Wednesday, June 7, 2017

Umuhimu wa Kumpigia Mbuzi Gitaa

Katika jamii yetu wa-Tanzania, usemi kwamba usimpigie mbuzi gitaa unachukuliwa kuwa ni ukweli usiopingika, busara isiyo na walakini. Ni kile kinachojulikana kama busara ya kawaida, yaani "common sense," kwa ki-Ingereza. Lakini je, mtazamo huu ni sahihi? Hili ndilo suala ninalopenda kulijadili hapa, kwa mtazamo wangu kama msomi, mtafiti na mwalimu.

Napenda kutamka wazi kuwa kwa msomi au mwalimu au mtafiti, "common sense" ni kitu cha kujihadhari nacho. Kazi ya msomi, mwalimu au mtafiti si kuzingatia, kuafiki, au kuhalalisha "common sense," bali kuhoji na kudadisi "common sense." Ndivyo alivyofanya mwelimishaji maarufu Socrates. Kuna wengi wengine, kama vile Galileo. Jamii yote ilielewa kuwa jua linaizunguka dunia, kwani kila mtu alijionea mwenyewe. Ilikuwa ni "common sense." Lakini Galileo, akiendeleza mawazo ya Copernicus, alisema kuwa ni dunia ndio inayolizunguka jua. Jamii ya Galileo ilimtia matatani, kama vile jamii ya Socrates ilivyomtia matatani.

Turudi kwenye suala la kumpigia mbuzi gitaa. Ninapenda kusema kuwa ni wajibu wa msomi, mtafiti, au mwalimu kuhoji hii busara ya jamii kwamba kumpigia mbuzi gitaa ni kupoteza muda au ni ujinga. Msimamo huu wa jamii una walakini mkubwa. Ukipiga gitaa, inatoa sauti. Je, jamii inamaanisha kuwa mbuzi hana uwezo wa kutambua na kuguswa na sauti? Kama jamii inaamini hivyo, inakosea.

Sisi ambao tulikulia kijijini tukichunga mbuzi tunajua kuwa mbuzi wana milio yao ambayo wanatumia kuwasiliana. Hata wakati wa kuchunga, tulikuwa tunaweza kutambua mlio wa mbuzi mwenye dhiki. Tulikuwa tunawaita mbuzi kwa majina tuliyowapa au kwa kupiga mluzi. Kwa hivi, jamii inakosea iwapo inaamini kuwa mbuzi hawana uwezo wa kujieleza, kutambua au kuguswa na sauti.

Suala la kulitafakari ni sauti ipi ambayo mbuzi anaitambua na kuguswa nayo, na ipi hawezi kuitambua na kuguswa nayo. Kinachohitajika si hiyo "common sense" kwamba usimpigie mbuzi gitaa, bali utafiti. Tunatakiwa kumpigia mbuzi gitaa tena na tena, kwa mitindo mbali mbali.

Utafiti hauwekewi kikomo. Hata pale tunapodhani tumepata ufumbuzi wa suala, hatupigi marufuku utafiti zaidi wa suala hilo. Badala ya kuridhika na busara ya jamii kuwa tusimpigie mbuzi gitaa, mtafiti au msomi huwaza: kwa nini nisimpigie mbuzi gitaa? Itakuwaje nikimpigia mbuzi gitaa? Ngoja nimpigie mbuzi gitaa nione kitakachotokea. Huu ndio mtazamo wa mtafiti, msomi, na mwalimu. Hii duku duku ya kujua huitwa "intellectual curiosity" kwa ki-Ingereza.

Msomi au mtafiti au mwalimu ni mtu anayetafuta elimu muda wote. Thomas Edison, mvumbuzi maarufu, alifanya majaribio ya kuvumbua na kuunda vitu akashindwa mara nyingi sana, lakini hatimaye alivumbua balbu ya umeme. Huu ndio moyo unaohitajika katika suala hili la kumpigia mbuzi gitaa. Tukitaka mfumo wa elimu wa kweli, inatubidi tujenge mtazamo na mwelekeo huu wa kutambua umuhimu kumpigia mbuzi gitaa.

Unapofanya utafiti kwa ajili ya kuchunguza suala fulani huwezi kujua matokeo yatakuwa yepi. Unaweza kupata matokeo ambayo hukutegemea. Katika majaribio yake ndani ya maabara, mwaka 1928 Alexander Fleming aliona kitu kimejitokeza kwenye kisahani kimojawapo alimoweka vitu vya kuvichunguza. Kitu hicho kilikuwa kimejitokeza bila yeye kutegemea, lakini ndicho kilikuja kubainika kuwa ni penicillin.

Kwa hivyo, mtu ukianza kumpigia mbuzi gitaa, ukawa anafuatilia kwa makini kila kinachotokea, huenda utajifunza mambo ambayo hakutegemea kuhusu tabia na hisia za mbuzi. Inawezekana ukipiga gitaa mara ya kwanza usione lolote likitokea. Lakini je, unajuaje kama hakutakuwa na mabadiliko yoyote ukimpigia mara kumi, au mara mia, au zaidi?

Kama unadhani ninatania, napenda tujikumbushe utafiti na uvumbuzi aliofanya Ivan Pavlov akitumia mbwa. Pavlov alifanya majaribio ambayo yalitoa mchango mkubwa katika taaluma ya saikolojia. Nashauri msomaji utafute taarifa za Pavlov na majaribio yake na uvumbuzi aliofanya. Huenda utakubaliana nami kuwa suala la kumpigia mbuzi gitaa si la kupuuzwa. Ni muhimu.

3 comments:

Anonymous said...

Chapisho zuri sana, naomba niliweke kwenye kundi letu wa whatsapp, likiambatana na chanzo ambacho ni blog hii.

Mbele said...

Hamna shida, ndugu anonymous. Sambaza tu. Lengo ni kueneza mawazo kama changamoto ya fikra zaidi.

Unknown said...

Asante sana Profesa Mbele. Nimesuuzika kweli na huu uchambuzi asubuhi hii ya leo. Umenifanya asubuhi yangu kuwa njema zaidi kwa kunipa moyo wa kusoma (na kuandika) zaidi, na ari ya kutafiti zaidi. Hali kadhalika, umenipa moyo wa kuendelea kumpigia gitaa zaidi huyu "mbuzi" wetu adhimu, japokuwa msisitizo wa wafurukutwa wa "common sense" ni kunisihi niache kwa kuwa ninapoteza muda wangu bure.

Pia nakushukuru sana kwa kunikumbusha Nicolaus Copernicus na machachari yake, mmoja wa Wapolishi walioacha "legacy" kamambe katika tasnia ya fizikia, hisabati uchumi na hata falsafa, na kwa kunikumbusha kina Socrates na Galileo. Unaitendea haki tasnia yako ya ualimu na uandishi sana sana tu.

Andiko zuri kabisa lililoshiba hoja.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...