Wednesday, March 30, 2011

Maskani Yangu Madison, 1980-86

Wikiendi hii iliyopita, nilipokuwa Madison kwenye mkutano wa Peace Corps, nilitembelea sehemu kadhaa nilizozifahamu tangu wakati nasoma Chuo Kikuu cha Wisconsin-Madison, 1980-86. Nilivutiwa kwa namna ya pekee na wazo la kutembelea maskani yangu miaka ile.

Niliingia Madison nikitokea Tanzania mwezi Agosti mwaka 1980. Sikumbuki tarehe. Lakini nilifikia mahali palipoitwa Union South, katika eneo la Chuo. Hapo nilikaa siku chache, nikingojea fedha kutoka Ofisi ya Fulbright, ambao ndio walinilipia gharama zote za masomo.

Baada ya siku chache za kukaa Union South, nilihamia Saxony Apartments, sehemu inayoonekana hapa kushoto. Jengo nilimoishi liko nyuma ya hili linaloonekana.

Saxony Apartments ilikuwa maarufu, kwa vile walikuwepo wa-Afrika wengi. Tulijisikia nyumbani.

Nadhani nilikaa hapo Saxony Apartments kwa mwaka moja na zaidi, nikahamia Mtaa wa West Wilson, namba 420, jengo linaloonekana hapa kushoto. Ni karibu na Ziwa Monona. Wa-Tanzania tulikuwa na mshikamano sana, tukitembeleana na kushirikiana katika raha na shida. Nakumbuka mikusanyiko tuliyofanyia hapa kwangu.

Miaka yangu ya mwisho mjini Madison, niliishi mahala paitwapo Eagle Heights, eneo lenye nyumba nyingi sana za wanafunzi wenye familia. Nilikuwa naishi katika nyumba hii, orofa ya juu. Ukianzia kushoto, ni dirisha la tatu na la nne.

Wikiendi hii nilipokuwa nazungukia maeneo hayo nilijiwa na kumbukumbu nyingi za miaka ile. Niliwakumbuka wa-Tanzania na wa-Afrika wengine tuliosoma wote, na mengine mengi. Yawezekana baadhi yao wataziona picha hizi na kukumbuka mambo ya miaka ile.

Tuesday, March 29, 2011

Mkutano wa Peace Corps, Madison, Ulifana

Machi 24-27 nilikuwa Madison, Wisconsin, kuhudhuria mkutano wa Peace Corps, uliojumuisha waMarekani walioenda kujitolea Afrika chini ya mpango wa shirika la Peace Corps. Mwaka huu ni mwaka wa maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Peace Corps, na maadhimisho hayo yanafanyika sehemu mbali mbali hapa Marekani.

Mkutano huu wa Madison ulikuwa na mengi ya kuelimisha na kusisimua kuanzia historia ya kuanzishwa kwa Peace Corps hadi masimulizi na kumbukumbu za watu walioenda katika nchi mbali mbali za Afrika kujitolea katika nyanja mbali mbali.

Kulikuwa na masumulizi kuhusu Rais Kennedy ambaye alichangia kuotesha mbegu ya Peace Corps kwa mtazamo wake wa kuwahamasisha raia wake wawe na moyo wa kujitolea, si kwa nchi yao tu, bali kwa ulimwengu. Rais Kennedy aliweka sahihi ya kuzindua Peace Corps tarehe 1 Machi, 1961.

Kulikuwa na masimulizi kuhusu Sargent Shriver, ambaye ndiye alikuwa mwanzilishi wa Peace Corps, akiwa na moyo na ari isiyomithilika iliyowasha moto mioyoni mwa wana Peace Corps, moto ambao bado unaendelea kuwaka, ukiwahamasisha kwenda kujitolea sehemu mbali mbali za dunia, na kuishi katika mazingira yoyote.

Kulikuwa na masimulizi kuhusu Kwame Nkrumah alivyojenga shule sehemu mbali mbali za nchi yake, akakuta hana walimu. Ndipo alipomwambia Scriver kuwa wanahitajika walimu. Na Peace Corps ikafanya hima kuandaa watu wakaenda Ghana mwaka 1961. Jina la Julius Nyerere pia lilitajwa, kwani naye aliwakaribisha Peace Corps mapema hivyo hivyo.

Watu mbali mbali, kama vile mabalozi, wasomi, walimu, wajasiriamali na waandishi walikuwepo kuelezea kumbukumbu zao za Peace Corps na mtazamo wao kuhusu umuhimu wa Peace Corps katika maisha yao na ya wanadamu kwa ujumla.

Nilipata fursa ya kukutana na watu waliojitolea Tanzania, kama vile Mzee Ernie Zaremba, ambaye tulipiga hii picha. Tulipiga stori siku zote tatu kuhusu Tanzania. Yeye alijitolea miaka ya 1964-66 Mwanza, Misungwi. Mzee huyu sasa anajishughulisha na kurekodi habari za wana Peace Corps, na kuwaunganisha. Huwa anatembelea Tanzania kukutana na watu waliofahamiana na wana Peace Corps au waliofaidika kutokana na Peace Corps kwa namna moja au nyingine.

Nilipiga stori na Mark Green, ambaye alikuwa balozi wa Marekani Tanzania, 2007-2009. Nilianza kufuatilia habari za Mark Green alipokuwa balozi. Niligundua kuwa maskani yake ni Wisconsin, na kuwa aliwahi kufundisha katika kijiji fulani Kenya. Nilivutiwa na shughuli zake nchini mwetu, nikagundua kuwa tulisoma wote katika chuo kikuu cha Wisconsin-Madison, ingawa hatukufahamiana. Mimi nilimaliza shahada ya uzamifu mwaka 1986 na yeye 1987. Sote tulifurahi kufahamiana.

Kitu kimoja kilichonifurahisha zaidi katika mkutano huu ni kukutana na rafiki yangu Mwalimu Wade DallaGranna, ambaye tulifahamiana mwaka 1980, nilipofika Madison kusoma. Yeye alikuwa amerejea kutoka Lesotho, ambako alikuwa mwana Peace Corps.

Tangu nilipomaliza masomo Madison na kurudi Tanzania katikati ya mwaka 1986, hatukuwahi kukutana tena, hadi hiyo juzi. Tulifurahi sana, tukawaambia wengine pia.

Nina mengi ya kuelezea kuhusu mkutano huu, na natengemea kuendelea kuandika. Inatia moyo na hamasa kubwa kuwemo katika jumuia kubwa namna ile ya watu ambao fikra na mazungumzo yao ni juu ya kujitolea na kuwasaidia binadamu wengine, kujenga mahusiano mema duniani, na kuwaletea wengine maisha bora na mafanikio.

Monday, March 28, 2011

Dhana Duni ya Mfumo Kristo

Kila kukicha, unajitokeza ushahidi kwamba kiwango cha kufikiri miongoni mwa wa-Tanzania wengi ni duni. Siku hizi, kwa mfano, imeibuka hii dhana ya mfumo Kristo.

Walioibuni dhana hii na ambao wanaieneza wana ajenda ya kujenga hoja kuwa mfumo wa utawala na uchumi Tanzania unaendeshwa kwa misingi ya kiKristu, na kwa lengo la kuwanufaisha wa-Kristu na kuwakandamiza na kuwanyima wa-Islam fursa na haki wanazostahili, katika nyanja mbali mbali, kama vile elimu na uongozi.

Hii ndio dhana ya msingi ya hiki kinachoitwa mfumo Kristo. Wanaojenga hoja hii wanadai kuwa serikali ya Tanzania yenyewe inaendeshwa na maaskofu kama sehemu ya uendelezaji wa huu wanaouita mfumo Kristo.

Kwanza napenda kusema, kama ninavyosema daima, kuwa kila mtu ana uhuru wa kutoa mawazo yake. Uhuru huu ni pamoja na uhuru wa kuyahoji au kuyapinga mawazo ya wengine, kufuatana na mchakato wa kujielimisha na kutafakari masuala. Ni pamoja na uhuru wa kuyapinga mawazo yako mwenyewe.

Nashangaa kwa nini mfumo mbovu uhusishwe na jina la Yesu Kristu. Dini zote mbili, u-Islam na u-Kristu, zinamtambua na kumheshimu Yesu. Yesu anatambuliwa kama Mungu katika u-Kristu. Na katika u-Islam, anatambuliwa kama mtume maarufu. Dini zote zinamheshimu sana Yesu.

Kama mfumo wa Tanzania umeoza kama inavyosemwa, hauwezi kuwa mfumo Kristo. Kuuita mfumo Kristo ni dhihaka isiyo kifani. Huwezi kuuhusisha uchafu wowote na Mungu au mtume. Kama kweli maaskofu wanaendekeza na kuulinda mfumo wa dhuluma, wanakiuka mafundisho na maadili ya Kristo. Huu si mfumo Kristo. Mfumo Kristo ni mfumo wa haki na maadili aliyotufundisha Kristo.

Sidhani kama inahitaji akili ya pekee sana kuitambua hoja hii. Lakini ni wazi kuwa watu wengi Tanzania wana kiwango duni cha kufikiri au kuelewa mambo. Kwa dhana yao ya mfumo Kristo, wanaudhihaki u-Kristo, na pia wanaudhihaki u-Islam. Ila, kutokana na akili zao duni, hawatambui hilo. Kilichopo ni kuwaombea dua njema, waweze kujitambua na kujirekebisha.

Wednesday, March 23, 2011

Eti Wahadhiri Waeneza Siasa za Chuki Vyuoni

Niomeona taarifa hii hapa chini nikaona lazima niseme moja mawili, nikitumia wadhifa wangu kama mwanataaluma na mzoefu wa kufundisha au kutoa mihadhara vyuo vikuu sehemu mbali mbali za dunia.

Sio kazi ya serikali kuingia darasani chuo kikuu ili kuchunguza mwalimu anafundisha nini au anafundishaje. Hii ni kazi ya wanataaluma na wahadhiri, kufuatana na taratibu zinazotambulika katika jumuia ya wanataaluma. Taratibu hizi ni za kulinda, kutathmini, kuratibu na kuboresha viwango vya utafiti, ufundishaji na taaluma kwa ujumla.

Serikali inapaswa kutambua kuwa dhana ya chuo kikuu, duniani pote, inaendana na haitengeki na uhuru wa kitaaluma. Walimu wa vyuo vikuu sio tu wana wajibu, bali uhuru wa kufukuzia taaluma bila vipingamizi, kwa mujibu wa vigezo vya taaluma hizo vinavyotambulika miongoni mwa wanataaluma kimataifa.

Kama kuna walakini katika utendaji kazi wa mwalimu wa chuo kikuu, kama vile kutofundisha somo inavyotegemewa, wanaowajibika kuchunguza ni wanataaluma wenzake, si serikali. Serikali haitegemewi wala kuruhusiwa kuingilia uhuru wa walimu na watafiti chuo kikuu katika kufanya utafiti, ufundishaji, uandishi na kadhalika kwa misingi na viwango vinavyotambuliwa kitaaluma.

Jambo jingine la msingi kabisa kuhusu chuo kikuu ni kuwa hapa ni mahala pa tafakari na malumbano kuhusu masuala mbali mbali, kwa kiwango cha juu kabisa. Ni mahala ambapo fikra za kila aina na hoja za kila aina zinapaswa kusikika na kuchambuliwa.

