Sunday, August 25, 2013

Ziara Yangu Finland Imefanikiwa Sana

Tarehe 19 hadi 24 nilikuwa kwenye Chuo Kikuu cha Turku, Finland, kwenye mkutano wa kitaaluma. Nilialikwa nikatoe mmoja ya mihadhara maalum, "keynote address." Mhadhara wangu ulikuwa "The Epic as a Discourse on National Identity." Utafiti, ufundishaji na uandishi wangu kuanzia kwenye mwaka 1977 umekuwa zaidi kuhusu masimulizi kama yale ya Iliad, Odyssey, Dede Korkut, Sundiata, Liongo Fumo, Kilenzi, Beowulf, Gassire, Ibonia, na Kalevala. Anayeonekana pichani kulia, ni Profesa Pekka Hakamies, mwenyekiti wa jopo la maandalizi, aliyenialika. Washiriki walikuja kutoka pande mbali mbali za dunia.


Hapa kushoto niko mbele ya kanisa moja, mjini Turku. Sikupata muda wa kuingia ndani, bali nilikuwa napita hapo nje kila nikiwa njiani baina ya hoteli nilyofikia na sehemu ya mkutano, mwendo wa dakika kama 15 kwa mguu.
Jioni ya tarehe 23 nilialikwa Helsinki, kwa chakula cha jioni. Hapo nilikutana na wa-Tanzania kadhaa waliokuja kujumuika nami. Ukarimu wao sitausahau.
2 comments:

Yasinta Ngonyani said...

Natumai safari ilikuwa njema na kila kitu kilienda salama....

Mbele said...

Shukrani. Safari ilikuwa njema kabisa, yenye mafanikio. Lakini niliteseka mwa siku nyingi kabla ya kusafiri, nikiandaa mhadhara wangu. Nimechakaa, na hata baada ya kurejea tena hapa Marekani, tarehe 24, niko hoi naugulia.

Ndio shughuli zinavyokuwa, unapigika kweli kweli, ndipo uweze kutoa mchango wa maana.