Saturday, March 11, 2017

Mashairi ya Robert Frost

Leo nina jambo la kusema, kuhusu mashairi ya Robert Frost, ambayo nimekuwa nikiyasoma sambamba na kazi zingine za fasihi au taaluma. Ni mazoea yangu kusoma kiholela, kama nilivyowahi kuandika katika blogu hii.

Mashairi ya Frost ninayoongelea yamo katika kitabu kiitwacho Robert Frost: Selected Poems, ambacho binti yangu alininunulia. Wakati ule, nilijitahidi kuyasoma, lakini ninayafurahia zaidi wakati huu, labda ni kwa kuwa akili yangu imetulia kuliko wakati ule.

Leo, kwa mfano, nimesoma shairi liitwalo "The Black Cottage." Tunaelezwa kuhusu watu wawili wanavyoijongea nyumba ndogo iliyofichika nyuma ya miti na nyasi mbali na barabara. Wanaikaribia na kuchungulia ndani. Mmoja wao, ambaye ni mchungaji, anafahamu habari za nyumba hii ambayo sasa haina watu.

Anamweleza mwenzake kuwa bibi kizee aliyeishi humu alifariki, na watoto wake, wote wanaume, wanaishi mbali, ila hawataki kuiuza nyumba wala chochote kilichomo. Walipangia kuwa wanakuja mara moja kwa mwaka, lakini mwaka huu hawajaja. Baba yao alikufa katika vita ya wa-Marekani wenyewe kwa wenyewe ("Civil War"), eneo la Fredericksburg au Gettysburg.

Sehemu kubwa inayobaki ya shairi hili inaelezea fikra za marehemu bibi kizee kuhusu masuala mbali mbali yatokanayo na vita ile, kama vile malengo ya vita, na usawa wa binadamu. Mchungaji anaonesha kuwa fikra na mitazamo ya bibi kizee yule ilikuwa ya pekee na pia ya kutatanisha.

Hata mimi siwezi kusema nimeelewa vizuri mtazamo wa bibi kizee huyu, ingawa nimelisoma shairi hili na kulirudia. Itanibidi nilisome tena na tena. Vile vile, nimeona itakuwa jambo jema kufanya utafiti ili nione kama kuna tahakiki za shairi hili ambazo zimechapishwa. Daima, hii njia bora ya kujipanua upeo kuhusu utungo wa fasihi.

Kama kawaida, Frost anaandika kwa mtindo unaokufanya msomaji ujisikie kuwa anafanya nawe maongezi ya kina. Unawajibika kumsikiliza huku ukitafakari asemayo. Kusoma shairi hili, kama mashairi mengine ya Frost kunahitaji akili  tulivu.

Jambo moja linalonivutia katika kusoma mashairi haya ya Frost ni kuwa ninasoma alichoandika yeye mwenyewe, sio tafsiri. Ni bahati kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na mwandishi namna hiyo. Ninakuwa na fursa kamili ya kuguswa na umahiri wa mwandishi katika kuelezea mambo, kuanzia hisia na fikra zake na za wahusika, hadi vitu na mazingira.

No comments: