Tuesday, July 12, 2016

Hemingway Auneemesha Mji wa Pamplona kwa Utalii

Wiki hii mji wa Pamplona nchini Hispania unafurikwa na maelfu ya watalii kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Ni kwa nini? Ni kwa sababu ya jadi ya tangu karne kadhaa zilizopita ya kusherehekea tamasha liitwalo San Fermin. Sherehe hizi hufanyika kila mwaka wakati huu wa Julai. Kati ya mambo yanayofanyika ni michezo ya kukimbizana na mafahali ("running of the bulls") na michezo ya kupambana na mafahali ("bull-fighting"), kama nilivyogusia katika blogu hii.

Ingawa jadi hii iko katika miji mingi nchini Hispania, dunia inafahamu zaidi Pamplona. Hii inatokana na mwandishi maarufu Ernest Hemingway. Baada ya kushuhudia tamasha hili mjini Pamplona kuanzia mwaka 1923, hasa hiyo "running of the bulls" na "bull-fighting," alivutiwa sana, akaielezea kwa ustadi katika riwaya yake ya kwanza The Sun Also Rises.

Ingawa ilikuwa ni riwaya yake ya kwanza, The Sun Also Rises ilimjengea Hemingway umaarufu kama mwandishi. Ulimwengu ulivutiwa na bado unavutiwa na usimuliaji wake, na hapo ndipo umaarufu wa tamasha la Pamplona ulipozuka na kusambaa. Tangu mwaka ule 1926 ilipochapishwa The Sun Also Rises hadi leo, mji wa Pamplona umeendelea kuifunika miji mingine kwa kuvutia watalii.

Hii si mara yangu ya kwanza kuongelea jinsi watu wengine ulimwenguni wanavyoneemeka kwa kutumia maandishi na jina la Hemingway kama kivutio cha utalii. Cuba ni mfano mojawapo. Hemingway huyu huyu alitembelea Tanganyika na sehemu zingine za Afrika Mashariki. Aliandika kitabu maarufu cha Green Hills of Afrika kuhusu mizunguko yake nchini Tanganyika, akiwinda kwenye mbuga kama Serengeti, Ngorongoro, Manyara, na Tarangire, akapita maeneo kama Babati, Kondoa, Handeni, na Tanga. Hiyo ilikuwa katika mizunguko yake ya mwaka 1933-34.

Katika mizunguko yake ya mwaka 1953-54, Hemingway alipita kwenye maeneo mengine pia kama vile Iringa na Mwanza. Katika barua zake, ziko ambazo zilitumwa kutoka kwenye posta za Tanganyika, kama vile John's Corner na Arusha. Hivi karibuni, nilipokwenda kuzuru maktaba ya J.F. Kennedy, lengo langu moja lilikuwa kuziona barua ambazo Hemingway aliandika alipokuwa maeneo haya. Nilikuwa nimezisoma zikiwa zimepigwa chapa vitabuni, lakini nilitaka kuona hati ya mkono wake.

Hizi ni taarifa ambazo zinahitaji utafiti na kisha kuzitumia kama wanavyofanya wenzetu. Nimepata hamasa ya kuandika ujumbe huu leo kwa kuwa huu ni wakati muafaka, ambapo ninafuatilia mambo yanayofanyika Pamploma wiki hii.


No comments: