Thursday, October 8, 2015

Wanafunzi Wangu wa Ki-Ingereza

Ni yapata mwezi sasa tangu tuanze muhula mpya wa masomo hapa chuoni St. Olaf. Ninafundisha kozi mbili, South Asian Literature na "First Year Writing." Hii ya kwanza ni kozi ya fasihi ya ki-Ingereza kutoka India, Pakistan, na Sri Lanka. Ya pili ni kozi ya uandishi wa ki-Ingereza. Picha hii kushoto, ya darasa la ki-Ingereza (FYW), tulipiga leo. Mwanafunzi mmoja hayumo. Niliweka picha ya darasa kama hili katika blogu hii.

Nilipenda ualimu tangu utotoni. Ninawapenda wanafunzi. Ninawaambia hivyo tangu siku ya kwanza ya masomo, nao wanashuhudia hivyo siku zote. Wanajionea ninavyojituma kuwaelimisha kwa uwezo wangu wote na kwa moyo moja. Sina ubaguzi, dhulma, wala upendeleo. Hiyo imekuwa tabia yangu tangu nilipoanza kufundisha, mwaka 1976, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Ninajivunia jambo hilo.

Kwa miezi mingi, hasa mwaka jana, afya yangu haikuwa njema, na nilichukua likizo ya matibabu. Ingawa nimeanza tena kufundisha, inatokea mara moja moja kwamba sijisikii vizuri. Juzi ilitokea hivyo, ikabidi niwaambie wanafunzi hao waendelee kuandika insha niliyowaagiza kabla, nikawaaga.

Jana, nilipofika ofisini, nilikuta kadi mlangoni pangu, ambayo picha yake inaonekana hapa kushoto. Wanafunzi hao walikuwa wameniandikia hiyo kadi na ndani walikuwa wamesaini majina yao. Maneno yanayoonekana pichani yanatokana na michapo yangu darasani. Nilivyoipata kadi hii, niliguswa. Nimewaambia hivyo leo, tulipoanza kipindi.

Ualimu si kazi rahisi. Inahusu taaluma. Inahusu malezi. Inahusu kuwashauri na kuwasaidia wanafunzi katika hali mbali mbali za maisha. Lakini, hayo ndiyo mambo yanayonivutia katika ualimu. Mafanikio ya wanafunzi masomoni na maishani ndio mafanikio na furaha yangu.

2 comments:

Pascal Bacuez said...

Asalam aleikum Mzee Mbele, hapo leo posti yako imenifurahisha kwa kuwa ni sahihi kabisa, ualimu ni kazi ngumu ! Ila hapo kwenye ujumbe waliokuachia wanafunzi wako, wasingeandika "ukajiliwaze kwenye mvungu wa mwembe ! Hawajui kwamba utapata makepu ! Uwafundishie basi, utamaduni huo ! Wasalaam

Mbele said...

Aleiku salaam, Mzee Pascal Bacuez. Ajabu, nami leo nimetembelea blogu yako ya Kimbilio, kama kawaida yangu, halafu nimekuja hapa kwangu nikaona umepita hapa. Shukrani.

Hao wanafunzi wangu wananikumbusha michapo yangu ya darasani. Hili dhana ya "chini ya mwembe" nimewahi kuwaambia, kwamba nangojea siku ya kustaafu na kurudi kijijini kwangu, nikajumuike na wazee wenzangu chini ya mwembe, tukimwaga maneno ya busara kwa vijana.

Wanafunzi karibu wote ni wa-Marekani, na wengi hawafahamu hata hizo dhana kama "Asalaam aleikum," au "Insh'Allah." Huwa nawafundisha, na nazitumia darasani, na wao wanapenda kuzitumia.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...