Wednesday, March 30, 2011

Maskani Yangu Madison, 1980-86

Wikiendi hii iliyopita, nilipokuwa Madison kwenye mkutano wa Peace Corps, nilitembelea sehemu kadhaa nilizozifahamu tangu wakati nasoma Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison, 1980-86. Nilivutiwa kwa namna ya pekee na wazo la kutembelea maskani yangu miaka ile.

Niliingia Madison nikitokea Tanzania mwezi Agosti mwaka 1980. Sikumbuki tarehe. Lakini nilifikia mahali palipoitwa Union South, katika eneo la Chuo. Hapo nilikaa siku chache, nikingojea fedha kutoka Ofisi ya Fulbright, ambao ndio walinilipia gharama zote za masomo.

Baada ya siku chache za kukaa Union South, nilihamia Saxony Apartments, sehemu inayoonekana hapa kushoto. Jengo nilimoishi liko nyuma ya hili linaloonekana.

Saxony Apartments ilikuwa maarufu, kwa vile walikuwepo wa-Afrika wengi. Tulijisikia nyumbani.

Nadhani nilikaa hapo Saxony Apartments kwa mwaka moja na zaidi, nikahamia Mtaa wa West Wilson, namba 420, jengo linaloonekana hapa kushoto. Ni karibu na Ziwa Monona. Wa-Tanzania tulikuwa na mshikamano sana, tukitembeleana na kushirikiana katika raha na shida. Nakumbuka mikusanyiko tuliyofanyia hapa kwangu.

Miaka yangu ya mwisho mjini Madison, niliishi mahala paitwapo Eagle Heights, eneo lenye nyumba nyingi sana za wanafunzi wenye familia. Nilikuwa naishi katika nyumba hii, orofa ya juu. Ukianzia kushoto, ni dirisha la tatu na la nne.

Wikiendi hii nilipokuwa nazungukia maeneo hayo nilijiwa na kumbukumbu nyingi za miaka ile. Niliwakumbuka wa-Tanzania na wa-Afrika wengine tuliosoma wote, na mengine mengi. Yawezekana baadhi yao wataziona picha hizi na kukumbuka mambo ya miaka ile.

2 comments:

PBF Rungwe Pilot Project said...


Asante sana Profesa kwa kutushirikisha mambo ya huko Marekani wakati unasoma huko siku za nyuma. Ni watu wachache wanaopata fursa kama hiyo ya kutembelea vyuo na shule walizosoma. Naanza kuona umuhimu wa kufanya hiyo na kuona mazingira yaliyochangia kutufinyanga kitaaluma na tukawa hivi tulivyo.
Asante kwa namna nzuri ulivyooandika hiyo habari na inahamasisha.

Mbele said...

Ni kweli usemavyo. Kwa upande wangu, nashukuru kwamba nilipata fursa ya kusomea masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison, miaka ya 1980-86. Kwa masomo niliyosomea, chuo hiki kilikuwa chenye umaarufu sana duniani, na kwa wengi kilikubalika kuwa ndicho kilikuwa kinaongoza duniani. Tulikuwa tunahenyeshwa sana, lakini baada ya taabu zote niliona nimeivishwa vizuri. Ninajiamini katika masomo yale, popote duniani ninapokwenda kutoa mihadhara.

Nilikuwa mwanafunzi bora katika chuo kile, hata nikapata tuzo ya mwanafunzi bora, nikiwa ni mmoja wa wanafunzi kumi tu waliotunukiwa, kati ya wanafunzi maelfu wa shahada za juu. Siku moja Profesa Harold Scheub, maarufu duniani, ambaye alikuwa msimamizi mkuu wa tasnifu yangu ya uzamifu, aliniita pembeni akaniambia, "Inaonekana ulipata msingi mzuri sana kimasomo huko ulikotoka."

Hapo nilitambua kwa namna ya pekee maana ya elimu niliyopata Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Mkwawa High School (Iringa), seminari Katoliki za Likonde na Hanga (Ruvuma), na shule ya msingi Litembo (Ruvuma), bila kusahau msukumo wa wazazi wangu tangu nikiwa shule ya msingi.

Kama unavyosema, tunapaswa kuzikumbuka shule zetu na kushukuru kwa jinsi zilivyotujenga.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...