Ingawa mimi ni muumini wa dini, m-Katoliki, ninapenda kuzifahamu dini zingine. Sijiwekei mipaka. Sina tatizo na watu wa dini tofauti na yangu, wala watu wasio na dini. Ninajifunza kutoka kwao. Mtu unajifunza mengi kutoka kwa watu wenye mawazo tofauti na yako.
Ninasoma vitabu vya dini zingine, kama nilivyowahi kueleza katika blogu hii. Vile vile ninasoma vitabu vinavyohoji au kupinga dini. Fikra za wapinga dini zinafikirisha. Mfano ni kauli ya Karl Marx: "Religion is the sigh of the oppressed creature, the heart of a heartless world, and the soul of soulless conditions. It is the opium of the people."
Ninaipenda kauli hiyo ya Marx kwa kuwa inafikirisha na kusisimua akili. Kuna ubaya gani kwa mtu kuiponda dini namna hii? Kuna sababu gani ya mimi muumini kumchukia mtu wa aina hiyo? Kama vile mimi ninavyotetea haki na uhuru wa kuwa na mawazo yangu, naye ana haki na uhuru wa kuwa na mawazo tofauti na yangu. Ana uhuru wa kujieleza na kusambaza mawazo yake.
Ninavyo vitabu vinavyohoji u-Kristu. Mifano ni Jesus: Prophet of Islam, kilichotungwa na Muhammad Ata Ur-Rahim na Ahmad Thomson; The Gnostic Gospels, kilichotungwa na Elaine Pagels; na The Essential Gnostic Gospels, Including the Gospel of Thomas & The Gospel of Mary, kilichotungwa na Alan Jacobs. Nina vitabu vinavyouhoji u-Islam, vya waandishi kama Ayaan Hirsi Ali na Nawaal el Saadawi. Kuna vingine ambavyo bado sina, ila nitavinunua, kama vile vya Wafa Sultan na Ibn Warraq.
Kama mtu umejengeka katika dini yako na unatambua umuhimu na maana yake, kuna sababu gani ya kuvichukia vitabu vinavyoihoji dini? Jazba au masononeko ya nini, kama si ishara ya udhaifu na ubabaishaji wako mwenyewe? Binafsi, niko imara, na wahenga walisema, kelele za chura hazimzuii ng'ombe kunywa maji.
Fikra zinazohoji dini ninaziona kuwa zenye manufaa. Mimi kama muumini ninazichukulia hizo kama fursa ya kuimarisha imani, sawa na misukosuko inavyomkomaza mtu. Wakristu tunafundishwa uvumilivu, na hii ni njia ya kujipima tuna imani kiasi gani. Kama kawaida, nakaribisha maoni.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
No comments:
Post a Comment