Wednesday, April 6, 2011

Mijadala ya Dini ni Muhimu

Watu wengi katika jamii yetu wanasema kuwa tusiendekeze mijadala ya dini. Wanasema kuwa ni tishio kwa amani na maelewano. Ninapenda kutafakari suala hilo.

Binafsi, naamini kuwa watu wenye akili timamu wanaweza kujadili mada yoyote bila matatizo. Watu wa aina hiyo wanajua kuwa katika mjadala wanachopaswa kufanya ni kutoa hoja, kusikiliza hoja, na kupinga hoja kwa hoja.

Watu wenye akili timamu wanafahamu kuwa, katika mjadala, kila mtu ana uhuru wa kuelezea fikra zake na mtazamo wake, na ana haki ya kusikilizwa. Na kila mtu ana wajibu wa kusikiliza hoja na mtazamo wa wengine.

Suala la mijadala, kwa watu wenye akili timamu, ni suala lililojengeka katika haki, uhuru, na wajibu, kama nilivyoelezea hapo juu. Wajibu huo ni pamoja na wajibu wa kuheshimiana katika hiyo mijadala. Kwa maana hiyo, mada yoyote inaweza kujadiliwa na watu wenye akili timamu, iwe ni siasa, uchumi, au dini.

Kuna pia wajibu wa kujielimisha. Mbali ya kwenda shule, au kusoma vitabu, mijadala ni njia mojawapo muhimu ya kuelimishana. Siamini kama dini zetu zinatutegemea tuwe waumini mbumbumbu. Naamini kuwa Muumba mwenyewe anatutegemea tuwe waumini tunaojibidisha kuzifahamu dini zetu. Kwa hivi, kusoma kuhusu dini na kushiriki mijadala kuhusu dini ni wajibu.

Sasa tatizo liko wapi, inapokuja kwenye dini, hadi watu waseme kuwa tusiendekeze mijadala ya dini? Tatizo si mada, bali vichwa vya wahusika. Labda ni wajinga au walevi. Hili ndilo tatizo. Wajinga au walevi wakipewa mada yoyote, uwezekano wa kushikana mashati ni mkubwa. Hata kama mada ni kuhusu umuhimu wa kujenga hospitali au kupeleka watoto shule, wajinga au walevi wanaweza kushikana mashati.

Suali ni je, kwa nini mada yoyote iwe ni hatari kujadiliwa? Na tukisema leo tusijadili dini, huenda kesho tutasema tusijadili siasa, na keshokutwa tusijadili elimu, na kadhalika. Kwa nini mada yoyote iwe ni hatari kujadiliwa? Inamaanisha kuwa wa-Tanzania ni wajinga au walevi?

Kama ni walevi, tupunguze ulabu. Kama ni wajinga, kinachopaswa kufanya ni juhudi za kufuta ujinga, ili tufikie mahali wa-Tanzania wawe na akili timamu kama nilivyoelezea hapo juu. Tunahitaji maandalizi ili mada kama dini ziweze kujadiliwa sawa na mada zingine, kuchangia elimu na maelewano.

3 comments:

Albert Kissima said...

Prof Mbele, nashukuru kwa kuwekea msisitizo jambo hili. Watu wameshajengewa/jijengea dhana ya kuwa mambo yahusuyo dini/imani, hayapaswi kujadiliwa maana hayana majibu. Mijadala inayomuhusu Mungu mathalani, watu wanawoga wa kujadili maana "sikio haliwezi kuwa kubwa kuliko kichwa"; haiwezekani kumjadili aliyetupa uhai, ni kufuru. Dini nyingi zinaambatana na vitisho ambavyo huwajengea waumini hofu ya kuhoji au kujadili mambo yahusuyo dini.

Mbele said...

Shukrani kwa ujumbe. Ni kweli usemavyo, kwamba watu tumejijengea hiyo dhana na hofu.

Nadhani tatizo letu ni ubabaishaji. Kama kweli mtu umejengeka vizuri kama mu-Islam, kwa mfano, au m-Kristu, au m-Hindu, na kadhalika huwezi kutetereka na mijadala. Imani yako katika dini yako kama ni imara, na unajua kabisa kuwa dini ni imani, haiwezi kutishiwa na dini ya wengine, ambayo nayo imejengeka katika imani.

Sasa suali la kuwauliza hao waoga ni hili: Imani ya fulani iweje tishio kwa imani yangu? Hapo ndipo ninapoona ubabaishaji.

Sasa kutokana na huu ubabaishaji ndipo tunapata hivi vitisho.

Anonymous said...

nakupa tano Professa.

Huwa najoiuliza, hata haki za kawaida bongo huseama watu wakidai basi amani itavunjika.

Hivi si kweli kuwa kuwepo kwa amani ndo nyenzo (tool) bora ya ku-maximize upatikanaji wa haki?

"making the most out of peace" au kuichuma amani.


Kwa nini watu wabadilishe haki yao kwa amani ambayo wadhani atavunjika wakati sivyo?

Huu si usemi tuu wa kulinda ubwanyeye na ukandamizaji kadhaa wa serikali au vibosile?

kwa nini kukompromize haki? hiyo so ndo itavunja amani?

hata hapa US najuwa watu wanasema kuwa anaye-compromize liberty kwa amani kadhaa hastahili vyoote amani wala haki.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...