Saturday, July 30, 2016

Serikali ya CCM na Mikutano ya Kisiasa

Katika siku hizi chache, tumeshuhudia ubabe wa CCM na serikali ya CCM ambao ni hujuma dhidi ya haki za binadamu. Baada ya UKAWA kutangaza azma yao ya kufanya mikutano na maandamano ya amani nchi nzima (Tanzania) tumesikia kauli za vitisho kutoka kwa CCM na serikali yake.


Napenda kusema kuwa ninapinga msimamo wa CCM na serikali ya CCM kuhusu suala hilo kwa sababu ni hujuma dhidi ya haki za binadamu. Katiba ya Tanzania, ya mwaka 1977, 20 (1) imeweka wazi msimamo wake:

Every person has the freedom to freely and peaceably assemble, associate and cooperate with other persons, and for that purpose, express views publicly and to form and join with associations or organizations formed for purposes of preserving or furthering his beliefs or interests or any other interests.

Tamko hili la katiba ya Tanzania linaendana na tangazo la kimataifa la haki za binadamu ("The Universal Declaration of Human Rights"), vifungu namba 18, 19, 20, na 21. Nashauri kila mtu ajisomee, kwani tangazo liko sehemu mbali mbali mtandaoni.

Tumemsikia msemaji wa CCM akitoa vitisho kwa watu wa UKAWA kuhusu azma yao ya kuandamana, na amesema kuwa watakaofanya hivyo waende na wake na watoto wao kwenye mstari wa mbele wa maandamano. Kisha amewaagiza polisi wajiandae.


Huyu mheshimiwa anahitaji kuelimishwa. Asome maneno ya katiba ya Tanzania niliyonukuu hapa juu, na mengine ambayo sijanukuu, ambayo yanatamka wazi kuwa mtu hashurutishwi kushiriki mambo ya vyama vya siasa. Ni hiari. Kwa maana hiyo, kauli ya huyu msemaji wa CCM ni ya kijinga.


Mtu akiwa mwanachama wa chama cha siasa hana uwezo wala ruhusa kwa mujibu wa katiba ya Tanzania kumshinikiza mwenzake. Kila mtu ana uhuru wake na haki zake. Anaweza kuwa mke wa mtu wa chama fulani, lakini yeye akawa wa chama kingine, au akawa hana chama. Kauli ya msemaji wa CCM ni ya kijinga.


Msemaji wa CCM anadhihirisha jinsi alivyo na fikra za kimfumo dume, kwamba mume ni kama mtawala mwenye wadhifa wa kuamuru mke wake afuate anayotaka yeye. Dunia ya leo inasisitiza kuheshimu haki sawa kwa wanawake na wanaume. Huyu msemaji wa CCM anawafundisha nini watoto wa Tanzania? Lakini huyu ndiye ambaye CCM imemwona kuwa anafaa kuwa msemaji wake. Ni mpeperusha bendera wa CCM. Ni shida kweli.


Msemaji huyu amedhihirisha wazi kuwa anayahusisha maandamano na vurugu na hata umwagaji damu. Hajatoa mfano wowote kuthibitisha jambo hilo. Ni lini waandamaji wa Tanzania waliandamana wakiwa na silaha, wakasababisha vurugu na umwagaji damu? Wenye historia ya kubeba silaha na kuvuruga maandamano ya kisiasa ambayo ni ya amani, na hata kujeruhi na kuua waandamanaji wasio na hatia wanafahamika.


Juu ya yote, msemaji wa CCM anapaswa kuwa mstari wa mbele kuwaelimisha raia juu ya haki na wajibu wao katika maandamano. Asisitize kuwa katiba ya Tanzania inatambua haki na uhuru wa watu kufanya mikutano na maandamano kwa amani. Serikali ya CCM iheshimu katiba ya Tanzania. Iheshimu haki za binadamu.


Tanzania ni nchi yenye heshima tangu ilikotoka. Uvunjwaji wa haki za binadamu unaiharibia heshima nchi yetu, na mzalendo yeyote hawezi kuafiki jambo hilo.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...