Chuo kikuu cha kweli, chenye hadhi ya chuo kikuu, ni maskani ya wachochezi wa fikra na hoja, katika taaluma mbali mbali, ikiwemo siasa. Huwezi kumwambia mtafiti au mhadhiri asiiponde serikali iliyoko madarakani iwapo utafiti na tafakari yake inampeleka huko.

Dhana ya kwamba kuna wanaoeneza siasa za chuki miongoni mwa wanafunzi wa chuo kikuu ni dhana ya kusikitisha. Inamaanisha kuwa hao wanafunzi ni wajinga sana, au ni wavivu sana, ambao hawana uwezo au dhamira ya kujibidisha katika kusoma na kutafakari mambo ili waweze kugundua mapungufu ya hoja wanazosikia, na kupambana kwa hoja. Inamaanisha hao ni wanafunzi mbumbumbu, wasio na akili au wasiotumia akili. Kitendawili ni je, walifikaje hapo chuoni, kama si kwa njia za panya?

Wanafunzi wa chuo kikuu wanawajibika kuwa tayari na makini katika kupambana kwa hoja na wanafunzi wenzao na pia na walimu wao. Ni fedheha iwapo wanafunzi hao kiwango chao ni duni kiasi cha kuweza kupotoshwa na walimu wao. Hawastahili kuitwa wanafunzi wa chuo kikuu, na hicho chuo chenyewe hakistahili kuitwa chuo kikuu. Na ni fedheha kama tumefikia mahali ambapo serikali inaona ije darasani kuwanusuru hao wanafunzi feki.


------------------------------------------------------------------------------------
WAHADHIRI WAENEZA SIASA ZA CHUKI VYUONI


Chanzo:Habari Leo

Wahadhiri waeneza siasa za chuki vyuoni
Imeandikwa na Theopista Nsanzugwanko; Tarehe: 23rd March 2011


SERIKALI inawachunguza wahadhiri wa vyuo vikuu nchini wanaotumia muda mrefu madarasani kuzungumzia siasa badala ya kufanya kazi zinazohusu taaluma.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo, Serikali ina taarifa kuwa, baadhi ya wahadhiri wanatumia muda wa kutoa mihadhara ya masomo kwa kuzungumzia siasa hasa kupiga vita Serikali iliyopo madarakani.

“Tunaendelea na uchunguzi wa kuwabaini baadhi ya wahadhiri wanaojihusisha na siasa kwa kuingia madarasani na kuzungumzia siasa kwa dakika kumi kabla ya kuanza kufundisha,” amesema Mulugo.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, lengo la wahadhiri hao ni kuwafanya wanafunzi kuchochea migomo na maandamano na kupandikiza chuki baina ya Serikali na wanafunzi.

Naibu Waziri ameyasema hayo katika mkutano kati ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa na wahadhiri wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Muhimbili (Muhas), Dar es Salaam.

Mulugo amesema, ingawa si katika chuo hicho, lakini kuna taarifa katika baadhi ya vyuo vikuu, wahadhiri wanafanya hivyo na kuwaonya kuwa kazi yao ni kuelimisha na si kuwavuruga wanafunzi akili kwa kuchanganya yale wanaojifunza na siasa na akawataka kujiepusha na siasa kwa kuwa wao ni wataalamu.

“Tena siasa zenyewe ni za kupiga vita Serikali iliyopo madarakani, tutawachukulia hatua,” alisisitiza.

Kauli hiyo iliungwa mkono na Waziri Kawambwa ambaye aliongeza kuwa wahadhiri wasipojihusisha katika siasa, watasaidia kuweka utulivu katika vyuo na kuepusha migogoro.

Awali, kabla ya onyo hilo, Dk. Kawambwa alisema Baraza la Mawaziri limeazimia kuanzia Machi mwaka huu wahadhiri wastaafu walipwe pensheni sawa na wastaafu wengine serikalini.

