Wednesday, October 14, 2009

Mwalimu Angerudi Leo Angejisikiaje?

Makala hii imechapishwa katika KWANZA JAMII, Oktoba 13-19, 2009

Profesa Joseph L. Mbele

Imetimia miaka kumi tangu Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, alipofariki London, Oktoba 14, 1999. Ni jambo jema kutumia muda huu kumkumbuka kwa namna ya pekee, kwa mchango wake kwa Tanganyika (na baadaye Tanzania), Afrika na dunia kwa ujumla. Ni vizuri pia kutumia muda huu kutafakari mwenendo wa nchi yetu, tukilinganisha na makusudio aliyokuwa nayo Mwalimu wakati wa uhai wake.

Mchango wa Mwalimu katika harakati za kupigania Uhuru wa Tanganyika unatambulika. Akishirikiana na viongozi wengine wa sehemu mbali mbali za nchi, wa dini na rangi mbali mbali, na wananchi kwa ujumla, Mwalimu Nyerere aliongoza Tanganyika kufikia Uhuru, Desemba 9, 1961.

Hapo alitoa hotuba ambayo maneno yake ni vigumu kusahaulika, kwa jinsi yalivyoelezea kwa ufasaha hisia na matumaini ya Taifa letu changa. Mwalimu alisema, “Sisi tunataka kuwasha mwenge, na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro, ili umulike hata nje ya mipaka yetu, ulete tumaini pale ambapo hakuna matumaini, upendo mahali palipo na chuki, na heshima palipojaa dharau.”

Hotuba hii ilikuwa ni kielelezo kizuri cha malengo aliyokuwa nayo Mwalimu kwa nchi yetu. Ilisisimua nchi nzima na kuleta changamoto kwa wananchi katika ari ya kulijenga Taifa lao. Katika hotuba na maandishi yake mbali mbali, miaka yote ya maisha yake, Mwalimu Nyerere alifafanua masuala na wajibu mbali mbali wa wananchi, viongozi, na Taifa kwa ujumla. Aliweka sera ya kujenga uchumi wa kijamaa, ambamo njia kuu za uchumi zinamilikiwa na umma, kupitia serikali yao, kwa manufaa ya umma. Alielezea wajibu wa kila mtu kufanya kazi, na kupata kipato kutokana na mchango wake. Aliongelea kutokomeza unyonyaji, iwe ni wa mtu dhidi ya mwingine, au tabaka la jamii dhidi ya tabaka jingine.

Kuhusu elimu alifundisha kuwa elimu ni haki ya kila binadamu, itolewe kwa watu wote, bure. Mwalimu alifafanua wajibu wa wasomi kuwa ni kuutumikia umma. Elimu ilitakiwa iwe inayochochea udadisi wa kifikra, na kujitegemea. Alisisitiza kuwa elimu haina mwisho. Alijenga utaratibu wa elimu ya watu wazima na kisomo chenye manufaa, ili watu waweze kujiendelea katika fani mbali mbali, iwe ni ukulima, uvuvi, useremala, na kadhalika. Pamoja na kuona elimu kuwa ni namna ya kupambana na adui ujinga, elimu ilihesabiwa kuwa njia ya kuondokana na utumwa wa kimawazo na ukoloni mambo leo.

Mwalimu alijali suala la huduma za afya na matibabu, akiyachukulia mambo hayo kuwa ni haki ya kila mtu. Ingekuwa uwezo wa nchi kuwa mdogo, huduma zingepelekwa kila mahali. Na katika kuwazia hilo, akaona kuwa vijiji vya ujamaa ndio mfumo muafaka wa kuwezesha huduma kama elimu, afya, na burudani kuwafikia wananchi.

Kisiasa, Mwalimu Nyerere alisimama kidete kutetea wanyonge na kujenga misingi ya demokrasia ya wakulima na wafanyakazi. Muda mfupi tu baada ya Uhuru, Mwalimu aliandaa na kutangaza Azimio la Arusha na miongozo mbali mbali ya kujenga usawa katika nchi yetu.

