Saturday, December 19, 2015

Kuchapisha Vitabu Mtandaoni

Kutokana na taarifa ninazoandika katika blogu hii, na sehemu zingine, watu wengi wanafahamu kuwa nimechapisha vitabu vyangu mtandaoni. Nimeshawasaidia waandishi kadhaa wa mataifa mbali mbali kuchapisha vitabu vyao kwa mtindo huo. Kwa upande wa Tanzania, niliwahi kuongea na wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kuhusu suala hilo, na nilinukuliwa katika gazeti la Mwananchi.

Mara kwa mara, watu huniulizia kuhusu kuchapisha vitabu vyao. Napenda kuongelea tena suala hili, hasa matokeo ya kuchapisha vitabu mtandaoni. Kwanza, ni muhimu kufahamu kwamba kuna njia nyingi za kuchapisha vitabu mtandaoni. Ni juu ya mwandishi kuchagua. Binafsi, ninatumia njia ambayo ni rahisi kabisa, isiyo na gharama, au yenye gharama ndogo kiasi kwamba haiwi kizuizi kwangu.

Kuchapisha kwa namna hii ni rahisi sana. Mbali ya kutokuwa na gharama, haichukui muda, ili mradi mswada umeshaandaliwa kama faili la kielektroniki. Kinachobaki ni kuuingiza mswada kwenye tovuti ya kuchapishia, na haichukui dakika kumi kumaliza shughuli hii na kitabu kikawa tayari kununuliwa na watu popote ulimwenguni.

Jambo moja linalovutia sana katika kuchapisha vitabu mtandaoni kwa namna nifanyavyo ni kwamba vitabu hupatikana bila kikomo. Vinahifadhiwa kama mafaili ya kielektroniki, na huchapishwa kama kitabu halisi pale tu mdau anapoagiza nakala. Akiagiza nakala moja, inachapishwa hiyo hiyo. Akiagiza mia au elfu ni hivyo hivyo. Hakuna udhia wa kutunza shehena ya vitabu ghalani na kungojea wateja, huku vikiwa katika hatari ya kuharibiwa na unyevu, mende, au panya.

Hata hivi, nimeona kuna matatizo. Kwanza kwa upande wa mnunuzi. Ni lazima awe na namna ya kununua mtandaoni. Kwa kawaida hii inamaanisha awe na "credit card" kama vile VISA na Mastercard. Jambo la pili ni bei. Nikiangalia vitabu vyangu, naona wazi kuwa kama vingechapishwa mahali kama Tanzania kwa mtindo wa jadi, vingekuwa na bei nafuu kuliko ilivyo sasa.

Lakini, kwa upande mwingine, kama kitabu kinachapishwa kama kitabu pepe, yaani "e-book," kinaweza kuuzwa kwa bei ndogo sana, kuliko bei ya kuchapisha kwa mtindo wa jadi. Mdau anatakiwa awe na kifaa cha kuhifadhia na kusomea kitabu pepe, yaani "e-reader" au "e-book reader," kama vile Kindle au Nook.

Pamoja na kuwepo kwa vitabu pepe na vifaa vya kuhifadhia na kusomea vitabu hivyo, imethibitika tena na tena kwamba wadau wengi bado wanavitaka vitabu vya jadi, yaani vya karatasi na majalada. Mazoea haya na mapenzi ya vitabu vya jadi yamejengeka na hayaonekani kutoweka mioyoni mwa wengi.

Tekinolojia ya kuchapisha vitabu mtandaoni inawaathiri wachapishaji wa jadi kwa namna mbali mbali. Kadiri siku zinavyopita, wengi wao wanaona faida ya kuchapisha vitabu mtandaoni. Tekinolojia hii mpya inawasukuma kwenda na wakati ili wasipoteze biashara katika mazingira ya ushindani na mabadiliko yasiyoisha.

12 comments:

Theo said...

Nashukuru Profesa kwa maelezo hayo yakinifu kuhusu kuchapisha vitabu kwa njia ya mtandao.Aidha, changamoto hiyo ya bei naona pengine yawezekana kuwa kuzuizi kikubwa cha watu kuweza kununua vitabu vilivyochspishwa kwa njia hiyo. Kwa upande wa visa, master cards angalau kwa shehemu kubwa imewezeshwa na mabenki Mengi ya hapa Tanzania.

