Bado nina mengi ya kusema kuhusu safari yangu ya wiki iliyopita nchini Finland, kwenye mkutano. Nina kumbukumbu nyingi, na kama nilivyowahi kusema zamani, blogu yangu ni mahali ninapojiwekea mambo yangu binafsi.
Kama nilivyotamka, nilialikwa kutoa mhadhara maalum, ambao hapa Marekani huitwa "keynote address." Mada yangu ilikuwa "The Epic as a Discourse on National Identity."
Baada ya kutoa mhadhara,
mtoa mhadhara alikuwa anakabidhiwa ua. Ua hilo ni shukrani ya waandaaji wa mkutano.
Hapa kushoto anaonekana Profesa Pekka Hakamies, mwenyekiti wa kamati ya maandilizi, ambaye aliniletea mwaliko.
Tulioalikwa kutoa hiyo mihadhara maalum tulikuwa watano, kila mtu akatoa mhadhara wake kwa wakati tofauti. Mhadhara wa aina hiyo hutolewa mbele ya washiriki wote wa mkutano, na unategemewa kuweka msingi au changamoto za kujadiliwa na washiriki katika vikao mbali mbali ambamo mada mbali mbali hutolewa.
Katika kuhudhuria hivyo vikao vya baadaye, nilifurahi kuwasikia washiriki mara kadhaa wakinukuu yale niliyoyosema. Katika taaluma, haya ni mafanikio. Wazo hili linaweza kuwa gumu kwa wa-Tanzania wengi kulielewa, kwani wanadhani mafanikio ni pesa. Kama huna pesa, wa-Tanzania hao wanakushangaa ukiwaambia umefanikiwa.
Jambo linalofurahisha pia ni kuwa unapokuwa umealikwa kama nilivyoalikwa, halafu ukachangia mkutano kwa ufanisi, unakuwa umewahakikishia waandaaji kuwa hawakukosea kukualika, na unakuwa umewaridhisha washiriki kwa kuwapa mawazo na fikra mpya.
Ni fursa pia ya kukitangaza chuo chako. Nilipokuwa mwajiriwa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, kuanzia mwaka 1976 hadi 1990, shughuli zangu hizi zilikuwa zinakitangaza chuo kile. Lakini kuanzia mwaka 1991, nilivyoondoka kabisa kutokana na mizengwe ya pale, nimeridhika kabisa kuwa mwajiriwa wa Chuo cha St. Olaf na kukitangaza.
Tofauti na fikra au hisia za wa-Tanzania wengi, sijabadili uraia, na sitabadili, wala sijawahi hata kuwazia kwa namna yoyote kuchukua uraia wa Marekani. Badala yake, nimejitafutia njia kadhaa muhimu za kuitumikia nchi yangu kwa kutumia fursa za hapa ughaibuni.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Leo ni kumbukumbu ya siku ya kuzaliwa kwangu, ambayo ni tarehe 17 Agosti, 1951. Familia yangu, ndugu, na marafiki wamejumuika nami kushereh...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Kutafsiri kazi ya fasihi ni kazi ngumu ya kuchemsha bongo. Inahitaji ufahamu wa hali ya juu wa lugha husika, na pia hisia makini za kifasih...
3 comments:
Usemayo ni kweli mwalimu Mbele. Kwa msomi yoyote, kunukuliwa na wasomi wenzake ni tunu zaidi ya pesa. Ni ushahdi kuwa kama msomi una mchango kwa jamii. Na hili ndilo lengu mahsusi la usomi. Huwa nafurahi nikigundua kuwa maandiko yangu yamenukuliwa na wenzangu.
Kila la heri na uzidi kutoa mchango zaidi na zaidi.
Shukrani mkuu. Utamaduni huu wa kuthamini taaluma niliuona unafifia tangu mwaka 1986, niliporejea nchini baada ya kuwepo Marekani miaka sita nikisoma. Siku hizi hali ni mbaya zaidi, mara dufu, na vijana wa leo, ambao wanaingia katika shughuli kama hizi za kufundisha vyuoni, hawaelewi kabisa tulikotoka na hawaoni mifano ipasayo kutoka kwa wale waliotangulia. Ni pesa tu, na magari, na kadhalika.
Profesa ukifungua baa maarufu ndio unaheshimiwa, si ukichapisha kitabu muhimu cha taaluma. Fungua baa maarufu, uwe na wateja kama, wabunge, mawaziri na vigogo wengine. Halafu uwe umepaki shangingi lako hapo pembeni.
Naomba nichukue fursa hii kusema kwamba nasikitika hatukuendeleza yale mawasiliano yetu ya zamani, kuhusiana na vitabu vyetu. Naona itakuwa jambo jema tukijitahidi angalau mwaka huu kurejea kwenye mazungumzo yale.
Asante kaka. Ni kweli hatukuweza kuendeleza majadiliano yetu kuhusiana na vitabu vyetu. Nilikuwa nahangaishwa na kingine cha Kwetu ni Wapi ambacho nilipata mchapishaji akakubali kukichapisha halafu sijui "alifinywa" akaamua kuvunja mkataba. Pia niliandika kingine cha Nyuma ya Pazia kuonyesha jinsi ufisadi ulivyochukua mahali pa uwajibikaji na madili mahali pa maadili. Ni juzi tu nilimtumia kingine cha Diwani ya Mwalimu Nkwazi, hiki ni cha maishairi yanayokinzana na uwekezaji na ujambasishaji wa taifa. Sijui kama atakichapisha. Baada ya hapo mimi na mke wangu tulitunga kingine cha watoto cha WANYAMA WETU ambacho juzi aliniambia kuwa atakichapisha kwa vile kinafa kufundishia mashuleni. Kwa ufupi ni kwamba, hata kama sitachapisha, sitaacha kuandika. Kwa sasa nipo naandika kingine cha ELIMU NI UFUNGUO baada ya mimi na mke wangu kuandika kingine cha watoto cha Nkuzi's strange Friends.
Hivyo kaka ukiona kimya jua nipo mwituni nikiandika makala kwa ajili ya safu zangu na kuchapa kazi ili niishi. Nimefurahi ulipogusia uwekezaji kwenye mabaa na short time guest houses ambao unafanywa na watu wenye hata hadhi ya uprofesa kama ndugu yangu Prof J.ma Kapu... sitaki nimalizie. Umesahau kuwa baraza letu la mawaziri limejaa vihiyo walioghushi shahada kama nduguyo Emmy Nchimbi na wengine wengi.
Anyway, nadhani bado una namba yangu ya simu. Tunaweza kuongea kwenye wikendi.
Kila la heri ndugu yangu na nimefarijika kusikia toka kwako.
Post a Comment