Kwa miezi kadhaa nimekuwa nikiwazia kuandika ujumbe kuelezea kuwa ninamkubali Freeman Mbowe kuwa ndiye kiongozi wa kitaifa wa kupigiwa mfano. Nina sababu zangu, ambazo nitazieleza hapa.
Kabla sijafanya hivyo, nataka nifafanue kuwa mimi si mwanachama wa chama chochote cha siasa. Baadhi ya watu wamekuwa wakinibambikiza uanachama wa CHADEMA. Ukweli ni kwamba sijawahi kukanyaga katika ofisi yoyote ya CHADEMA, wala sijawahi kuiona hata kadi ya CHADEMA, isipokuwa katika picha mitandaoni. Sijawahi kuhudhuria mkutano wa CHADEMA.
Watu hao wanaonibambikiza chama sijui akili yao ikoje. Mimi ni mtu huru ninayetambua na kutumia haki yangu ya kutoa maoni na kujieleza kuhusu masuala yoyote, yakiwemo ya siasa. Nikisema jambo kuikosoa CCM, kwa mfano, sifanyi hivyo kwa sababu ya kuwa katika chama tofauti. Akili yangu haihitaji chama ili iweze kufikiri.
Baada ya ufafanuzi huo, napenda kurejea kwenye mada. Kwa nini ninamwenzi Freeman Mbowe kama kiongozi wa kupigiwa mfano? Si suala la mihemko au ushabiki. Ni suala la hoja.
Leo, katika taaluma ya saikolojia, tunaambiwa kuwa kuna aina nyingi za akili. Suala hilo kitaaluma linaongelewa chini ya kichwa cha "multiple intelligence" au "multiple intelligences."
Kufuatana na ufuatiliaji wangu wa mada hiyo, nimejifunza kwamba uongozi unahitaji aina ya akili iitwayo "emotional intelligence." Labda kwa ki-Swahili niseme akili hisia. Kwa maneno mengine, mtu mwenye akili hiyo ndiye anaumudu uongozi. Anakuwa kiongozi wa kweli.
Mtu huyo anakuwa mwenye kujitambua. Anatambua hisia zake na hisia za wengine. Kutokana na hilo, anazimudu hisia zake na hisia za wengine, kwa maana kwamba anajitawala vizuri, na anajali hisia za wenzake. Hana mihemko. Anakuwa msikivu. Watu wakitofautiana, yeye anakuwa msuluhishi. Anajenga umoja na maelewano. Anavutia watu. Watu wa kila aina wanamkubali kama kiongozi.
Mtu huyu anajiamini. Wale anaowaongoza wanakuwa huru kung'ara katika maeneo ya ujuzi wao. Yeye hawi mtu wa kutaka sifa, aonekane yeye ndio zaidi. Wenzake waking'ara kumzidi, kwake ni sawa. Vipaji vya kila moja anaviona ni mtaji wa manufaa kwa wote. Anachofanya si kuzuia vipaji hivyo visijitokeze, bali anaviratibisha kwa manufaa ya wote. Hii kwa ki-Ingereza huitwa "leveraging."
Nikirejea kwa Freeman Mbowe, ninaona anakidhi vigezo hivyo. Kuna watu wanambeza Mbowe, eti hana elimu ya kutosha. Wengine wanasema huyu ni DJ. Watu hao ni wajinga, kwa namna mbili. Kwanza hawaelewi kuwa elimu si ya shuleni na vyuoni tu. Inapatikana pia nje ya shule na vyuo. Pili hawaelewi hiyo dhana "emotional intelligence" kama kigezo na msingi wa uongozi.
Wangejua, wasingeshangaa kwa nini huyu Mbowe wanayemsema hana elimu ya kutosha, lakini ndiye kiongozi wa maprofesa, wanasheria maarufu, na kadhalika. Ni kwa sababu yeye hatingishiki na kung'ara kwa hao wenye kisomo zaidi yake. Hatingishiki na umaarufu wa wenzake, akina Tundu Lissu, Msigwa, Lema, au Halima Mdee. Wote wako naye, naye yuko nao. Hiyo ndio tabia ya mtu anayejiamini.
Kutokan na akili yake hiyo na busara zitokanazo, Mbowe amefanikiwa kuijenga CHADEMA mwaka hadi mwaka, hadi leo imekuwa ni chama kikuu cha upinzani, chenye kuongoza majimbo na miji mikubwa. Ingekuwa kuna fursa na uhuru sawa kwa kila chama kufanya shughuli zake kama inavyoelekezwa na katiba na sheria, nina hakika CHADEMA ingekuwa mbali zaidi.
Jambo jingine la muhimu sana linalonivutia kwa Freeman Mbowe ni uzalendo wake. Hata pamoja na magumu yote ambayo chama chake kinawekewa na utawala, daima anaongelea mustakabali wa Taifa. Hata mimi ambaye si mwana CHADEMA ninaguswa na hilo, kwamba anatuwazia wa-Tanzania, na nchi yetu sote, si wana CHADEMA pekee. Huyu ndiye Mbowe ninayemwona mimi.
Nimesema kuwa mimi si mwanachama wa chama chochote cha siasa. Ila napenda kusema kuwa kutokana na kwamba mimi ni mwanataaluma na mwalimu, kama ingekuwa ni lazima kuwa na chama, ningekuwa CHADEMA. Ninaona jinsi CHADEMA inavyopigania uhuru na haki zilizomo katika katiba, ikiwemo uhuru na haki ya kutoa mawazo na kujieleza, na uhuru wa mikutano.
Uhuru wa fikra ni msingi wa kustawi yale ninayofanya kama mwanataaluma na mwalimu. Elimu haistawi bila uhuru wa kutoa mawazo na kujieleza. Elimu inaihusu jamii nzima. Mikutano ni sehemu ya hiyo elimu ya jamii. Kwa hivyo, ni wazi kwangu kuwa kama ingekuwa lazima kuwemo katika chama, ningekuwa CHADEMA. Ningekuwa huko si kwa sababu CHADEMA inakidhi mategemeo yangu yote kuhusu masuala yote ya kitaifa, bali kwa sababu hii moja ambayo nimeelezea. Kama mwanataaluma ninayehitaji uhuru wa kufikiri na kutoa mawazo, na ninayetaka elimu ishamiri katika nchi yetu, ningejisikia huru kuwa na kiongozi Freeman Mbowe.