Monday, March 7, 2011

Uandishi Bora wa ki-Ingereza

Suala la uandishi bora kwa ki-Ingereza limenifikirisha kwa miaka mingi na bado ninalifikiria. Nilipokuwa kijana, nilidhani kuwa uandishi bora wa ki-Ingereza ulihitaji matumizi ya maneno magumu na mbwembwe katika miundo ya sentensi. Kwa vile nilipata bahati ya kujifunza ki-Latini, nikiwa shule ya seminari, nilikuwa na uwezo wa kuyafahamu maneno mengi magumu ya ki-Ingereza, kwani asili yake ni ki-Latini.

Imani yangu hii ilikuja kugonga mwamba nilipokuwa nasomea shahada ya uzamifu katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison. Hapo nilikumbana na profesa Harold Scheub, ambaye alikuwa mkali kama mbogo katika suala la uandishi kwa maana kuwa alikuwa anataka uandishi unaotumia lugha nyepesi, kama ilivyoelezwa katika kitabu cha Elements of Style kilichotungwa na William Strunk na E.B. White. Huu ni uandishi usio na mbwembwe. Kila neno ni lazima lichunguzwe ili kuona kama ni lazima liwepo kwenye sentensi au la. Kama si lazima, sherti liondolewe.

Nilipata taabu sana kujifunza kuandika namna hiyo ya kutumia maneno yanayohitajika tu, tena yawe ya kawaida, bila mbwembwe. Sio mimi tu, bali kwetu wanafunzi wote ilikuwa ni kilio na kusaga meno.

Nilipopata jukumu la kufundisha uandishi bora wa ki-Ingereza hapa chuoni St. Olaf, nami nilianza tangu mwanzo kusisitiza hayo niliyojifunza kwa Profesa Scheub. Wakati huo huo, katika kuendelea kujibidisha katika kujifunza, nilitambua kuwa ni kweli huo ndio uandishi unaohesabiwa kuwa uandishi bora. Kwa mfano, ninajifunza mengi kutoka kwa mwandishi Ernest Hemingway, kama nilivyoelezea hapa.

Sasa basi, katika darasa langu la uandishi bora wa ki-Ingereza, huwa nawapa wanafunzi baadhi ya maandishi yangu ambayo yamechapishwa, ili wayachunguze na kuona ni vipi wanaweza kuyarekebisha ili yawe bora zaidi. Kwa mfano, nawapa insha yangu iitwayo "Do You Have an Accent?"

Insha hii imeandikwa vizuri. Hata walimu wengine wa ki-Ingereza wameipenda. Kwa mfano soma hapa. Lakini najua kuwa mtu makini akiichunguza zaidi, ataona vipengele ambavyo vingeweza kuboreshwa. Ndio maana nawapa wanafunzi wangu insha hii ili wajaribu kuvigundua vipengele hivi na kuvirekebisha. Ni zoezi ambalo linafaa kwa yeyote anayedhani anaifahamu lugha ya ki-Ingereza. Mimi mwenyewe nimegundua vitu yapata nane ambavyo vinahitaji kurekebishwa ili insha iwe bora zaidi. Hebu nawe iangalie insha hiyo kwa makini: "Do You Have an Accent?".

Saturday, March 5, 2011

Tafakari: Mwalimu Nyerere Aliiogopa CCM

Makala hii, "Mwalimu Nyerere Aliiogopa CCM," niliichapisha kwanza mwaka jana. Soma hapa. Kwa kuzingatia umuhimu wa ujumbe, nimeona niichapishe tena.
----------------------------

Mwalimu Nyerere Aliiogopa CCM

Ingawa alikuwa mwanzilishi wa CCM, kwa nia njema ya kuendeleza mapinduzi katika nchi yetu, miaka ilivyozidi kwenda Mwalimu Nyerere alishuhudia jinsi CCM ilivyobadilika na kuwa mzigo kwake na pia tishio kwa usalama wa Taifa.

