Thursday, November 26, 2015

Utendi wa Mikidadi na Mayasa

Wiki hii, bila kutegemea, nimevutiwa na wazo la kusoma Utendi wa Mikidadi na Mayasa. Ninazo tendi kadhaa, kuanzia za zamani kama vile Mwana Kupona, Fumo Liongo, na Ras il Ghuli, hadi za enzi zetu hizi. Ninapenda kuzisoma na kuzitafakari, sambamba na tungo za aina hiyo za mataifa mengine, kama vile Gilgamesh, Iliad na Odyssey, Sundiata, na Kalevala.

Nimeusikia Utendi wa Mikidadi na Mayasa tangu zamani. Sijui lini nilinunua nakala yangu ya utendi huu, lakini sikupata wasaa wa kuusoma. Kwa kuupitia haraka haraka, nimeona kuwa una mambo yanayofanana na yale yaliyomo katika tendi zingine maarufu za ki-Swahili kama Ras il Ghuli. Kwa mfano, dhamira ya mapigano kama njia ya kuthibitisha ushujaa imejengeka katika Utendi wa Mikidadi na Mayasa, kama ilivyo katika Utendi wa Ras il Ghuli.

Mayasa ni shujaa mwanamke anayenikumbusha shujaa mwanamke aitwaye Dalgha katika Utendi wa Ras il Ghuli. Wote wawili ni wapiganaji hodari na hatari sana, ambao yeyote anayetaka kuwaoa sherti kwanza apigane nao na kuwashinda. Hata ungekuwa mwanamme hodari na jasiri kiasi gani, kupambana nao ni kama kujitakia aibu au kifo.

Baada ya kuonja mvuto wa  Utendi wa Mikidadi na Mayasa, ninajizatiti kuusoma kikamilifu. Nikiweka nidhamu nikamaliza kuusoma, nitafurahi kuandika juu yake katika blogu hii, angalau kifupi, kama nilivyoandika juu ya Tenzi Tatu za Kale.

No comments: