
Kama nilivyotamka, nilialikwa kutoa mhadhara maalum, ambao hapa Marekani huitwa "keynote address." Mada yangu ilikuwa "The Epic as a Discourse on National Identity."
Baada ya kutoa mhadhara, mtoa mhadhara alikuwa anakabidhiwa ua. Ua hilo ni shukrani ya waandaaji wa mkutano.
Hapa kushoto anaonekana Profesa Pekka Hakamies, mwenyekiti wa kamati ya maandilizi, ambaye aliniletea mwaliko.
Tulioalikwa kutoa hiyo mihadhara maalum tulikuwa watano, kila mtu akatoa mhadhara wake kwa wakati tofauti. Mhadhara wa aina hiyo hutolewa mbele ya washiriki wote wa mkutano, na unategemewa kuweka msingi au changamoto za kujadiliwa na washiriki katika vikao mbali mbali ambamo mada mbali mbali hutolewa.
Katika kuhudhuria hivyo vikao vya baadaye, nilifurahi kuwasikia washiriki mara kadhaa wakinukuu yale niliyoyosema. Katika taaluma, haya ni mafanikio. Wazo hili linaweza kuwa gumu kwa wa-Tanzania wengi kulielewa, kwani wanadhani mafanikio ni pesa. Kama huna pesa, wa-Tanzania hao wanakushangaa ukiwaambia umefanikiwa.

Ni fursa pia ya kukitangaza chuo chako. Nilipokuwa mwajiriwa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuanzia mwaka 1976 hadi 1990, shughuli zangu hizi zilikuwa zinakitangaza chuo kile. Lakini kuanzia mwaka 1991, nilivyoondoka kabisa kutokana na mizengwe ya pale, nimeridhika kabisa kuwa mwajiriwa wa Chuo cha St. Olaf na kukitangaza.
Tofauti na fikra au hisia za wa-Tanzania wengi, sijabadili uraia, na sitabadili, wala sijawahi hata kuwazia kwa namna yoyote kuchukua uraia wa Marekani. Badala yake, nimejitafutia njia kadhaa muhimu za kuitumikia nchi yangu kwa kutumia fursa za hapa ughaibuni.