Mbele said...

Ndugu Theo, shukrani kwa ujumbe wako. Sijafuatilia kwa karibu maendeleo ya huduma za mabenki nchini Tanzania, kwa hivi nashukuru kwa taarifa yako. Ingawa nimeongelea gharama ya vitabu, lakini katika mkabala mpana zaidi hoja yangu ya miaka mingi imekuwa kwamba bei ya vitabu si tatizo ukizingatia kuwa wa-Tanzania kwa ujumla wanatumia hela nyingi zaidi katika mambo kama sherehe na bia.

Hata hivi, ninaamini kuwa zikifanyika juhudi endelevu za kuelimisha umma, tutafikia wakati ambapo watu watatambua umuhimu wa kuwekeza katika vitabu. Itawezekana kuwafanya watu waelewe kuwa kadiri siku zinavyopita, dunia inazidi kwenda kwa msingi wa "knowledge economy." Kwa ufahamu huu, watu wataona ulazima wa kuwekeza katika vitabu na nyenzo zingine za elimu na maarifa.

Unknown said...

Aksante Prof. kwa taarifa nzuri sana ya kuchapisha vitabu mtandaoni.

Mbele said...

Ndugu Mlengela

Shukrani kwa ujumbe wako. Nimefurahi umetembelea hapa kwangu. Miaka mingi imepita tangu tuonane pale Diamond Jubilee, Dar es Salaam, kwenye tamasha la Tripod Media. Nakutakia kila la heri.

manotajunior said...

Asante sana profesa kwa maelezo mazuri, mimi pia ni mmoja wa waandishi lakini bado sijapata fursa ya kutoka itakuwa vizuri kama utanicheki kwenye email yangu manotajunior@gmail.com nipate mwongozo wako zaidi nina vitabu viwili mpaka sasa ila bado sijafanikiwa kuvipublish hivyo profesa naomba tuwasiliane kweny hyo email yangu kwa mwongozo zaidi.

Mbele said...

Ndugu manotajunior

Kwanza, hongera kwa kujibidisha katika uandishi. Unaweza kuniandikia kwa kutumia anwani hii africonexion@gmail.com.

Unknown said...

Nakaribia kufungua website yangu ya kuuza vitabu mtandaoni, itajulikana kwa jina la www.makavazi.com nawakaribisha muuze vitabu vyenu mtandaoni pia tunatoa huduma ya uhariri wa vitabu kwa waandishi

Mbele said...

Ni wazo zuri, Jacob Maganga Media. Kila la heri.

John Chacha said...

Nimevutiwa na maelezo yako ili naomba mawasiliano yako tuwasiliane kwa kuwa hivi karibuni natarajia kutoa kitabu ambacho naamini kitawavutia watanzania wengi kutokana na mpangilio na mambo niliyoandika.

Mbele said...

Ndugu John Chacha

Shukrani kwa kutembelea hapa kwetu na kuandika ujumbe. Hongera kwa kuandika kitabu. Ushauri wangu ni kuwa andika ujiridhishe kwamba umeandika kwa ustadi kabisa, kadiri ya uwezo wako. Hiki kiwe kipaumbele na kigezo cha msingi. Kuhusu wa-Tanzania, usiwategemee sana, kwani utamaduni wa kununua na kusoma vitabu, au hata kusoma vitabu vya bure vilivyoko maktabani, ni tatizo. Maktabani utawakuta zaidi wanafunzi, ambao wanawania kufaulu mitihani.

Usiwawazie sana wa-Tanzania. Kitabu bora husomwa popote duniani, kiwe ni cha taaluma au fasihi. Taaluma haitambui mipaka ya nchi, na fasihi bora ni hivyo hivyo.

Kuhusu mawasiliano nami, unaweza kutumia africonexion@gmail.com

onesmo mkepule said...

Asante sana Prof kwa kutufumbua macho juu ya uchapishaji wa vitabu mtandaoni.

Unknown said...

Shukran professa, ntakucheki kwa e-mail

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...