinua Achebe kiitwacho There Was a Country. Humo Achebe ameelezea vizuri sana jinsi msimamo wa Tanzania ulivyoshangiliwa na watu wa Biafra. Jina la Tanzania lilikuwa linatajwa kila mahali. Miziki ya Tanzania ilipigwa kila mahali. Katika Half of a Yellow Sun, kuna baa ambayo ilibadilishwa jina ikaitwa Tanzania Bar.

Kwa wasiofahamu napenda kusema kuwa sehemu iliyoitwa Biafra ni sehemu wanayoishi zaidi watu wa kabila la Igbo. Kutokana na siasa za Nigeria, ambamo ukabila una nafasi kubwa sana, dhuluma dhidi ya waIgbo, ikiwemo wengi kuuawa, hasa sehemu za kaskazini mwa Nigeria, ndio kitu kilichosababisha wakakimbilia kwao na kujitangaza kuwa ni taifa huru la Biafra. Chinua Achebe, ambaye alifariki hivi karibuni, na Chimamanda Ngozi Adichie ni wa kabila hilo.

Kwa kumalizia, bora niseme tu kwamba kuliko kusimuliwa, ni bora mtu ujipatie nakala ujisomee. Nasema hivyo nikijua fika kwamba ushauri huu hauna maana kwa jamii ya wa-Tanzania, kwani utamaduni wa kununua vitabu na kuvisoma haupo. Kuna uwezekano mkubwa kwamba ushauri wangu utazingatiwa na watu wa nchi zingine kama vile Kenya, ambayo ni makini kwa masuala ya aina hiyo.

2 comments:

Anonymous said...

Prof kuna siri gani ya wanaijeria kuwa waandishi wazuri wa vitabu katika fasihi kwa kiingereza, sijui kwa lugha nyingine za kiafrika?
Ona huyu tena
http://www.bbc.co.uk/news/world-africa-23230999.

Mbele said...

Mdau anonymous, shukrani kwa mchango wako. Naamini kabisa kuwa ili kuwa mwandishi bora, mtu lazima uwe msomaji hodari wa waandishi bora.

Mwandishi Ernest Hemingway alisema kuwa mwandishi lazima usome maandishi ya waandishi wote maarufu waliokutangulia, ili ujue wajibu wako wa kufanya vema kuliko wao. Alitoa mtihani mkubwa mno.

Wenzetu Nigeria wana historia ndefu ya kuwa na waandishi bora, na vijana husoma hayo maandishi, sambama na kusoma kazi za waandishi wengine wa nje ya Nigeria, nje ya Afrika. Ndio maana, ukisoma maandishi kama ya Chimamanda Ngozi Adichie, utaona anawataja, na wengine wanaotajwa ukimwonyesha m-Matanzania si ajabu ukagundua kuwa hata hajawahi kuwasikia.

Ni wa-Tanzania wepi ambao wanasoma maandishi ya waandishi kama Nadine Gordimer, J. M. Coetzee, Salman Rushdie, David Malouf, Chinua Achebe, William Faulkner, Ernest Hemingway, Orhan Pamouk, Ngugi wa Thiong'o, Naguib Mahfouz, Nuruddin Farah?

Nchi zinazotuzunguka, yaani Malawi, Kenya na Uganda ziko mbele sana katika uandishi wa ki-Ingereza. Wakati sisi tunaendekeza uzembe, wenzetu wanapiga kitabu.

Mmalawi ambaye lugha mama yake ni Kiyao, Kichewa au Kitumbuka, utamkuta anapiga ki-Ingereza sawa sawa. Mtanzania, ambaye naye ana lugha mama yake, anashindwa nini kukijua kiIngereza kama mJaluo au m-Kikuyu au m-Mnyankore anavyokijua?

Sisi ni Taifa la wazembe. Ukienda huko Nigeria, utakuta wana pia waandishi mahiri wa lugha za nchi ile kama vile ki-Yoruba, ki-Hausa, na ki-Igbo.