Saturday, January 31, 2009

Raha ya Kununua Vitabu

Tangu nilipokuwa kijana mdogo, nilipenda kununua na kusoma vitabu. Niliwahi hata kununua vitabu ambavyo vilikuwa vigumu mno kwangu kuvielewa. Nakumbuka, kwa mfano, kitabu kimoja cha falsafa, kilichoandikwa kiIngereza, ambacho nilinunua ila nilipata taabu sana kukisoma. Pamoja na kuwa somo la kiIngereza nilikuwa nalipenda na kuliweza kuliko masomo yote, kitabu hiki kilinishinda kwa wakati ule wa ujana wangu. Lakini nilifurahi kuwa nacho katika maktaba yangu ndogo.

Nilinunua pia vitabu vya kiSwahili. Kwa mfano, nakumbuka vizuri kitabu cha Shaaban Robert, Maisha Yangu. Vile vile, nakumbuka kitabu cha Yusuf Ulenge, Nguzo ya Maji na Hadithi Nyingine. Wakati ule, sikujua kabisa kuwa Yusuf Ulenge alikuwa mdogo wa Shaaban Robert. Hayo nimekuja kujua mwaka 2008, baada ya kununua na kusoma kitabu kiitwacho Barua za Shaaban Robert 1931-1958, kilichochapishwa na Taasisi ya Uchunguzi wa Kiswahili, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa mara ya kwanza mwaka 2002. Nimefurahi sana kufahamu kuwa Yusuf Ulenge alikuwa mdogo wa Shaaban Robert, na barua zilizomo katika kitabu hiki ni hazina kubwa kwa yeyote anayemwenzi Shaaban Robert.

Nilipoingia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kusoma, mwaka 1973, niliendelea na tabia ya kununua vitabu. Nilinunua vitabu vingi sana, kiasi kwamba, wanafunzi wenzangu wakinitembelea bwenini walikuwa wanashangaa uwingi wa vitabu vyangu. Niliendelea hivyo nilivyokuwa masomoni katika chuo kikuu cha Wisconsin-Madison, 1980-86. Kwa miaka sita niliyokaa pale, nilinunua vitabu vingi sana, na nakisia nilitumia yapata dola 2000 kununulia vitabu. Nilikuwa nimepata ufadhili wa shirika la Fulbright, na haikuwa vigumu kwangu kutumia sehemu ya hela hizo kwa kununulia vitabu. Siku moja, nakumbuka, nilitumia dola 100 kununulia seti nzima ya hadithi za Alfu Lela u Lela zilizotafsiriwa kwa kiIngereza na Sir Richard Burton. Niliporudi Tanzania na shehena hiyo ya vitabu, kuendelea kufundisha katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, watu walinishangaa kwa kununua vitabu badala ya gari.

Utamaduni wa kununua na kusoma vitabu ninauona sana hapa Marekani. Ni kawaida watu kwenda kwenye maduka ya vitabu, kuangalia vitabu na kuvinunua. Wanahudhuria sana tamasha za vitabu. Mara nyingi, watu wanapotaka kumpelekea mtu zawadi, wanamnunulia kitabu, awe ni rafiki, ndugu, mzazi, au mchumba. Zawadi ya kitabu inapendwa. Watu wakienda kupumzika kwenye sehemu za mapumziko, kama vile bustani za mijini, aghalabu wanakuwa na kitabu cha kujisomea.

Ninafahamu tabia za Wamarekani kuhusu suala la kununua vitabu na kujisomea. Hapa siongelei wanafunzi, bali raia wa kawaida, wafanyakazi na kadhalika. Ninakutana nao mara kwa mara ninaposhiriki katika maonyesho ya vitabu, au ninapokwenda kutoa mihadhara. Hapa naleta picha chache za matukio haya.


Hapo naonekana nikiwa na mama mmoja kwenye warsha mjini St. Paul, Minnesota. Anaangalia kwa makini vitabu vyangu. Tabia hii inanivutia na pia ndio tabia inayohitajika, kwani kujielimisha ni wajibu wa kila binadamu. Kusoma vitabu ni njia moja ya kujielimisha.















Hapa juu nimesongwa na wataalam mbali mbali katika sekta ya elimu, ambao walikuwa wanahudhuria mkutano kwenye Chuo Kikuu cha Iowa. Nilikuwa hapo na vitabu vyangu. Kama inavyoonekana, tuko katika shughuli nzito ya masuali na majibu.