Alifafanua kwamba uamuzi huo unatokana na malalamiko ya wahadhiri wastaafu kwamba wanapata mafao finyu kutoka Mfuko wa Pensheni wa PPF tofauti na wanaostaafu kutoka Serikali Kuu ambao hupata mafao yenye neema kutoka Mfuko wa Pensheni ya Wafanyakazi wa Serikali Kuu (GSPF).

Mbali na Dk. Kawambwa, pia Rais Jakaya Kikwete katika shughuli tofauti ya kuzindua Bodi ya Wakurugenzi ya Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Hifadhi ya Jamii (SSRA) jana, aligusia malalamiko ya wafanyakazi wote kuhusu tofauti kubwa ya sana katika utoaji wa mafao ya mkupuo na pensheni ya uzeeni.

“Utakuta wafanyakazi wenye viwango sawa vya mshahara, muda sawa wa utumishi wanapostaafu, mmoja anapata hadi mara tatu zaidi ya mwenzake aliye mfuko mwingine,” alisema Rais Kikwete.

Kutokana na tofauti hiyo aliyosema imelalamikiwa na vyama vingi vya wafanyakazi, Rais Kikwete aliagiza SSRA iangalie tofauti hiyo kwa makini na kuhakikisha kunakuwa na uwiano sawa wa mafao kati ya mfuko na mfuko, lakini akawataka pia wazingatie ustawi wa mfuko huo.

Lakini kuhusu maombi ya wahadhiri wa Muhas, kutaka kulipwa mafao kwa mkupuo kwa asilimia 50 ya mafao yao na kulipwa kwa miaka 15 baada ya kupokea mafao ya mkupuo, Dk. Kawambwa alisema bado yanafanyiwa kazi.

Kati hilo, Dk. Kawambwa alibainisha wataalamu wanaangalia suala la malipo hayo kwa kuwa limeonekana na utata unaoweza kusababisha baadhi ya mifuko kufa iwapo itapata wastaafu wengi hivyo unaangaliwa mfumo utakaotumiwa na mifuko yote.

Akizungumzia madai ya wahadhiri wa chuo hicho kuhusu posho ya nyumba ambazo hawajalipwa kuanzia mwaka jana, alisema hali hiyo ilitokana na ufinyu wa bajeti, lakini tayari wamepeleka malalamiko yao kwa Wizara ya Fedha ili walipwe katika bajeti ijayo.

Kabla ya kauli hizo za mawaziri, Makamu Mkuu wa Chuo hicho Profesa Kisali Pallangyo alielezea changamoto anazopata ikiwemo ya miundombinu michache ya chuo hicho.

Kutokana na uhaba huo wa miundombinu, kati ya wanafunzi wanne wanaostahili kujiunga na chuo hicho, ni mmoja tu anayepata nafasi wakati Taifa linakabiliwa na uhaba mkubwa wa wataalamu wa afya.

Dk. Kawambwa akijibu hoja hiyo, alisema, katika kuongeza wataalamu hasa katika masomo ya sayansi, Serikali imejipanga katika mpango wa maendeleo ya elimu ya juu kuboresha miundombinu ya vyuo hivyo ili wanafunzi wote wenye sifa wajiunge na vyuo stahili.

Sunday, March 20, 2011

Kazi ya Kunywa

Ukiondoa kazi ya kukaa vijiweni, kazi muhimu ya wa-Tanzania wengi ni kunywa. Huyu jamaa kwenye katuni ni m-Tanzania halisi. Yuko kazini, wala hafanyi mchezo. Ameshaamrisha kuwa kaunta ihamie hapa alipo, tena haraka sana.



Wako wa-Tanzania ambao wanajifunza kunywa tangu utotoni. Wanapofikia ujana wanakuwa wameshahitimu.

Kazi ya kunywa ni muhimu kwa wa-Tanzania wengi kiasi kuwa wamehamia baa, na wanaishi huko, kama nilivyoandika hapa.

