Tuesday, August 19, 2014

Laiti Ningekuwa na Bendera ya Tanzania

Jana nimeona taarifa mtandaoni kuwa Jumamosi hii, tarehe 23, mjini Faribault, Minnesota, kutakuwepo na tamasha la kimataifa la tamaduni. Hapo hapo nilipiga simu kwa waandaaji, ili kuona kama bado kuna nafasi ya mimi kushiriki.

Leo mratibu mkuu wa tamasha, amenipigia simu. Tumeongea kwa muda, nami nikamwulizia kama bado kuna nafasi ya kushiriki katika tamasha. Hapo hapo aliniambia kuwa nafasi bado iko, na kwamba tukimaliza maongezi atanitumia fomu ya kujisajili.

Tuliongelea shughuli nifanyazo katika jamii, ikiwemo kushiriki matamasha ya aina hii kama mwandishi na mwelimishaji, hasa kuhusu masuala ya tofauti za tamaduni na athari zake. Tuligusia pia ushiriki wangu katika masuala ya Faribault, kama ilivyotamkwa katika taarifa hii hapa.

Wakati tunaendelea na mazungumzo, aliniuliza kama nina bendera ya nchi yangu, yaani Tanzania. Alifafanua kwamba kwenye jukwaa kuu, zitakuwepo bendera za nchi wanakotoka washiriki wa tamasha, na kuna kipindi ambapo wawakilishi wa nchi hizo watakuwepo jukwaani wakiwa na bendera zao. Watapata dakika kadhaa za kuongelea mbele ya kadamnasi kuhusu nchi zao na hizo bendera. Hapo nilijisikia vibaya, kwani sina bendera ya Tanzania ya ukubwa utakiwao, ambao ni angalau futi  tatu kwa tano. Nilikiri kuwa sina, ila nikasema nitajitahidi katika siku hizi mbili tatu kutafuta.

Baada ya maongezi, nimeangalia mtandaoni nione wapi naweza kuipata bendera ya aina hiyo. Nimeona sehemu kadhaa, ambapo naweza kuagiza bendera hiyo. Nimepiga simu sehemu tatu, nikaambiwa kuwa hatawezekana kuipata kabla ya tamasha.

Kwa maana hiyo, nimekwama. Nimekosa fursa ya kuelezea habari za Tanzania na bendera yetu, mbele ya wote watakaohudhuria tamasha. Nimejifunza. Niko mbioni kuagiza bendera, niweze kuitumia siku za usoni.

Mji wa Faribault uko umbali wa maili kama 25 tu kutoka hapa ninapoishi. Nami si mgeni katika mji ule, kwani, kwa miaka iliyopita, nimeshafanya shughuli nyingi za jamii katika mji ule, kama ilivyoelezwa hapa, hapa, na hapa.

Lakini, pamoja na yote, hili suala la kutokuwa na bendera limenikera na papo hapo limenigutua. Mimi kama m-Tanzania, tena sio m-Tanzania wa uraia pacha, ningejisikia vizuri sana kuwepo kwenye jukwaa kuu na bendera yangu, nikasema mawili matatu kuhusu nchi yangu na bendera yake. Dosari hii ni lazima irekebishwe hima.

4 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Jsmani hata mtu mmoja huko hana? Umesema ya kweli kabida...mie ninayo ila ndogo....niendapo teba bitatafuta kubwa....kila la kheri kutangaza utamaduni wetu.

Mbele said...

Shukrani kwa ujumbe. Kwa kiasi fulani, ni tatizo la malezi. Tangu Tanganyika ipate Uhuru, mwaka 1961, nikiwa darasa la tatu, bendera ya Taifa ilikuwa kitu cha hadhi ya aina yake. Ilionekana mahali maalum tu. Ningeweza kuelezea zaidi kuhusu aina ya heshima iliyopewa bendera ya Taifa.

Nilishangaa nilipokuja Marekani. Hapa hata binafsi wanaopenda wanamiliki na kupeperusha bendera ya Taifa lao kwenye paa la nyumba, mbele ya nyumba, juu ya pikipiki, na kadhalika. Ndio namna yao ya kuonyesha heshima kwa bendera, na uzalendo.

Ilibidi nami nibadilike nilipoona hayo ya Marekani, kwa maana kwamba ningejipatia nami bendera kubwa ya Tanzania na kuihifadhi nyumbani. Nisingeipeperusha juu ya paa, au juu ya gari, kwani hii si Tanzania, bali ingenifaa katika shughuli kama hii ya kesho kutwa mjini Faribault.

Anonymous said...

Mwalimu hapo, wasiliana na Ubalozi wa Tanzania-Washington DC, au Balozi wa kudumu(Tanzania)UN-New York. Wanatakiwa kukusaidia kwenye hili kama suluhisho la muda mfupi.

Mbele said...

Ndugu Anonymous, shukrani kwa ujumbe wako, unaoonyesha nia ya kunisaidia. Nashukuru. Wakati nahangaika kutafuta bendera, wazo la kuwasiliana na Ubalozi wetu, Washington, D.C., lilinijia.

Hata hivi, kwa vile siku ya tamasha ilikuwa imekaribia sana, niliamua tu kuwa baada ya tamasha nijitafutie na kujinunulia bendera hiyo. Niko njiani kufanya hivyo. Halafu, nitakapostaafu na kurudi Tanzania, miaka ya karibuni, nitakwenda na bendera yangu.

Sijui kama raia binafsi anaruhusiwa kupeperusha nyumbani pake bendera ya aina ninayoiwazia, yaani kubwa ya futi tatu kwa tano. Wakija mgambo, nitavaana nao :-)

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...