Hapa niko na akina mama kwenye warsha niliyosaidia kuendesha, kwenye mji wa Grantsburg, Wisconsin. Wanaonekana wakiwa na furaha kwa kuvipata vitabu. Hii hali ya kufurahi kwa sababu ya kupata kitabu ni nadra nchini Tanzania. Hapo kwenye picha, mama moja anaonekana ameshika hela. Bei ya kitabu kimoja ni dola 14. Lakini anaonekana mwenye furaha. Ninapokuwa Tanzania, nikiwaambia watu kuwa bei ya kitabu changu ni dola 14, wanastuka na wengi wanaishia hapo. Wako wanaoomba wapunguziwe bei, na wako wanaoomba wapewe bure. Sio kila anayeomba kupunguziwa bei au kupewa kitabu cha bure ana tatizo la hela. Watanzania wengi wana hela sana. Hela wanazonunulia bia, kwa mfano, ni nyingi sana, kila wiki. Msimamo wangu ni kuwa hao wenye kuthamini bia kuliko vitabu wanao uhuru wa kuendelea na msimamo wao huo. Tunapishana mawazo, kwani mimi naamini kuwa mawazo yaliyomo katika vitabu vyangu yana thamani kuliko bia. Halafu, najiuliza, inakuwaje watu hao wasiombe kupunguziwa bei ya bia, ambayo inapanda muda wote?

Hapo ni pale kwenye mkutano Chuo Kikuu cha Iowa. Niko katika mjadala na mtaalam wa masuala ya elimu baada ya yeye kununua kitabu.


Picha hii inanivutia labda kuliko zote na ni hazina ya pekee kwangu. Huyu mama ni wa kutoka Nigeria. Hapa tulikuwa kwenye mkutano katika mji wa Minneapolis. Alifika na mwanae kwenye meza yangu na tuliongea kuhusu shughuli zangu za ufundishaji, utafiti, na uandishi. Kilichonivutia zaidi ni kitendo chake cha kuja na binti yake. Kumlea mtoto katika hali hii ya kupenda vitabu ni jambo la kupigiwa mfano. Je, ni wazazi wangapi katika nchi yetu wanafanya hivyo? Lazima tujitafiti, na tujizatiti ipasavyo katika kukuza taifa la kesho.

Saturday, January 24, 2009

Chakula Bora

Niliwahi kuandika makala, Kuku kwa Mrija. Leo nimeona nilete makala juu ya vyakula anavyokula Rais Mpya wa Marekani, Barack Obama, makala ambayo inasisitiza umuhimu wa kuangalia tunakula nini, na inaonyesha kuwa kiongozi anaweza kutoa mfano kwa wananchi. Kama nilivyosema katika ile makala ya Kuku kwa Mrija, kuna tabia mbaya inayojengeka miongoni mwa Watanzania, ya kushabikia vyakula ambavyo au havina faida kiafya au vina madhara kiafya. Lakini kutokana na kasumba, watu wanaona wanajipatia hadhi ya juu kwa kutumia vyakula hivi.

Makala ninayoleta hapa imeandikwa kwa kiIngereza, na ingawa blogu yangu hii inatumia kiSwahili, nimeona nivunje utaratibu huu kutokana na umuhimu wa suala la chakula. Ninategemea kuwa wale ambao hawajui kiIngereza labda wataweza kupata msaada wa kutafsiriwa makala hii. Watanzania na wengine wote tunaweza kujifunza mengi kutokana na makala hii inayomhusu Rais Obama. Soma hapa.

Monday, January 19, 2009

Waafrika Wanamwenzi Obama?

Kesho, tarehe 20 January, 2009, Barack Obama anaapishwa kama rais wa 44 wa Marekani. Dunia nzima iko katika heka heka za furaha na matumaini yasiyo kifani kutokana na ushindi wa Obama katika kampeni za urais wa Marekani.

Waafrika nao wamejawa na furaha, na wanajivunia, wakizingatia kuwa baba yake Obama ni Mwafrika mwenzao, kutoka Kenya. Waafrika wanaamini kuwa Rais Obama atajenga uhusiano bora na Afrika, kwani Afrika ni kwake.