Mwalimu Nyerere alishughulikia utamaduni pia, akihamasisha watu kuuthamini utamaduni wao, maadili, lugha, na sanaa. Mwalimu aliipa kipaumbele lugha ya kiSwahili akaifanya lugha ya Taifa. Aliitumia katika hotuba na maandishi yake, kuanzia insha hadi mashairi. Alitafsiri tamthilia za Shakespeare: “The Merchant of Venice” na “Julius Caesar” kwa kiSwahili, akathibitisha utajiri wa lugha ya kiSwahili na pia kuwafungulia waTanzania milango waone utajiri uliomo katika falsafa na uandishi wa bingwa huyu ambaye alisifiwa pia sana na Shaaban Robert.

Mwalimu alitambua kuwa nchi yetu msingi wake mkuu ni wakulima. Kwa hivi alijibidisha kujenga sera ya kuleta maendeleo vijijini. Kufuata na hali halisi ya nchi yetu, aliona kuwa njia muafaka ni viijiji vya ujamaa. Sera hii ilikuwa na lengo la kuleta maendeleo vijijini katika usawa na kujitegemea. Ni sera aliyoifafanua mara kwa mara, kuanzia pale alipotangaza Azimio la Arusha.

Taifa letu lilihitaji kuwa na sera kuhusu uhusiano wetu na nchi zingine na nafasi yetu duniani. Mwalimu alisisitiza kuwa nchi yetu ni huru na haifungamani na upande wowote. Tuko tayari kuwa marafiki na nchi yoyote kwa misingi ya kuheshimiana. Hatumruhusu rafiki yetu kutuchagulia maadui zetu.

Kwa vile watu wengi Afrika na duniani walikuwa bado wanapigania uhuru na ukombozi, nchi yetu ilikuwa na msimamo wa kuunga mkono harakati za ukombozi duniani kote. Tulikuwa bega kwa bega na wenzetu katika nchi za kusini mwa Afrika, Palestina, Sahara Magharibi. Tuliunga mkono harakati za Wamarekani weusi, na kadhalika.

Maisha yake yote, Mwalimu alizingatia mwelekeo huo. Hakuwahi kuchepuka kutoka kwenye imani yake juu ya Ujamaa. Wako ambao wanadai kuwa aliwahi kusema kuwa Ujamaa umeshindwa. Madai hayo hayana ukweli. Hakuna ushahidi ambao umetolewa kwamba Mwalimu aliwahi kusema kuwa Ujamaa umeshindwa. Ni uzushi tu ambao wengi wameusikia na wanaurudia kama vile ungekuwa ukweli.

Leo hii Tanzania haifuati mwelekeo wa Mwalimu. Wazo la kujenga uchumi unaojitegemea limetupwa kando. Badala ya kuendeleza malengo ya Azimio la Arusha, kuyaweka katika hali ya kuendana na mazingira ya leo, chama tawala cha CCM kilileta Azimio la Zanzibar, ambalo Mwalimu Nyerere alilishutumu. Azimio la Zanzibar lililegeza masharti ya uongozi yaliyowekwa miaka iliyotangulia.
Leo tunaongelea kukua kwa uchumi, lakini si mgawanyo wa mali katika jamii. Nchi yetu ina matabaka, na tofauti kati ya matajiri na maskili inazidi kuwa kubwa. Hii ni hali ya hatari kwa siku za usoni.

Kwa sera zake, kama zilivyotamkwa katika Azimio la Zanzibar, CCM ilifungua milango ambayo hatimaye imeuwezesha ufisadi kuota mizizi na kustawi katika nchi yetu. CCM haishughuliki katika kudumisha urithi wa Mwalimu Nyerere. Inaonekana wazi kuwa CCM ingependa fikra za Mwalimu Nyerere zisahaulike, kutokana na ukweli kuwa CCM imeachana na fikra hizo, na pia kwa miaka mingi kabla hajafariki, Mwalimu Nyerere alikuwa anaishutumu na kuikosoa CCM.

