Sunday, August 11, 2013

Afrifest 2013 Ilifana Minnesota

Jana, mjini Brooklyn Park hapa Minnesota, yalifanyika maonesho ya Afrifest. Afrifest ni tamasha linalofanyika mara moja kwa mwaka, likiwajumuisha watu wenye Asili ya Afrika na wengine wowote wale, kwa lengo la kufahamiana, kujielimisha, na kujipatia burdani mbali mbali. Watu wa kila aina walishiriki, wazee, vijana, na watoto.

Hapa kushoto tunawaona watoto wakiwa na mpiga ngoma maarufu hapa Minnesota. Aliwaonyesha namna ya kupiga ngoma, na pia aliwaelezea maana na matumizi ya ngoma katika tamaduni za Afrika.


Watu walikuwa wameambiwa kuwa tamasha lilipangiwa kuanza saa sita mchana. Kuanzia hapo watu walikuwa wanafika, kwa wakati wao.

Vijana kutoka benki ya Wells Fargo walifanya kazi nzuri ya kujitolea, kuwahudumia waliohudhuria. Walikuwa wamevalia tisheti nyekundu.

Hapa ni banda ambapo watu walikuwa wanajipatia chakule. Wahusika wanajua sana kuandaa vyakula, kama vile wali na kuku.Siku nzima, kulikuwa na muziki kutoka sehemu mbali mbali za Afrika. Vibao vya akina Diamond na Mr. Nice kutoka Tanzania vilisikika.


Hapa naonekana kwenye meza yangu nikiwa na vitabu vyangu. Nimekaa na mdau wangu wa siku nyingi, Ndugu Nyangweso.

Mimi kama mwalimu, mchango wangu mkubwa katika siku ya Afrifest ni kuelimisha umma kuhusu historia na masuala mbali mbali ya watu wenye asili ya Afrika, kuanzia chimbuko la binadamu Afrika, hadi himaya mbali mbali zilizojitokeza Afrika, biashara ya utumwa ndani na nje ya Afrika, ukoloni, harakati za uhuru, changamoto za leo na fursa za siku za usoni.
Yapata saa 10 na nusu alasiri, kama taarifa zilivyokuwa zimeelezea, Mheshimiwa Al Franken, seneta kutoka Minnesota, alijitokeza kwenye tamasha. Kulitokea msisimko mkubwa, kwani kila mtu alitaka kumsalimia na kuongea naye. Picha nyingi zilipigwa, ambazo ni kumbukumbu nzuri.

1 comment: