Tarehe 11 Juni, katika mji wa Brooklyn Park, Minnesota, yalifanyika maonesho ya utamaduni wa Afrika, kama nilivyowahi kutangaza katika
blogu hii. Kulikuwa na hotuba mbali mbali kuhusu masuala kama afya na mengine mengi.

Kulikuwa na ngoma za watu wa Kamerun ambao wanaonekana hapa kushoto. Tena mmoja wa wachezaji ni mwanasheria maarufu hapa Minnesota, ambaye tumefahamiana miaka kadhaa. Alikuwa anayarudi magoma sawa na mtu wa kule kijijini.

Wadau wa aina aina walikuja kwenye maonesho hayo. Kwa upande wa Afrika Mashariki, walikuja wa-Kenya wengi na wa-Ganda, na kulikuwa na meza zao ambapo waliweka majina ya nchi zao. Hapakuwa na meza ya Tanzania, yenye bendera ya nchi kama ilivyokuwa kwa wenzetu. Mdau mmoja kutoka Ethiopia aliniuliza inakuwaje hakuna meza ya wa-Tanzania, wakati wengine wa Afrika Mashariki wana meza. Mimi natoka mji wa mbali, na nilikuwa nimejilipia maonesho hayo kama mtu binafsi sio kama mwakilishi wa Tanzania. Labda wa-Tanzania tusaidiane kutoa maelezo, maana nimeongelea sana kwenye blogu hii na zingine suala la wa-Tanzania kutoonekana kwenye shughuli za aina hii, zinazojumuisha mataifa mbali mbali. Tunakwenda kinyume na alivyotufundisha Mwalimu Nyerere.

Shirika moja dogo la wa-Marekani linaloshughulikia tatizo la kipindupindu Tanzania lilikuwa na meza ambapo taarifa mbali mbali zilikuwepo. Niliongea sana dada Katie JohnsTon ambaye ni mhusika. Yeye na mwenzake mmoja wanajiandaa kwa safari ya Tanzania.

Hapa kushoto kuna meza ya vitu kutoka Kamerun.

Akina mama kutoka Senegal na Togo walionesha vitu mbali mbali vya kwao, zikiwemo nguo, vikapu na vinyago.

Kulikuwepo pia na maonesho ya mitindo ya mavazi. Hapa kushoto anaonekana mwendeshaji wa shughuli hii, Dr. Woldu, aliyevaa nguo nyeupe, na msichana akipita na vazi mojawapo.

Fasihi simulizi na andishi ni sehemu muhimu ya utamaduni. Mimi kama mtafiti hurekodi urithi huo na kuuandikia makala na vitabu. Hapa kushoto anaonekana binti yangu akinisaidia kuonesha na kuelezea kazi zangu hizo. Nimemzoesha tangu alipokuwa mdogo zaidi, na anaweza kuniwakilisha hata kama nimesafiri.

Hapa kushoto niko na mwendeshaji mojawapo wa maonesho haya, Dr. Samuel Woldu kutoka Ethiopia. Mwenye shati la kitenge ni Bwana Albert Nyembwe kutoka Kongo Kinshasa. Ni mwanzilishi na mkurugenzi wa taasisi ya
Cilongo. Pia ni shabiki na mpiga debe mkubwa wa maandishi yangu.

Watoto wa umri mbali mbali, walikuwepo. Hawakuwa watazamaji tu, bali wengine walishiriki kwa vitendo, kama vile nyimbo.

Kwaya ya wa-Kenya iliimba nyimbo mbali mbali, tena kwa kiSwahili. Tukizingatia kuwa lugha ni msingi mkubwa wa utamaduni, hao wa-Kenya walituwakilisha vizuri sisi watu wa Afrika Mashariki.

Kule nyuma kwenye kibanda cha Knight's Cafe akina mama walikuwa wanauza vyakula kutoka sehemu mbali mbali za Afrika. Hapo nilinunua na kuonja chakula kutoka Togo. Sio jambo gumu kuelewa jinsi utamaduni ulivyofungamana na chakula. Kwa kiasi kikubwa chakula ni utambulisho wa utamaduni.