Tarehe 21 Julai, wakati natoka Peramiho kurudi Songea, dala dala ilisimama kidogo kwenye kitongoji cha Lizaboni, ambacho ni sehemu ya Songea.Hapo niliona mchezo wa "pool" unaendelea, nikapiga picha hii nikiwa ndani ya dala dala.
Hii ni picha ya kanisa kuu la Peramiho, ambayo nilipiga tarehe 21 Julai. Safari yangu ya Peramiho niliielezea hapa.
Mwaka 1991 nilipata fursa ya kwenda India, kwa utafiti wa mwezi moja. Nilifikia katika taasisi ya American Studies Research Center, ambayo ilikuwa sehemu ya Chuo Kikuu cha Osmania, mjini Hyderabad. Hii ilikuwa ni mara yangu ya kwanza kuishi na wa-Hindi.
Kwa bahati nzuri, ninasoma misahafu na maandishi mengine ya u-Hindu. Ninafahamu kiasi cha kuridhisha kuhusu historia ya dini hii, imani yake. Ni dini yenye miungu wengi, baadhi wanafahamika kwa kila muumini na kuabudiwa, na wengine hawafahamiki na kila muumini. Baadhi ya miungu hao wanachorwa wakiwa na umbo la wanyama. Kwa mfano mungu aitwaye Ganesha anawakilishwa na tembo, na mungu aitwaye Hanuman anawakilishwa na umbo la tumbili. Ndio maana hapa kwenye picha kushoto, ninaziangalia sanamu kwa uchaji.
Hapa tuko mlangoni pa nyumba ya ibada. Tunapiga kengele, kabla ya kuingia. Sikuelewa maana yake, lakini nimesoma hivi karibuni kuwa huu ni utaratibu wa kuwafahamisha miungu kuwa umekaribia kuingia hapo.
Hapo kushoto naonekana nikitoa heshima katika nyumba hii ya ibada. Mhusika wa nyumba hii anaonekana akitabasamu, ingawa alijua kuwa mimi si m-Hindu. Ni ishara kuwa watu wa dini mbali mbali tunaweza kuheshimiana na kupendana bila tatizo.
Hapa naonekana nimekaa kwa heshima kabisa ndani ya nyumba ya ibada. Sikumbuki kama nilikuwa ninasali, au kama nilisali vipi, au labda nilikuwa nimegubikwa na mshangao kuwemo katika nyumba hii ya ibada ya dini ambayo sio yangu. Katika mazingira kama haya, mtu unaogopa kukiuka utaratibu, kwa hivi nadhani nilikuwa na woga fulani.
Hapa ninaonekana nikiendelea kutoa heshima katika nyumba hii ya ibada. Kwa kufanya hivyo, siamini kama nilikiuka imani yangu ya Katoliki. Niliwahi kukaribishwa misikitini katika mji wa Lamu. Niliingia kwa heshima zote, na bado mimi ni m-Katoliki. Nashukuru kupata fursa ya kuona nyumba hizo za ibada na hivi kujiongezea ufahamu kuhusu dini hizo. Kwa mtazamo wangu, hii ni njia moja ya kujenga maelewano na kuheshimiana miongoni mwa watu wa dini mbali mbali.
Katuni hii nimeiona katika mtandao wa Facebook. Inamwonyesha mchora picha na mteja wake. Huyu mteja ni mu-Islam anayeonekana amekaa kwenye kochi, akiwa ameshika ua.


Tarehe 21 Juni nilitembelea Peramiho, mkoani Ruvuma. Peramiho
ni kituo kikuu kimojawapo cha Kanisa Katoliki nchini Tanzania, tangu
enzi za m-Jerumani, ambapo wamishenari walijenga kanisa hapa.
Walianzisha hospitali, shule, vyuo vya ualimu, ufundi na uuguzi; shirika la uchapishaji, na mambo mengine
muhimu kwa jamii. Hapa kushoto ni picha ya Kanisa Kuu linavyoonekana
leo. 


Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...