Mwaka 1993 Mwalimu alichapisha kitabu kiitwacho Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania (Harare: Zimbabwe Publishing House, 1993). Pamoja na mambo mengine katika kitabu hiki, Mwalimu alisema kuwa kuna kansa katika uongozi wa CCM. Nanukuu baadhi ya maneno yake:

Chama cha Mapinduzi, kwa sababu ya uzito wa historia yake, hadhi ya jina lake, mfumo wa wavu wake, mazoea ya watu, na ubovu wa Vyama vya Upinzani, kinaweza kuchaguliwa na Watanzania, pamoja na kansa ya uongozi wake. Au watu wanaweza wakachoka, wakasema, "potelea mbali:" wakachagua Chama cho chote, ilimradi tu watokane na kansa ya uongozi wa CCM. Hainifurahishi kuyasema haya, lakini uhai wa Nchi yetu unataka yasemwe. (Ukurasa 61)

Mwalimu hakuishia hapo, bali aliongezea namna hii:

Nilisema awali kwamba kansa ya uongozi ndani ya Chama cha Mapinduzi isingekuwa ni jambo la kutisha sana kama tungekuwa tumeanza kuona Chama kizuri cha upinzani kinachoweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM. Ubovu wa uongozi ndani ya CCM ndio uliofanya nikapendekeza tuanzishe mfumo wa Vyama Vingi. Nilitumaini kuwa tunaweza kupata Chama kingine kizuri ambacho kingeweza kuiongoza Nchi yetu badala ya CCM; au ambacho kingekilazimisha Chama cha Mapinduzi kusafisha uongozi wake, kwa kuhofia kuwa bila kufanya hivyo kitashindwa katika uchaguzi ujao. Lakini bado sijakiona Chama makini cha upinzani; na wala dalili zo zote za kuondoa kansa ya uongozi ndani ya CCM. Bila upinzani mzuri wa nje, na bila demokrasia halisi ndani ya Chama cha Mapinduzi, Chama hiki kitazidi kudidimia chini ya uzito wa uongozi mbovu. Kwa hali yetu ya kisiasa ilivyo nchini hili si jambo la kutarajia bila hofu na wasi wasi! (Ukurasa 66)

Ni wa-Tanzania wangapi wenye utamaduni wa kusoma vitabu? Ni wangapi wanaosoma vitabu vya Mwalimu Nyerere? Ni wazi kuwa umbumbumbu miongoni mwa wa-Tanzania ni neema kwa CCM.

Friday, March 4, 2011

Makala Yangu Imepita

Blogu yangu ni sehemu ninapoweka chochote nipendacho, hata mambo binafsi, kama kumbukumbu au hata kujifurahisha. Niliwahi kusema hivyo. Leo nina taarifa ambayo imeniletea furaha moyoni.

Niliandika siku chache zilizopita kwamba mhariri wa jarida la Monday Development alikuwa ameiomba makala yangu, "What is Development?" Baada ya kuikarabati kidogo, niliipeleka.

Ni siku chache tu zimepita, nami nimefurahi kupata ujumbe kutoka kwa msahihisha makala (copy editor) wa jarida hilo. Hakuona kitu cha kusahihisha. Badala yake ameandika: "Thank you for the thoughtful, honest and well-written article."

Kwa huku Marekani, uamuzi wa msahihisha makala ni wa mwisho kabla ya makala kuchapishwa. Taarifa kama hii inaniongezea ari ya kuendelea na jitihada ya kuandika vizuri. Ninajua kuwa ninaweza kuandika vizuri kwa ki-Ingereza. Kama andiko langu likawa si zuri, sababu itakuwa ni uvivu au kukosa muda, sio kutojua ki-Ingereza bora kinakuwaje.

Wakati moja, mwandishi Jim Heynen, ambaye tulikuwa tunafundisha wote katika idara ya ki-Ingereza hapa chuoni St. Olaf, aliiona insha yangu moja fupi, "If You Came Where I was Born," akaomba aitumie katika darasa lake la uandishi kama mfano wa uandishi bora. Aliitumia hivyo hadi alipostaafu. Kutokana na umaarufu wa huyu mwandishi, niliguswa sana na jambo hilo.

Kwa hali hiyo, sikushangaa kupata ujumbe wa msahihisha makala wa Monday Development kuhusu makala yangu. Ila nina furaha sana kutokana na ukweli kwamba mzunguko wa jarida hili ulivyo mpana, makala yangu hii italisambaza jina langu kuliko chochote kingine ambacho nimeandika hadi sasa. Ninahisi hivyo, na ninahisi makala hii fupi itanifungulia milango na fursa mbali mbali, nami sitasita kuweka taarifa hapa katika blogu yangu.

Lakini hayo hayaji kwa muujiza au kwa bahati nasibu. Ni matokeo ya kujituma na kujishughulisha kwa dhati. Pamoja na kuandika, nimejikita katika shughuli ya kufundisha uandishi bora wa ki-Ingereza. Kuangalia na kutathmini uandishi wa wanafunzi na kuona makosa wanayofanya katika kutumia ki-Ingereza na kuyasahihisha imekuwa ni namna ya kujinoa mimi mwenyewe.

Hitimisho langu ni kuwa kama mimi nimefikia hatua hiyo, kutokana na juhudi, kila mtu anaweza pia, katika uwanja wake, kwa kutumia juhudi. Hakuna sababu ya kukata tamaa. Hii ndio habari yangu ya leo, habari binafsi ambayo naamini itawapa moyo wengine, hata kama ni wachache. Inatosha.

Wednesday, March 2, 2011

Orijino Komedi Wamtangaza Yesu



Kibao hiki cha Orijino Komedi kiliniacha hoi kabisa tangu nilipokiona mara ya kwanza. Mimi ni m-Katoliki. Kila ninapokiangalia kibao hiki, naishiwa nguvu, kwa jinsi Orijino Komedi wanavyoimba na kukatika. Ni balaa babu kubwa. Papo hapo wanawasilisha ujumbe kwa namna isiyosahaulika. Najikuta nikisema Mungu asifiwe kwa vipaji alivyowajalia Orijino Komedi.

Nashukuru kwamba miaka zaidi ya kumi iliyopita niliamua kuanza kumtafakari Yesu mimi mwenyewe. Ninaamini kwa dhati kuwa, kwa jinsi alivyokuwa karibu na watu na pia mpenda michapo, Yesu angeafiki jinsi Orijino Komedi wanavyotangaza neno lake kwa huo mtindo wao wa kuyaruka majoka.

Nawashukuru sana Orijino Komedi kwa kuleta neno la Yesu kwa namna hii ya kuvutia na kugusa moyo.

Sunday, February 27, 2011

Vitabu vya Chap Chap

Wengi wetu tunalalamika kuwa utamaduni wa kusoma vitabu umefifia au kufa miongoni mwa wa-Tanzania. Malalamiko haya yako sana katika hii blogu yangu. Kwa mfano, soma hapa.

Labda kuna haja ya kufafanua kitu tunachokilalamikia, maana wa-Tanzania hao hao inaonekana wanasoma sana vitabu ambavyo vinatungwa papo kwa papo kuhusu masuala kama vile mapenzi.

Vitabu hivi vinaandikwa haraka na kuchapishwa haraka na ndio maana naviita vitabu vya chap chap. Ni vijitabu, kwani vina kurasa chache tu.


Mwaka jana nilipokuwa Tanzania nilinunua kitabu cha aina hiyo kiitwacho "Pata Mambo, Part 5 ," kilichoandikwa na Fuad Kitogo (Dar es Salaam: Elite Business). Ingawa hiki ni kijitabu cha kurasa 40 tu, kinashughulikia masuala mengi kama inavyooneka katika picha ya jarida hapo juu.

Hivi vitabu vya chap chap si vitabu vyenye kiwango cha kuridhisha kitaaluma, bali vinawavutia na labda kuwaridhisha wasomaji wa ki-Tanzania. Katika ukurasa wa kwanza kuna maelezo haya: "Kitabu hiki ni mwendelezo wa vitabu vya Pata Mambo kuanzia namba moja vinavyopendwa kusomwa nchi nzima."

Kuwepo kwa vitabu hivi na kupendwa kwake ni changamoto kwetu sisi tunaodai kuwa utamaduni wa kusoma vitabu umefifia Tanzania. Labda uvivu tunaoulalamikia uko kwenye kusoma vitabu vikubwa vinavyotumia muda na fikra zaidi katika kuvisoma, tofauti na hivi vya chap chap ambavyo ni rahisi kuvisoma na kuvimaliza.

Friday, February 25, 2011

SUPER MUHOGO: Unga Safi wa Muhogo

Katika pita pita zangu, nimeona tangazo kwenye blogu ya Lady JayDee la wajasiriamali wa Chanika, Dar es Salaam, wanaouza unga wa muhogo. Wamemwomba Lady JayDee awawekee tangazo hilo kwenye blogu yake, naye amefanya hivyo.

Nimevutiwa na jambo hili. Njia madhubuti ya kujenga uchumi wa nchi yetu ni kuzalisha bidhaa na kuziuza nje, ili tupate fedha za kigeni. Kuuza bidhaa zetu nje kunaleta ajira nchini.

Hili ni jambo rahisi kulielewa. Hata mimi ambaye sikusomea somo la uchumi nimeandika kuhusu suala hili katika kitabu changu cha CHANGAMOTO, nikielezea namna mbali mbali jinsi wa-Tanzania tunavyohujumu uchumi wa nchi yetu. Mfano moja ni jinsi tunavyozishabikia bidhaa za kutoka nchi za nje, bila kutambua kuwa tunawapa ajira watu wa nchi zingine. Wakati huo huo, wa-Tanzania wanalalamikia uhaba wa ajira nchini. Tunapaswa kuuza bidhaa na huduma kwa wengine.

Kutokana na yote hayo, nimevutiwa na hao wajasiriamali wanaouza unga wa muhogo. Nimeamua kusaidia kutangaza biashara yao hapa kwenye blogu yangu. Nawatakia mafanikio tele katika kuboresha maisha yao na kuinua uchumi wa nchi.

Wednesday, February 23, 2011

Makala ya "Kwanza Jamii" Yaendelea Kupeta

Niliwahi kuandika kuhusu makala yangu ya kwanza kuchapishwa katika gazeti la Kwanza Jamii, "Maendeleo ni Nini," ambayo hatimaye ilichapishwa huku Marekani, baada ya mimi kuombwa niitafsiri kwa ki-Ingereza. Soma hapa.

Wahenga walisema: dunia ni mduara, huzunguka kama pia. Bila kutegemea, tarehe 20 Oktoba nilipata barua pepe kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kuwa ni mhariri mkuu wa jarida la Monday Developments. Ujumbe wa msingi wa barua yake ni huu:

We cover issues and trends in international development and humanitarian assistance, and are a publication of InterAction—an alliance of 200 U.S.-based international development organizations focused on the world’s poor and most vulnerable people.

One of our upcoming issues will be discussing the topic: Is development the new colonialism? While researching the subject, I came across your article “What is Development? Colonialism Deconstructed” and found it very refreshing. As a journal geared primarily toward global NGO staff, I thought your critique of the term and notion of development would be an interesting point of view to our readers—who often only see their side of the issue.

I wonder if you might consider adapting your article to run in our publication? Our readership includes NGOs, universities, the UN, World Bank, and offices of the U.S. government –exactly the audience who should be exposed to the points you raise.

Sikusita; nilikubali ombi la kuikarabati makala yangu na juzi nimeipeleka. Mhariri amejibu na kushukuru akisema, "You raise interesting points that our NGO readership should consider as they perform their work."

Makala hii, pamoja na zingine nilizochapisha katika Kwanza Jamii imo katika kitabu cha CHANGAMOTO, ambacho kinapatikana mtandaoni, kama inavyoonekana upande wa kulia wa ukurasa huu, na pia Dar es Salaam, simu namba 0754888647 au 0717413073. Nilikichapisha kitabu hiki ili kuwapa wa-Tanzania wengi iwezekanavyo fursa ya kuyafahamu mawazo yangu, kwa lugha ya ki-Swahili.

Nilifanya hivi ingawa najua kuwa vitabu havithaminiwi miongoni mwa wa-Tanzania. Nimejiepusha na lawama. Hatimaye nitapenda kukitafsiri kitabu hiki kwa ki-Ingereza, hasa baada ya kuona jinsi makala hii moja niliyoitafsiri inavyopokelewa na wale wasiojua ki-Swahili.

Naweka taarifa hii hapa iwe changamoto kwa watoto na vijana wetu. Wajizatiti na shule na elimu, kama nilivyofanya na ninavyoendelea kufanya maishani mwangu, bila kuyumbishwa na chochote. Manufaa yake huonekana baadaye.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...