Sunday, July 31, 2016

Ujumbe kwa Rais Magufuli: Shirikiana na UKAWA

Mheshimiwa Rais Magufuli, salaam na pole kwa majukumu ya kutumbua majipu. Mimi ni raia wako, ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa. Nimeona nikuandikie, ingawa ninajua kuwa jadi ya ovyo iliyojengwa na chama chako cha CCM ni ya kutotambua uwepo wa sisi raia tusio na vyama. CCM imekuwa na historia ya kutotambua kuwa sisi tusio na chama ni raia wenye haki sawa katika nchi yetu, na wenye akili na mitazamo kuhusu mustakabali wa nchi yetu. Achana na hii jadi. Itakuponza.

Ninaandika ujumbe huu kukushauri ushirikiane na UKAWA. Nina sababu za kukushauri hivyo. Kwanza, kumbuka kwamba tangu ulipoingia madarakani kama rais, UKAWA walionyesha mapenzi yao kwako kwa dhati, wakadiriki kutangaza mara kwa mara kwamba ulikuwa unatekeleza ajenda yao. Mheshimiwa Rais Magufuli, hakuna hazina kubwa kwa kiongozi kama kukubalika kiasi hiki. Na katika nchi yenye wapinzani, kuweza kuwakonga nyoyo zao kama ulivyofanya ni jambo la pekee. Ni baraka uliyojaliwa. Tafadhali usiifuje.

Sisemi ujiunge na UKAWA. Wewe ni mwana-CCM, na una uhuru na haki kikatiba ya kubaki CCM. Lakini kumbuka uliyokuwa umeyaona katika CCM wakati wa kampeni za urais. Ulitamka tena na tena kwamba ndani ya CCM wako ambao ni CCM mchana, lakini usiku wanakuwa UKAWA. Kwa maana hiyo, uko katika chama ambacho ni kitendawili.

Nimepata taarifa kuwa siku za karibuni umekuwa ukisema kwamba hao ndumilakuwili waliomo CCM utawafagia kwa fagio la chuma. Laiti kama ungeweza kufanya hivyo. Laiti kama ningekuwa na namna ya kukusaidia kufanikisha azma hiyo. Kwa bahati mbaya, sina uwezo kabisa. Kwa bahati mbaya, nawajibika kukueleza kuwa hata wewe itakuwia shida sana kuwagundua ndumilakuwili hao.

Hao ni ndumilakuwili wazoefu. Wamekubuhu katika sanaa ya kujivika ngozi ya kondoo. Ni wazoefu wa kupalilia unga. Watakuhadaa daima kwa kujifanya ni watu wako, kumbe usiku wanakubomoa. Kumbuka usemi wa wahenga, kwamba kikulacho ki nguoni mwako. Hii ndio sababu nyingine ya mimi kukushauri ushirikiane na UKAWA.

Wewe mwenyewe, na sisi wote tunafahamu, kuwa wako CCM wenzako ambao ni wafuasi wa Lowassa. Wamejichimbia CCM. Wanaendelea kula bata huko CCM, ilhali ni wafuasi wa Lowassa. Lowassa mwenyewe amethibitisha kuwa ana wafuasi wake huko CCM na amewahimiza waendelee mshikamano naye na kumpa taarifa.

Sasa, Mheshimiwa Rais, unahitaji ushahidi gani zaidi kwamba huko CCM umekalia kuti bovu? Hata hivyo, kama nilivyosema, ninatambua haki na uhuru wako wa kuwemo katika chama ukipendacho. Una haki na uhuru wa kuwemo CCM. Siwezi kuingilia haki yako na uhuru wako.

Lakini ushauri wangu kwamba ushirikiane na UKAWA unaweza kuwa ndio njia bora ya wewe kufanikisha majukumu yako uliyoazimia. Ukiwa karibu na UKAWA, UKAWA wataendelea kukuunga mkono kama walivyofanya tangu ulipoingia madarakani.

Ninahisi kwamba kadiri watakavyozidi kukuamini, itakuwa rahisi kwako kuwashawishi wakutajie hao ndumilakuwili waliomo CCM, ambao wamevaa magwanda na vikofia vya CCM, lakini ni wakereketwa "orijino" wa Lowassa. Tafakari hilo, Mheshimiwa Rais Magufuli. Ninaona kuna mazuri mbele ya safari, iwapo utaanza kushirikiana na UKAWA.

Halafu, kumbuka kwamba hao UKAWA si maadui zako. Wanacholilia ni wewe kuwaacha wafanye shughuli zao kwa mujibu wa katiba, ikiwemo mikutano na maandamano ya amani. Ni hicho tu, Mheshimiwa Rais. Wanachohitaji ni demokrasia kama ilivyotamkwa katika katiba.

Kumbuka, Mheshimiwa Rais, ulikula kiapo cha kuilinda na kuitetea katiba ya Tanzania. Kwa kuwa wanachotaka UKAWA ni wewe kuzingatia katiba ambayo uliapa kuilinda na kuitetea, tatizo liko wapi? Ulikula kiapo cha kuitetea katiba, lakini kwa jinsi CCM, vyombo vya dola, na wewe mwenyewe mnavyosuasua, mtu anaweza kudhani kuwa labda wewe na serikali yako mlikula kiapo cha kutetea kitabu cha hadithi za Abunuwasi.

Sasa hivi, CCM wanaonekana wakijibidisha kutekeleza kauli mbiu yako ya Hapa Kazi Tu. Tunawashuhudia wanavyoshindana katika kupiga huu mzigo. Lakini, kama nilivyosema, kumbuka kuwa si wote wako nawe kwa dhati. Wako ambao ni wazoefu wa kupalilia unga. Wanakuwa CCM mchana, na usiku wanakuwa UKAWA.

No comments: