Sunday, July 17, 2016

Nimealikwa Maoneshoni Faribault, Minnesota

Jana nilipigiwa simu ambayo sikutegemea. Ilitoka kwa mjumbe wa kamati ya maandalizi ya International Festival Faribault. Hayo ni maonesho ya tamaduni za kimataifa yanayofanyika kila mwaka mjini Faribault, Minnesota. Mtu aliyenipigia simu alikuwa ananiulizia iwapo ninapangia kushiriki maonesho mwaka huu, ili wanitengee meza.

Nimewahi kuhudhuria maonesho haya miaka iliyopita, na nimekuwa nikiandika taarifa zake katika blogu hii. Nimekuwa nikishiriki kama mwandishi na mwalimu, nikiwa na meza ya vitabu vyangu na machapisho mengine. Hapo ninaongea na watu juu ya shughuli zangu za uandishi, ufundishaji, na utoaji ushauri kuhusu tofauti za tamaduni na athari zake katika ulimwengu wa utawandazi wa leo.

Kila mara, nimekuwa nikifuata utaratibu wanaofuata washiriki wengine, yaani kupeleka maombi kabla kwa kujaza fomu na kuipeleka, pamoja na malipo. Kutokana na jadi hiyo, niliguswa kupigiwa simu jana. Nilipata hisia kuwa waandaaji wa maonesho wanathamini ushiriki wangu, nami nitakuwa nao bega kwa bega.

Nitaandaa vitabu vyangu na machapisho mengine, na nitapata fursa ya kukitangaza kwa mara ya kwanza kwenye tamasha hili kitabu changu kipya, mwongozo wa Song of Lawino. Vile vile, kwa kuwa tamasha hili ni fursa kwa watu kuzitangaza nchi na tamaduni zao, nitachukua pia bendera ya Tanzania, ambayo niliitafuta kwa madhumuni ya aina hiyo, kama nilivyowahi kuandika katika blogu hii.

No comments: