Wednesday, May 14, 2014

Nimejifunza Katika Kuwapiga Picha Ndege

Nimejifunza mambo kadhaa katika kuwapiga picha ndege  kiasi cha yadi chache tu kutoka hapa nyumbani.

Kwanza sio ndege wa aina zote wanaruka zao  ukijaribu kuwasogea. Kuna aina ya ndege ambao  wana subira. Hao ni rahisi kuwapiga picha.

Katika ujumbe wangu wa juzi, sikufafanua suala hilo. Kwa hivi, leo narekebisha kauli yangu.


Jambo jingine ambalo nimejifunza ni kuhusu matumizi ya "zoom" kwenye kamera. "Zoom" ikielekezwa kwa ndege peke yake, halafu akakuzwa sana bila kitu kingine pembeni,  inapotosha ukubwa au udogo halisi wa ndege huyu. Ndege mdogo kabisa anaweza kuonekana mkubwa kama kuku.

Kwa hiyo leo nimejaribu kuwaonesha ndege wakiwa katika mazingira yao ili ukubwa au udogo wao ufananishwe na nyasi zinazowazunguka, au majani, au vijiti.

Monday, May 12, 2014

Ndege Mhandisi

Leo, katika matembezi huko nje, nilimwona ndege huyu akiwa ardhini, sio mtini. Alikuwa ng'ambo ya barabara, name nikiwa ng'ambo ya pili.

Kwa macho, alionekana ndege mdogo. Lakini nilipompiga picha, nikiwa nimefungua "zoom" ya kamera, nimegundua kuwa alikuwa amebeba nyasi mdomoni. Bila shaka ni nyasi za kujengea kiota.

Nilivutiwa na jinsi ndege huyo alivyo na nidhamu. Alifanya kazi hiyo bila usimamizi au amri ya yeyote. Na aliifanya kwa uaminifu ina kujiamini. Laiti wanadamu wote tungekuwa na moyo wa aina hii.

Sunday, May 11, 2014

Najaribu Kuwapiga Picha Ndege

Yapata wiki mbili zilizopita, nilinunua kamera mpya kule Amazon.com. Kwa vile bado afya yangu haijatengemaa, siendi mbali, bali hatua kadhaa tu kutoka hapa nyumbani. Kwa vile kipindi cha baridi kali kinaonakana kwisha, mazingira huko nje ni mazuri. Nyasi zimeota kwa vingi; hali ya hewa imeanza kuvutia,  na wanyama wadogo wadogo na ndege wa kila aina wanaonekana huko na huko.

Nimekuwa na hamu sana ya kupiga picha za ndege, lakini nimegundua ugumu wake. Ndege ni wajanja sana, wepesi kurukia tawi jingine unapotaka kuwapiga picha, au kuruka na kwenda zao. Lakini jana niliwaona ndege wawili wakubwa wakitembea pamoja. Sikuwa nimechukua kamera. Leo nilitoka tena, na ndege wale walikuwa sehemu ile ile ya jana wakitembea. Hao ingawa wanatembea, sio vigumu kuwapiga picha, nami nimepiga picha kadhaa. Kamera yangu ina "zoom" nzuri; kwa hivi sio lazima kuwasogea sana. Sina uzoefu na kamera hii; bado ninajifunza namna ya kuitumia katika vipengele vyake vyote.


Nmeamua kuwatafuta ndege na kuwapiga picha kutokana na kuvutiwa na picha anazopiga rafiki yangu, Profesa Bill Clemente wa Peru State College, Nebraska. Navutiwa sana na picha zake, na huwa nashangaa hao ndege anawawezaje. Picha zake nyingi huziweka katika Facebook. Hapo ndipo ninapoziona na kuzifurahia. Labda siku za usoni nami nitakuwa na uwezo kama wake.