Mara kwa mara zinapatikana taarifa za namna watu sehemu mbali mbali za dunia wanavyomwenzi Mwalimu Nyerere. Lakini tukifananisha na Tanzania tunaona kuwa nabiii huheshimiwa, isipokuwa nchini kwake. Hata hivi, tunayo fursa ya kujirekebisha, na dalili za kuleta matumaini zipo. Kwa mfano katika maadhimisho ya kifo cha Mwalimu Nyerere mwaka huu, Taasisi ya Mwalimu Nyerere itatoa vitabu kadhaa vya maandishi ya Mwalimu, yakiwemo maandishi ambayo hayajawahi kuchapishwa. Habari hii inaleta matumaini.

Napenda kumalizia kuwa niliyoandika hapa ni dondoo tu. Kila kipengele kinastahili makala ya pekee, hata kitabu. Lakini nina suali: je, leo hii Watanzania tunaweza kudiriki kusema kuwa tuwashe mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro kwa lengo la kuleta matumaini, upendo na heshima kwa wenzetu ulimwenguni? Ni nani duniani anayetuangalia leo akatamani kuwa kama tulivyo? Mwalimu Nyerere angerudi nchini leo, angejisikiaje?

2 comments:

Simon Kitururu said...

Nikikunukuu Prof: ''je, leo hii Watanzania tunaweza kudiriki kusema kuwa tuwashe mwenge na kuuweka juu ya Mlima Kilimanjaro kwa lengo la kuleta matumaini, upendo na heshima kwa wenzetu ulimwenguni? Ni nani duniani anayetuangalia leo akatamani kuwa kama tulivyo? Mwalimu Nyerere angerudi nchini leo, angejisikiaje?''


Sijui kwa nini, ILA mimi binafsi naamini Watanzania bado tunaweza kudiriki kusema Mwenge wetu Mlima Kilimanjaro unaweza kuleta upendo na heshima kwa wenzetu ulimwenguni.

Mimi naamini ni asilimia ndogo ya Watanzania ndio imepoteza maadili.

Na naamini hakuna kitu kibaya kama kufa moyo na kufa tumaini. na tumaini langu lina nuru kwa kuwa naamini kuwa Watanzania wengi wanaanza kuamka na kustukia yafanywayo na wachache ambayo ndio yauayo tumaini.

Na naamini Tanzania kama glasi inategemea na uiangaliavyo ki-Half FULL or HAlf empty. Na naamini kimtazamo fulani hata majirani zetu BADO wanatamani wangekuwa kama Tanzania.


Na haipingiki , Mwalimu angejisikia vibaya angerudi leo.:-(

Lakini kama Mwalimu , kazi ya mwalimu baada ya kujisikia vibaya baada yakustukia wanafunzi wake wamefeli, naamini kwa kawaida Mwalimu huanza upya kuandaa somo baada ya kuangalia ni kwa nini wanafunzi hawaelewi. Siamini Mwalimu Nyerere ni aina ya mtu mwenye kukata tamaa kirahisi na kwa hilo labda ingeawaamsha wanafunzi wake ambao wamejisahau na picha ndogo kwa kukwepa kuangalia PICHA KUBWA ni nini.

Mbele said...

Ndugu Kitururu, shukrani kwa mchango wako. Nami naamini kuwa Mwalimu Nyerere hakuwa mtu wa kukata tamaa. Hadi siku za mwisho za maisha yake, aliamini kuwa njia ya Azimio la Arusha ilikuwa ndio njia sahihi, pamoja na matatizo na upuuzi uliofanyika kulivuruga Azimio. Naamini angerudi leo angekuwa anaendelea kuelezea umuhimu na wajibu wa kupambana na mfumo hasi wa ubepari ambao umetuletea majanga tangu zamani za utumwa na ukoloni, na bado unaendelea kutuletea hayo majanga.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...