Lakini je, Waafrika wanaomshangilia Obama wanamfahamu Obama au wanashangilia tu kwa vile kwa asili yake ni Mwafrika? Ukweli ni kuwa, Waafrika wengi hawana fikra wala mtazamo kama wa Obama kwa mambo mengi. Kwa mfano, Obama amekuwa mstari wa mbele kwa shughuli za kujitolea kwa ajili ya jamii yake na binadamu kwa ujumla, amekuwa mtetezi wa wanyonge, na ameonyesha mfano mzuri wa kujibidisha katika elimu na kuwa binadamu bora.

Ajabu ni kuwa hata Waafrika ambao ni wazembe, wanaoendekeza rushwa na ufisadi, wasiothamini elimu, wasiothamini suala la kujitolea, wote wanamshangilia Obama. Kuna nini katika vichwa na mioyo ya watu hao?

Obama amezingatia sana suala la heshima kwa wanadamu wote bila kujali tofauti za rangi, dini, taifa, na kadhalika. Anaamini kuwa kila mtu anastahili fursa ya kufanya yale ambayo yanaendana na uwezo wake. Ana imani kubwa kuhusu uwezo wa binadamu, na kila binadamu.

Waafrika wengi ni wabaguzi, kwa misingi ya kabila, dini, na kadhalika. Hawatambui usawa wa binadamu, bali wanamthamini mtu wa kabila lao, kijiji chao, ukoo wao, dini yao, na kadhalika. Wakati Obama amechaguliwa na Wamarekani wa rangi na dini mbali mbali, na wakati Obama anawahamasisha Wamarekani kujiona kama kitu kimoja, bila kujali tofauti zao, wawe ni weusi, weupe, wanawake, wanaume, wa dini mbali mbali, na kadhalika, Waafrika wengi hawako tayari hata kumpigia kura mtu wa kabila lisilo lao.

Inashangaza kwamba Waafrika hao ambao wanapigana na kuchukiana kutokana na tofauti za lugha, utamaduni, kabila, na kadhalika, wanashangilia ushindi wa Obama na wanaamini kuwa Obama ni mtu wao. Inashangaza kuwa nao wanaamini wanamwenzi Obama, badala ya kutambua kuwa namna ya kweli ya kumwenzi Obama ni kufuata nyayo zake. Ni sahihi kabisa kuuliza: hao Waafrika wanamwenzi Obama kweli au wanajikanyaga?

Saturday, January 17, 2009

Watanzania na Mkutano wa Sullivan

Mwanzoni mwa mwezi Juni, 2008, mji wa Arusha ulipata fursa ya kuwakaribisha wageni wengi kwenye mkutano mkuu wa nane wa Sullivan. Nilikuwa katika mkoa wa Arusha pamoja na Wanafunzi kutoka Chuo cha Colorado, ambao nilikuwa nawafundisha kuhusu maandishi na safari za Ernest Hemingway maeneo hayo. Kwa hivi, sikupata fursa ya kuhudhuria mkutano wa Sullivan.

Hata hivi, nilipata fursa tele ya kuongea na Watanzania kuhusu mkutano huo. Lengo la taasisi ya Sullivan ni kuchangia maendeleo ya Afrika, kwa kujenga uhusiano wa kibiashara, kijamii, na kadhalika baina ya Afrika na hasa Marekani na Ulaya. Mwanzilishi wa taasisi alikuwa Mmarekani Mweusi, Rev. Leon Sullivan, na kwa sababu hiyo, taasisi hii imekuwa na mvuto mkubwa miongoni mwa Wamarekani Weusi. Hao wanaikaribisha kwa mikono miwili fursa ya kuwekeza barani Afrika na kuungana na Waafrika katika kutekeleza ajenda ya maendeleo.

Basi, kwenye mkutano wa Arusha, Wamerekani Weusi walikuja wengi sana, wakiwemo watu maarufu katika nyanja mbali mbali, wanasiasa, wafanya biashara, na wanataaluma. Mategemeo ya mkutano yalikuwa mengi, kama vile kutoa fursa ya wawekezaji kuleta mitaji, kujenga ushirikiano baina ya wafanya biashara wa Tanzania na hao wageni, na kujenga ushikiriano katika nyanja mbali mbali.

Katika mazungumzo yangu na Watanzania, nilikuwa nawauliza kama wao wamejiandaa vipi kwa yote hayo. Niliwauliza, Je, wanavyowania kushirikiana na Wamarekani, wamefanya juhudi yoyote kuwafahamu hao Wamarekani? Wanamfahamu Mmarekani Mweusi? Hapo nilimaanisha ufahamu wa tabia, hisia, imani, maadili, namna ya kufikiri, namna ya kuongea, na kadhalika. Je, Mtanzania anafahamu hayo? Au anadhani kuwa ni jambo rahisi tu kukutana na Wamerekani na kushughulika nao?

Maongezi yalikuwa mazuri, na nilipata fursa ya kuwaeleza umuhimu wa kujiandaa. Niliwapa mifano hai kuhusu tabia na hisia za Wamarekani Weusi. Mfano moja niliutoa kwa kutumia tabia za Watanzania wanapokuwa na wazungu. Watanzania, kama walivyo Waafrika wengine, wana tabia ya kumtetemekea mzungu. Katika mahoteli ya utalii, kwa mfano, wahudumu wa kiTanzania wanawahangaikia sana wazungu, na hawaoni tatizo kumwacha mteja Mwafrika akiwa bila huduma au kumwacha akingoja huduma hiyo hiyo, hata kama aliwahi.

Niliwaeleza kuwa endapo Wamarekani Weusi watakuja na kuona tabia hii, hawatafurahishwa; watakata tamaa, na huu unaweza ukawa ndio mwisho wa hili wazo la kujenga ushirikiano. Tatizo ni kwamba Watanzania kwa ujumla hawaelewi undani wa hali ya Marekani na mahusiano baina ya Wamarekani Weusi na weupe. Hawaelewi hisia na fikra za Wamarekani. Niliwaasa Watanzania waache kuishi katika ulimwengu wa giza na ndoto, bali waanze kujielimisha.

Mfano mwingine niliotoa ni namna ya kuongea. Wamarekani wanaongea kwa namna ambayo inaweza kuonekana ni maudhi kwa Mtanzania, wakati wao kwao ni sahihi. Na wao wanaweza kuudhiwa na namna Watanzania wanavyoongea, wakati kwa upande wa Tanzania ni sahihi. Na kuna mambo mengine mengi yanayotofautiana baina ya tamaduni hizi mbili.

Kwa hivi, niliwaambia Watanzania kuwa suala la kujielimisha kuhusu hao Wamarekani ni la msingi. Sikusita kuwaeleza kuwa mimi ni mtafiti na naandika sana kuhusu masuala hayo. Niliwaeleza kuwa waanze kulichukulia suala la kujisomea na kujielimisha kuwa ni suala muhimu, hata katika biashara. Kununua kitabu kwa ajili hiyo ni sawa na kununua kifaa kingine chochote kinachoboresha biashara. Kwa lugha rahisi, kitabu ni zana na mtaji muhimu.

Nitaendelea kufanya mazungumzo ya aina hii, kwa namna yoyote. Kwa bahati nzuri, nimeshaanza sasa utaratibu wa kuendesha semina, ninapokuwa Tanzania. Nilifanya hivyo mwaka jana, kama inavyoonekana hapa, na ndivyo itakavyokuwa siku zijazo, panapo majaliwa.

Sunday, January 11, 2009

Matawi ya CCM Nje ya Nchi

Kwa miezi mingi sasa, kumekuwa na habari za kuanzishwa matawi ya CCM nje ya Tanzania. Naamini kila Mtanzania anaweza kuwa na maoni yake kuhusu jambo hili, na mimi ninayo pia, ingawa mimi ni Mtanzania ambaye si mwanachama wa chama chochote cha siasa.

Niliishi nje ya Tanzania kwa mara ya kwanza miaka ya 1980-86, nikiwa masomoni Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison, Marekani. Nilipofika hapo, nilipokelewa vizuri na Watanzania waliokuwa wanasoma hapo. Walinipa kila msaada na ushauri niliohitaji ili kuzoea maisha yale mapya.

Jumuia hii ya Watanzania, ingawa haikuwa kubwa, ilikuwa kama familia huku ugenini. Wakati wa shida na raha tulijumuika. Na mara kwa mara tulikuwa tunakutana kwa maongezi na kustarehe pamoja. Kama mtu alishindwa kuja kwenye mikutano hii, ilikuwa ni sababu ya labda kuzidiwa na shughuli au kuwa safarini. Lakini hatukuwa na mtu aliyekuwa hatakiwi au aliyejiona hatakiwi au hahusiki katika mikutano hiyo.