Friday, May 9, 2014

Kitabu Kinawasaidia Wasafiri waMarekani

Ni furaha kwangu ninapoona malengo niliyokuwa nayo katika kuandika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences yanaendelea kutimia. Lengo kubwa lilikuwa kuwasaidia Wamarekani kuufahamu utamaduni wa MwAfrika, kadhalika kuwasaidia waAfrika kuufahamu utamaduni wa waMarekani.

WaMarekani wana tabia ya kusoma kuhusu nchi waendako. Nimeshaona tena na tena jinsi wale waendao Afrika wanavyosoma kitabu changu hicho Kama sehemu ya maandalizi ya safari.

Jana, wakati navinjari mtandaoni, niliona taarifa kutoka kwa wasasfiri kutoka Wisconsin ambao walienda Tanzania hivi karibuni. Kwa vile walishasoma kijitabu changu kabla ya kusfiri, ilikuwa rahisi kwao kuelewa mambo walioyoyaona kule Tanzania. Katika taarifa yao wameandika hivi:

In the United States we are accustomed to running from place to place, chasing time and cramming all we can into a day. In Tanzania we found a slower pace--we experienced "African Time." The day is not driven by the clock but rather shaped by people's relationships. It is accepted practice to be "late" as a result of lending a helping hand, catching up with an old friend, or extending hospitality to a stranger. This is something we learned prior to landing at the Julius Nyerere International Airport, having read "Africans and Americans: Embracing Cultural Differences" by Joseph L. Mbele as part of our seminar pre-work.

Kifungu hiki nimekinukuu kutoka katika taarifa nzima, ambayo ni hii hapa:www.leadershipwisconsin.org/2014/04/24/safari-of-a-lifetime-part-I/.

Monday, March 24, 2014

Namshukuru Mungu kwa Kunitoa Hospitalini

Tangu tarehe 1 Februari hadi tarehe 20 Machi nililazwa katika hospitali ya Allina Northwestern Minneapolis. Sasa niko nyumbani chini ya usimamizi wa wataalam wa kuimarisha afya ya viungo. Namshukuru Mungu.

Nawashukuru ndugu, jamaa, marafiki kutoka sehemu mbali mbali za dunia kwa salamu na sala zao. Nawashukuru madaktari na wauguzi. Inavyoonekana, nitakuwepo tena mitaani baada ya wiki kadhaa, Insha'Allah.


Sunday, January 26, 2014

Andikeni Vitabu Vyenu, Viwe Bora na Maarufu Kuliko Changu

Nawashauri akina anonymous wanaokikejeli kitabu changu wakati hata hawajakisoma waandike vitabu vya mada ile ile tuone kama wataweza.

Vinginevyo hao ni wapumbavu. Halafu, hakuna chuo kikuu kinachoweza kumtuza mtu cheo cha uprofesa kwa kuandika kitabu kama changu. Sio kitabu cha kitaaluma. Nimeshasema hayo tena na  tena katika blogu hii.

Saturday, January 25, 2014

Wiki Mbili Zijazo Kitabu Hiki Kinatimiza Miaka Tisa Tangu Kichapishwe

Wiki mbili tu kuanzia sasa, kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences kitatimiza miaka tisa tangu kichapishwe.

Sitaiacha siku hiyo ipite hivi hivi. Nawazia nini cha kufanya. Labda nitaandika ripoti kadhaa juu ya mafanikio yake. Kitabu hiki sikukiandika kwa ajili ya kujipatia pesa, ingawa kimeniletea pesa, tena sio chache.

Lengo langu na mafanikio yangu makubwa yamekuwa katika kuwagusa na kuwasaidia watu. Katika hilo najivunia kazi ngumu niliyofanya katika utafiti na uandishi wake.

Wako wachache ambao wamekuwa wakiniletea kejeli. Hao nawaona kama watu wasio na akili timamu. Kinachoudhi ni kuwa watu hao wanaongelea kitabu ambacho hawajakisoma.

Sitaweza kuleta maoni ya wote waliokisoma wakanipa maoni yao. Hao ni watu makini. Nawashukuru.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...