Saturday, June 24, 2017

Eti Tundu Lissu Anapinga Kila Kitu

Kuna wa-Tanzania wanaomlalamikia au kumshambulia Tundu Lissu eti anapinga kila kitu. Napenda kusema kuwa malalamiko na mashambulio haya ni ujinga.

Kutoa mawazo na kujieleza ni haki ya kila binadamu, ambayo imetambuliwa katika tangazo la kimataifa la haki za binadamu na imetambuliwa katika katiba ya Tanzania. Tundu Lissu anatumia haki yake. Haingilii wala kuzuia haki ya mtu yeyote kutoa mawazo. Watu wajibu hoja zake. Watu wenye akili hufanya hivyo.

Kama Tundu Lissu hakubaliani na yale wanayosema wengine, na anahoji au kupinga muda wote, tatizo liko wapi? Masuala yenyewe yanahusu maslahi ya Taifa. Kila mzalendo anawajibika kutoa mchango kadiri ya uwezo wake. Mawazo ni mchango mmoja wapo. Na hiki ndicho Tundu Lissu anachofanya. Akae kimya kwa nini? Hata mimi sikai kimya ninapoona maslahi ya nchi hayafuatiliwi ipasavyo au yanahujumiwa. Kutoa mawazo ni muhimu, na kukosoana, inapobidi.

Ni ujinga kutotambua kuwa anavyofanya Tundu Lissu anatoa changamoto ya kuwafanya watu wafikiri nje ya upeo waliozoea au nje ya upeo wanaouwazia wao. Elimu haisongi mbele kama hakuna watu wachochezi wa fikra kama Tundu Lissu. Watu wanaohoji fikra zinazokubalika na jamii wanaipa jamii fursa ya kufungua milango mipya ya fikra. Siafiki uwekaji wa mipaka katika kufikiri na kutafuta ukweli. Elimu haiwekewi mipaka.

Mimi kama mwalimu ninawajibika kuwalea vijana wawe watu wa kuhoji mambo bila ukomo. Vinginevyo, kuna sababu gani ya kujiita mwalimu? Kuna sababu gani ya kuwa na vyuo na kusema kuwa tunaelimisha? Watu makini ulimwenguni kote wanatambua kuwa dunia inazidi kuwa ya "knowledge economy." Bila tabia ya udadisi usiokuwa na mipaka, tutajengaje "knowledge economy"? Kwa maana hiyo, ninamwona Tundu Lissu kama mtu muhimu kwa maendeleo ya nchi, na ni mfano wa kuigwa.

2 comments:

Unknown said...

Mimi nimeona shida hata kumjibu yule ndugu aliyejinadi kuwa eti anatupatia oridha ya watu 10 ambao, kwa mawazo yske, ni hatari kwa usalama wa taifa. Namuona yeye kuwa ni hatari zaidi ya wote kwani hata kiwango chake cha kufikiri kimegota kwenye ulimbukeni usio kichwa wala miguu.

Muttulu said...

Tena ni ujinga kiwango phd

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...