Ningependelea Watanzania wanoishi nje waendeleze jadi hiyo. Mazingira ya huku nje ni tofauti na yale ya Tanzania. Mtu aliyeko Tanzania hana tatizo la upweke. Kuna ndugu, jamaa, marafiki na majirani muda wote. Mtanzania aliyeko Tanzania hana tatizo la kujikuta katika utamaduni mgeni na athari zake. Yuko kwake.

Watanzania walioko nje wanakutana na utamaduni usio wao, na hali hii ina athari za aina aina kwa kila mtu, na inaweza kuwa na madhara kisaikolojia. Watanzania wanaoishi nje ya nchi wanahitaji kuwa karibu na Watanzania wenzao bila ubaguzi wa aina yoyote. Kuanzisha matawi ya CCM au chama kingine chochote cha siasa huku nje ni kuathiri hali ambayo tayari ni ngumu.

Nakumbuka tulivyoishi Wisconsin, halafu najiuliza: Je, ingekuwa ndio leo, tuko Wisconsin, halafu baadhi yetu waanzishe tawi la CCM, hali ya jumuia yetu ingekuwaje? Je, kama baadhi nao wangeanzisha tawi la chama kingine, au matawi ya vyama vingine, hali ya jumuia yetu huku ugenini ingekuwaje?

Vyama vya siasa Tanzania, kuanzia CCM, vimekuwa mstari wa mbele katika kuhujumu amani na mshikamano nchini, hasa wakati wa uchaguzi. Mifano iko wazi, kama vile yaliyotokea Zanzibar mwaka 2001, kama ilivyoelezwa hapa, Tarime mwaka 2008, na sehemu mbali mbali nyingine. Vurugu za Visiwani ziliendana na mauaji, uvunjwaji wa haki za binadamu, na uharibifu wa mali uliosababisha watu kukimbilia sehemu kama Kenya na hata Somalia, kama inavyoelezwa hapa na hapa. Ni ajabu sana, kwamba Watanzania wakimbilie Somalia. Haya yote ni matokeo ya ukosefu wa uongozi bora, uongozi wa busara na haki. Kama CCM, ambayo ilishika hatamu za uongozi nchini, ingekuwa na uongozi bora, wa busara na haki, matatizo au hayangekuwepo au yangetatuliwa bila ubabe na vurugu kama zile.

Wasi wasi wangu ni kuwa, yanapoanzishwa matawi ya CCM nje ya nchi, fujo zinazoletwa na vyama vya siasa huko Tanzania zitahamia pia nje. Utengano unaoimarika Tanzania, kutokana na siasa za vyama, nahisi utatokea pia huko nje. Na kama nilivyosema, afadhali Tanzania kuna fursa nyingi za mtu kujumuika na wengine, na hakuna upweke na matatizo ya kisaikolojia yanayohusiana na kuishi katika utamaduni wa kigeni.

Ni vema Watanzania wanaoishi nje waweke nguvu katika kuboresha mshikamano na utaifa. Watoto wa waTanzania na vijana wa kiTanzania wanaoishi nje wanahitaji kuelimishwa kuijua Tanzania, kujua historia, siasa, utamaduni na maisha ya Tanzania, na kulipenda Taifa lao. Katika mazingira ya huku nje, jukumu hili ni gumu sana. Hata waTanzania ambao ni watu wazima wanaoishi nchi za nje wana shida katika kudumisha uelewa wa nchi yao, kutokana na kuwa mbali. Wengi hawana fursa ya kwenda Tanzania mara kwa mara, na mengi yanawapitia mbali. Wangeweka kipaumbele katika kuifahamu Tanzania, ili waweze kuwafundisha pia watoto wao. Katika mazingira haya, kushughulika na matawi ya CCM ni kupoteza mwelekeo unaopasika.

Watoto, vijana, na watu wazima wanaoishi Tanzania hawana tatizo hilo, kwani wako katika mazingira muafaka ya kuifahamu nchi yao. Wanakomaa katika uTanzania, na hata wakiamua kujiunga na chama cha siasa, hakuna tatizo. Lakini je, ni sawa kwa vijana wa kiTanzania wanaoishi nje kujibidisha na CCM wakati suala la utaifa linayumba katika mazingira ya ugenini? Je, ni sahihi watoto wa kiTanzania wanaokulia nje, ambako tunashindwa kuwapa elimu kamili ya siasa ya kiTanzania, waanze maisha yao kwa kuona mfarakano baina ya waTanzania, badala ya kukuzwa katika fikra zinazoendana na ukweli kuwa Tanzania ni nchi inayozingatia sana utaifa?

Kuna wakati ziitokea taarifa za mpango wa kuanzisha tawi la CCM sehemu fulani hapa Marekani. Wazo hili lilizua hisia kali za upinzani. Sijui kama tawi hilo lilianzishwa, ila ilikuwa wazi kabisa kuwa wazo la kuanzisha tawi hilo hapa Marekani lingeleta mtafaruku miongoni mwa Watanzania. Taarifa mbali mbali zimeonyesha pia kuwa hata sehemu za Ulaya, kuanzishwa kwa matawi ya CCM kumeleta hisia kali ambazo hazichangii mshikamano miongoni mwa Watanzania.

Hali hii ingetosha kuwafanya viongozi wa CCM Tanzania kutambua kuwa kuanzishwa matawi ya CCM huku nje kunaweza kuathiri mshikamano wa Watanzania na kuleta picha mbaya kuhusu Tanzania. Watanzania walioko nje wanapaswa kuwa na umoja na mshikamano kwa kila hali ili waweze kuwa mabalozi wazuri wa nchi yetu, waweze kuwa mfano kwa Waafrika wengine tunaokutana nao huku nje, ambao wengi wao wanabaguana kwa msingi wa ukabila. Sisi Watanzania tulipokuwa Wisconsin, tukikutana pamoja na kuongea Kiswahili, baadhi ya Waafrika walikuwa wanatuuliza kama sisi ni kabila moja. Hawakuwa na namna nyingine ya kufahamu au kuelezea kitendo cha watu kuwa na mshikamano wa namna hii, nje ya dhana ya ukabila. Hayo ndio mazuri ya Tanzania na uTanzania, ambayo naamini yanatishiwa na vitendo vya kuanzishwa matawi ya CCM huku nje.

Hayo ndio mambo yanayonisumbua akilini ninaposoma taarifa za kufunguliwa kwa matawi ya CCM huku nje. Matawi ya CCM au chama kingine chochote yakifunguliwa nchini, mimi sioni tatizo. Ni sehemu ya haki na uhuru wa kila Mtanzania. Lakini picha inakuwa tofauti tunapozungumzia hali halisi ya jumuia za Watanzania wanaoishi nchi za nje. Nilitegemea viongozi wa CCM wangefanya uchambuzi wa kina wa suala hilo, lakini sijaona dalili zozote za kunipa matumaini.

Friday, January 9, 2009

Mfano Bora wa Ujasiriamali

Neno ujasiriamali linasikika sana miongoni mwa Watanzania. Wengi wanajitahidi kuanzisha shughuli mbali mbali za kutoa huduma, kuuza bidhaa, na kadhalika, kama njia ya kujiongezea kipato na kujiendeleza kimaisha.

Lakini, wengi hawana ufahamu wa siri ya mafanikio na maendeleo katika shughuli hizo. Kutokana na hilo, wengi wanashikilia imani za ushirikina. Matokeo yake katika jamii yetu yamekuwa mabaya sana, kama vile mauaji ya watu wengi. Hali hii inatisha. Kwamba watu wanaamini kuwa vitendo hivi vya kishirikina ndivyo vinaleta mafanikio ni ishara ya kukosekana elimu katika jamii yetu, ikiwemo elimu ya kuendesha miradi mbali mbali.

Napenda kuleta taarifa kuhusu mjasiriamali mmoja ninayemfahamu, ambaye naamini anaonyesha mfano wa kuigwa na wajasiriamali wa Tanzania. Anaendesha mgahawa uitwao Tam Tam, katika mji wa Minneapolis, Minnesota. Ni mtu anayejibidiisha kufahamu biashara yake, wateja, na mambo mengine kadha wa kadha. Anajua kuwa elimu ni ufunguo wa mafanikio. Taarifa hizi zimeandikwa kiIngereza, lakini wengi wataweza kuzisoma na labda kuwaeleza wasojua kiIngereza. Soma hapa na pia hapa.