Shughuli nyingi za jamii Tanzania zinawezekana tu iwapo zinaendana na kunywa. Yaani ili watu waje kwenye hizi shughuli, ni muhimu ulabu uwepo. Hata kwenye uzinduzi wa kitu kama kitabu, ni muhimu pawe na ulabu, kama nilivyoelezea hapa.

Nilisoma kwenye jarida la Tanzania Schools Collection, 1, (2009), kuwa mtoto mmoja wa miaka kumi alionekana kwenye maonesho ya vitabu Dar es Salaam akiwa mwenyewe. Mratibu mojawapo wa maonesho alipomwuliza kwa nini hakuja na baba yake, mtoto alijibu kuwa baba angefika kama kungekuwa na bia (uk. 12).

Kwa mwendo huu, naweza kusema kuwa miaka ijayo, itabidi tuwe na bia kila mahali, kuanzia shuleni hadi Bungeni.

(Katuni nimeipata katika kitabu cha Kula...Mtoto wa Bosi, kilichoandikwa na Simon Regis na kuchapishwa na Regis Art Production, Dar es Salaam. Sikumbuki ni wapi nilipata hii picha nyingine. Ningependa kuweka taarifa ipasavyo)

Friday, March 18, 2011

JK: Maprofesa Wananisikitisha

JK: Maprofesa wananisikitisha

Chanzo: Uhuru

NA JANE MIHANJI

RAIS Jakaya Kikwete amewataka maprofesa na wasomi nchini kutunga vitabu ili kukabiliana na tatizo la kushuka kiwango cha elimu, kunakochangiwa na upungufu wa vitabu vya kiada na ziada.

Amesema anasikitishwa na kitendo cha maprofesa na wasomi chini kulalamikia upungufu wa vitabu katika fani mbalimbali, huku wakikwepa kutoa mchango wa kutatua tatizo hilo.

Rais Kikwete amewata kila mmoja kwa nafasi yake, kuhakikisha anafanya jitihada za kuboresha elimu ili kuwa na kizazi kilichowiva kitaaluma.

Alisema hayo jana, mjini Dar es Salaam, alipotembelea Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Taarifa ya wizara iliyosomwa na waziri, Dk. Shukuru Kawambwa, ilieleza uhaba wa vitabu ni moja ya matatizo yanayokwamisha sekta ya elimu.

Dk. Kawambwa alisema shule nyingi zinakabiliwa na upungufu wa vitabu na katika baadhi, wanafunzi hutumia vya tofauti, tatizo linaloweza kupatiwa ufumbuzi kwa wasomi kujikita katika uandishi wa vitabu.

"Hili ni tatizo, wakati tunasoma Msoga kitabu cha Bulicheka, mwanafunzi aliyekuwa akisoma Lindi alikisoma, lakini siku hizi mambo yamebadilika," alisema rais Kikwete na kuiagiza wizara kutoa kipaumbele katika uchapishaji vitabu vya kiada na ziada.

"Lazima tupange kila mwaka bajeti ya kuchapisha vitabu vya watoto wetu, hatuwezi kuacha waendelee kuchangia vitabu kwa kuwa hili ni la kwetu, na hatuwezi kusubiri wafadhili," alisema.

Alionya fedha za vitabu, maabara na ujenzi wa nyumba za walimu zisipelekwe katika matumizi mengine.

Kwa upande wake, Dk. Kawambwa alisema wizara inakabiliwa na upungufu wa walimu wa shule za msingi na sekondari, hususan katika mikoa ya pembezoni.

Alisema pia kuna tatizo la kiwango kidogo cha ufaulu kwa wanafunzi katika mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi, sekondari na ualimu, hususan masomo ya sayansi, hisabati na kiingereza.

Waziri Dk. Kawambwa alisema ufinyu wa bajeti katika utekelezaji programu za elimu na mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu pia ni tatizo kubwa.

Akizungumzia kiwango cha ufaulu, rais Kikwete aliwataka walimu wanaotunga mitihani ya shule za msingi, sekondari na vyuo, kuacha kutunga migumu kupita kiasi, kwa kuwa yawezekana kuwa ndicho chanzo cha matatizo.

