Sunday, May 26, 2013

Siku ya Vijana Kuhitimu

 Leo hapa chuoni St. Olaf tulikuwa na sherehe ya wanafunzi kuhitimu shahada ya kwanza. Kama kawaida kulikuwa na umati mkubwa wa watu, kuanzia wahitimu na ndugu na marafiki zao, wanafunzi wengine, na sisi walimu.

Ni siku ya furaha kwa wanafunzi wanaohitimu, lakini pia siku ya masononeko, kwani wanaondoka mahali ambapo walipazoea na wanaachana na watu ambao waliwazoea, kwa miaka minne.

Hapa kushoto niko na mwanafunzi mojawapo ambaye nilikuwa naye Tanzania mwezi Januari, katika kozi niliyofundisha juu ya mwandishi Ernest Hemingway.
Hapa kushoto niko na mwanafunzi ambaye alikuwa mmoja wa wale niliowaleta Tanzania mwaka 2011, kwa masomo katika mpango wa LCCT. Kwa mujibu wa mpango huo, mwanafunzi huyu alisoma chuo kikuu Dar es Salaam kwa muhula moja.

Hilo vazi nililovaa ndilo wanalopata wahitimu wa shahada ya uzamifu (PhD) katika chuo kikuu cha Wisconsin, Marekani, ambapo nilisoma 1980-86, nikahitimisha na tasnifu juu ya "The Hero in the African Epic." Rangi za mavazi hayo hutofautiana baina ya chuo na chuo.

4 comments:

Unknown said...

Graduation ni siku ya furaha sana. Kilichobaki ni kuyatumia maarifa waliyoyavuna kwa miaka minne kuziendeleza jamii zao. Profesa nadhani unakumbuka ule mfano wa mwalimu Nyerere aliyemmithilisha mtu aliyepelekwa shule na mtu katika kijiji chenye njaa halafu wanakijiji wakajibinya ili kumpatia chakula kidogo kilichobaki aende kijiji cha mbali kutafuta chakula kwa ajili ya kijiji chake.

Mbele said...

Ndugu Ado Shaibu, asante kwa ujumbe. Nami daima msimamo wangu umekuwa kwamba kupata shahada ni hatua tu katika njia ndefu ya kutoa mchango kwa jamii. Shahada ya uzamifu, kwa mfano, ni uthibitisho kuwa mtu unaweza kufanya utafiti wa kiwango cha juu.

Sasa basi, kinachotakiwa ni kwamba wale wenye shahada hii wathibitishe zaidi uwezo huu kwa kufanya utafiti na uandishi wa kiwango hicho.

Kuhusu huu mfano wa Nyerere, ni kwamba sisi tuliosoma enzi zake tuliuzingatia vizuri sana. Nyerere alikuwa na ushawishi wa hali ya juu, nasi tulikuwa wafuasi wake.

Nilikuja chuo kikuu cha Wisconsin-Madison, Marekani, mwaka 1980 kusomea shahada ya uzamifu, nikitokea chuo kikuu cha Dar es Salaam.

Kulikuwa na wa-Tanzania kadhaa pale. Ilikuwa kwamba mtu ukishatetea tasnifu yako, yaani umehitimu, tuseme labda leo, basi leo hii na kesho kazi ni kufungasha mizigo yako na kurudi Tanzania.

Tabia yetu ilikuwa hiyo, na tulikuwa tunawashangaa wenzetu kutoka nchi zingine za Afrika ambao, baada ya kuhitimu, walikuwa wanatafuta namna ya kubaki hapa Marekani.

Sisi hatukuwa na wazo hilo. Wazo letu lilikuwa lile lile la Nyerere, kwamba tumeletwa mbali kutafuta riziki ili turudi tukakifaidie kijiji chetu, yaani nchi yetu.

Mimi mwenyewe, nilipohitimu hiyo shahada ya uzamifu, nilidokezwa na profesa mojawapo kuwa ninaweza kuendelea kubaki Marekani nikitaka. Huo ulikuwa ni mwaka 1986, katikati.

Nilijibu kwa heshima kwamba nashukuru kwa wazo hilo, lakini ninataka kurudi nchini kwangu.

Ndivyo nilivyofanya. Nilirudi Tanzania na shehena kubwa ya vitabu ambavyo nilikuwa nimenunua kwa miaka sita niliyokaa Madison. Nilijua kuwa pamoja na elimu niliyoipata, hivi vitabu ndio nyenzo ya kuniwezesha kutoa mchango kwa kijiji, kama alivyotufundisha Nyerere.

Kwa kukaa nje miaka yote ile, bila kuja Tanzania, nilikuwa sifahamu kuwa nchi ilikuwa imebadilika. Nilishtuka nilipofika Tanzania na kuwasikia watu wakinishangaa kwa kuleta shehena ya vitabu badala ya "pick-up." Nilijiuliza hii jamii vipi? Mambo yaliendelea kuwa hivyo hadi hatimaye mwaka 1991 niliondoka na kuja kufundisha Marekani. Hapa ninajisikia raha, kwa sababu watu wanajali taaluma. Wanakuheshimu kwa ujuzi wako, utafiti wako, maandishi yako, na ufundishaji wako. Una gari, baiskeli, au unapekua kwa mguu, ni uamuzi wako na hakuna anayekuingilia au kukughasi.

Kwa taarifa ya zaidi ni kwamba nilipoondoka Tanzania kuja kufundisha Marekani, ile shehena ya vitabu vyangu alinitunzia rafiki yangu Profesa Mugyabuso Mulokozi, pale pale UDSM. Hii ndio habari yangu, kwa ufupi.

ham said...

Kuthamini vitu badala ya utu kutatupeleka kusikostahili.Ndiyo maana wengi hupenda njia za mkato wafike, potelea mbali hata kama ujuzi/ maarifa hakuna. Ole wetu tusipobadilika tutaendelea kumiliki maendeleo mdoli/mwanasesere. Tukija kuzinduka wenzetu walio makini wameshafika mbali, ndipo tutakapojua kuwa majuto nimjukuu. Nimeyapenda mno maneno yako yanayokisi usomi wa kina..."Nilishtuka nilipofika Tanzania na kuwasikia watu wakinishangaa kwa kuleta shehena ya vitabu badala ya "pick-up." Nilijiuliza hii jamii vipi? Mambo yaliendelea kuwa hivyo hadi hatimaye mwaka 1991 niliondoka na kuja kufundisha Marekani. Hapa ninajisikia raha, kwa sababu watu wanajali taaluma. Wanakuheshimu kwa ujuzi wako, utafiti wako, maandishi yako, na ufundishaji wako. Una gari, baiskeli, au unapekua kwa mguu, ni uamuzi wako na hakuna anayekuingilia au kukughasi." na mengine. Kwa mara nyingine ninakiri kuwa nimepata rutuba mpya itakayowasaidia kwa kiwango cha juu wanafunzi wangu ambao kupitia maelezo yako kwa Ndugu Ado. Niruhusu kutumia nukuu zako hizi kuonesha ni kwa kiwango gani wahitimu wengi wa leo katika ngazi mbalmbali za elimu wanahitimu ujinga. BRAVO Profesa.

Mbele said...

Ndugu ham, shukrani kwa ujumbe wako. Hakuna tatizo, tumia mawazo yangu kama ulivyoelezea. Tunachojaribu hapa ni kuwapa vijana mtazamo mpya kifikra na kimaisha, waone nini hasa ni muhimu katika maisha.

Kwa upande wangu, nilipata wito wa kuwa mwalimu tangu nilipokuwa mtoto mdogo, sijaanza hata darasa la kwanza.

Kazi pekee niliyokuwa naiwazia, na kwa maisha yote, ilikuwa ni kufundisha. Ndio maana vitabu ninavienzi sana. Ninavisoma sana, kila siku, sio vile tu ninavyovitumia darasani katika kufundisha, bali pia vya nyanja mbali mbali, ambavyo vinatajirisha akili yangu, kama vile falsafa, dini, saikolojia, siasa, na ujasiriamali.

Sijui tutaanzia wapi kuwapa vijana wa leo mtazamo kama ule aliohamasisha Mwalimu Nyerere, wa kusoma ili kutoa mchango kwa jamii, mtazamo ambao unajumlisha pia wazo la kujielimisha muda wote, kwani Nyerere huyo huyo alifundisha pia kuwa elimu haina mwisho.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...