Tuesday, January 6, 2009

Maongezi na Wanafunzi Wamarekani Waendao Tanzania


Leo nilikwenda kwenye mji wa Apple Valley, Minnesota, kuongea na wanafunzi wa Chuo cha Gustavus Adolphus kilichoko St. Peter, Minnesota. Mkutano wetu tulifanyia katika ukumbi wa kanisa la Shepherd of the Valley. Maongezi yangu yalikuwa sehemu ya maandalizi ya wanafunzi hao kwa ajili ya safari ya kwenda Tanzania kwa masomo ya mwezi moja. Safari yao inawafikisha Iringa, katika Chuo Kikuu cha Tumaini, na vijiji vya Tungamalenga na Ilula.

Nilikuwa nimeombwa na profesa wao nikaongee nao kuhusu masuala ya tofauti ya utamaduni wa Mwafrika na ule wa Mwamerika. Katika kujiandaa kuonana nami, wanafunzi hao walikuwa wameshasoma kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, ambacho wanafunzi wa vyuo vingi hapa Marekani wanakitumia pia, katika kujiandaa kwenda Afrika.

Baadhi ya wanafunzi hao wa Gustavus Adolphus wanasomea masuala ya afya. Nilitumia fursa ya leo kuwaeleza jinsi nilivyoingia katika shughuli ya kutafakari masuala ya tofauti baina ya utamaduni wa Mmarekani na wa Mwafrika, na jinsi ninavyopenda kuongea na watu mbali mbali kuhusu masuala hayo, wakiwemo wanafunzi, watafiti, wasafiri, na kadhalika.

Mazungumzo yetu yalidumu kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa sita kasorobo mchana. Wanafunzi waliuliza masuali mengi kutokana na yale waliyosoma katika kitabu changu, nami nilifanya kila juhudi kujibu na kutoa maelezo.

Chuo cha Gustavus Adolphus kimeshapeleka wanafunzi Tanzania kabla. Mwaka jana wanafunzi wa Chuo hiki pamoja na wale wa Chuo cha St. Olaf, ambapo nafundisha, walifanya safari ya Iringa, kwa masomo. Hao walikuwa wanafunzi wa somo la uuguzi ("Nursing.") Nilialikwa pia kuongea nao, kwenye mji huo huo wa Apple Valley, siku moja kabla ya safari yao ya Tanzania. Maongezi yalihusu masuala yaliyomo katika kitabu hicho hicho.

Nilipoandika kitabu changu, sikutegemea kuwa hata wauguzi wangekiona kinawafaa, kwani mimi sikusomea taaluma hiyo. Isipokuwa, nilipopata mwaliko wa kuongea na wanafunzi wa taaluma hii, nilianza kufahamu kilichokuwa kinawavutia.

Bila kuchelewa, nilichukua jukumu la kujielimisha, nikasoma majarida mbali mbali, na nikafahamu jinsi masuala ya utamaduni yanavyozingatiwa katika taaluma hii ya uuguzi. Juhusi hiyo ilinifanya nikiangalie kitabu changu kwa mtazamo mpya pia, nikaona kuwa nilikuwa nimeongelea masuala ya afya, usalama, vyakula, na mahusiano katika jamii, na mtazamo wa Wamarekani na Waafrika kuhusu masuala hayo yote. Hayo yote ni masuala muhimu kwa waganga na wauguzi.

Nilipokuwa narejea chuoni kwangu leo, nilikuwa na mawazo mengi kichwani. Kwa mfano niliwazia sana ukweli kwamba wanafunzi wanaotoka Tanzania kwenda kusoma Marekani au nchi zingine za nje hawapewi maandalizi ya aina hii. Wanapelekwa tu, wakajue wenyewe kuogelea au kuzama katika utamaduni wa kigeni. Hii ni hatari, na ingekuwa bora kama tungejifunza kutoka kwa hao Wamarekani.

Kwenye picha hapo juu, profesa wa hao wanafunzi ni mama aliyesimama nyuma, wa pili kutoka kulia. Mzee mwenye ndevu aliye pembeni yake, mwishoni kabisa, ni mchungaji.

Kwa taarifa zaidi za mradi huu soma hapa.

Monday, January 5, 2009

Kwa Kina na Prof. Joseph Mbele

Machi 28, 2008, yalitolewa mahojiano baina yangu na Bongo Celebrity. Kwa vile bado ninayo mawazo niliyotoa wakati ule, naona ni vema niyalete hapa pia, kama changamoto. Soma hapa

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...