"Changamoto ya ufaulu mdogo kama mnavyodai katika masomo ya sayansi, hisabati na kiingereza pengine inatokana na ugumu wa mitihani... lakini msitunge rahisi sana," alisema na kuongeza ni lazima wahitimu wawe na viwango vinavyostahili.

Wednesday, March 16, 2011

Eti Wananchi Msiwasikilize Wapinzani

Kuna mambo mengi katika siasa Tanzania siku hizi. Katika hali ya ushindani wa kisiasa uliopo, mara kwa mara tunawasikia hao wanaoitwa viongozi wetu wakisema, pengine kwa jazba, kuwa wananchi msimsikilize fulani au msiwasikilize watu fulani. Wanaotajwa hasa ni wapinzani. Wananchi wanaambiwa wasiwasikilize wapinzani.

Kiongozi wa kweli, mwenye busara na ufahamu, hawezi kutoa kauli za namna hiyo. Kila mtu ana haki ya kusikiliza mawazo mbali mbali, yawe vitabuni, magazetini, au kwenye mikutano ya hadhara. Haki hii inapaswa kutambuliwa, kutetewa na kuheshimiwa. Yeyote anayesemekana kuwa ni kiongozi anapaswa kufahamu hilo.

Pamoja na kwamba ni haki ya kila mtu, vile vile ni sehemu ya uhuru alio nao binadamu. Kila mtu ana uhuru wa kutafuta maoni, mawazo na mitazamo ya wengine katika masuala mbali mbali. Ana uhuru wa kusoma vitabu na magazeti, au kusikiliza redio na televisheni, au kusikiliza hotuba kwenye mikutano ya hadhara.

Zaidi ya suala la haki na uhuru, kuna suala la wajibu. Wananchi wana wajibu wa kufahamu yanayoendelea nchini mwao. Ni lazima wajibidishe kutafuta taarifa, mitazamo na uchambuzi mbali mbali kuhusu masuala ya nchi yao na dunia kwa ujumla. Bila hivyo, wananchi hao watakuwa ni wajinga na maamuzi yao yatakuwa ni ya kijinga na pengine ya hatari kwa nchi yao. Kuweka vizuizi au mipaka, kwamba tuwasikilize watu fulani tu au mitazamo ya aina fulani tu ni kukiuka wajibu. Kutafuta elimu ni wajibu wa kila binadamu mwenye akili timamu.

Kwa kuzingatia hayo, kila ninapowasikia hao wanaoitwa viongozi wakiwaasa wananchi eti wasiwasikilize watu fulani, najiuliza kama tuna viongozi au la. Na kama kuna wananchi wanaoafiki maelekezo hayo yasiyo na mantiki wala tija, ni wazi kuwa bado tuna njia ndefu, na labda niseme tunaelekea kubaya, kwa kuendekeza ujinga.

Kilipopigwa marufuku kitabu cha Hamza Njozi kuhusu mauaji ya Mwembechai, nilifanya juhudi kutetea haki ya mwandishi na nilipinga kitendo cha kupiga marufuku kitabu kile. Hamza Njozi mwenyewe, kwenye utangulize wa kitabu chake kilichofuata alinishukuru kwa msimamo wangu.

Msingi huu huu wa kutetea uhuru na haki ndio nautumia katika kuwashutumu hao wanaoitwa viongozi, ambao wanawaasa watu wasiwasikilize watu fulani. Kitu muhimu ni kila mtu mwenye fikra au wazo apewe fursa kamili ya kujieleza, na wenye kupinga nao wapewe fursa kamili ya kutoa hoja zao. Kuhusu kitabu cha Njozi, msimamo wangu ulikuwa kwamba wasiokubaliana naye, waandike vitabu vyao. Kwa njia hiyo tutaelimika sana.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...