Sunday, May 14, 2017

Vitabu Nilivyonunua Leo

Leo nilikwenda tena Apple Valley, kwa muda mfupi, nikaingia katika duka la Half Price Books. Niliangalia kwanza sehemu vinapowekwa vitabu vya Hemingway au juu ya Hemingway. Kitabu cha pekee nilichokiona, ambacho nimekifahamu kwa miezi kadhaa ila sijakinunua, ni Hemingway's Boat: Everything He Loved in Life, And Lost, kilichotungwa na Paul Hendrickson.

Nilielekea sehemu ambapo huwekwa vitabu vya bei rahisi kabisa. Kwa kuwa sikuwa na muda mwingi, niliangalia haraka haraka, nikaona kitabu cha Matigari cha Ngugi wa Thiong'o, kilichotafsiriwa kwa ki-Ingereza na Wangui wa Goro. Ngugi alikuwa amekiandika kwa Kikuyu. Nilivutiwa kuona kuwa ni nakala ya jalada gumu, iliyochapishwa na Africa World Press. Nilichukua. Wasomaji wa Ngugi wanakumbuka kuwa tafsiri hii ilichapishwa kwanza na Heinemann.

Kisha, sehemu hiyo hiyo, katika kuchungulia chungulia, niliona kitabu Contagious Success: Spreading High Performance Throughout Your Organization, kilichoandikwa na Susan Lucia Annunzio. Nilivyoona kuwa kinahusu mbinu za kusambaza ufanisi katika makampuni na mashirika nilikichukua hima. Dhana ya maambukizi ya mafanikio ilinivutia.

Ninapenda kusoma vitabu vinavyohusu ujasiriamali na biashara, kwa sababu mimi mwenyewe ninajiona kama mjasiriamali jamii ("social enterpreneur"). Vile vile, ninavipenda vitabu hivi vinahusu masuala yenye uhusiano na taaluma ambazo nimezizoea, hasa saikolojia.

Saturday, May 13, 2017

Msikilize Raia wa Marekani Anavyomrarua Kiongozi

Jambo moja linalonivutia kuhusu Marekani ni uhuru wa kujieleza. Katiba ya Marekani inalinda uhuru huo kikamilifu. Kwa mfano, kulikuwa na kesi dhidi ya mtu aliyechoma moto bendera ya Taifa, lakini mahakama kuu iliamua na imeendelea kusisitiza kuwa kuchoma moto bendera ya Taifa ni sehemu ya uhuru wa kujieleza, ambao unalindwa na katiba. Mahakama kuu inasisitiza kuwa kauli tata, za kukera, au za kuwakosoa watawala ndizo hasa katiba ilikusudiwa kuzilinda.

Serikali ya Marekani inafahamu kuwa raia ana uhuru na haki kamili ya kuikosoa. Viongozi wa Marekani wanajua hilo. Ninaleta video hapa, inayomwonyesha mwananchi akimfokea kiongozi bila kumung'unya maneno. Mwone kiongozi huyu kutoka chama tawala cha Rais Donald Trump alivyonywea, wakati kipigo kinaendelea.

Thursday, May 11, 2017

Shukrani kwa Msomaji

Msomaji mwingine wa kitabu cha Africans and Americans; Embracing Cultural Differences amejitokeza na kuandika maoni yake kuhusu kitabu hiki. Ameandika maneno matatu tu, "Short and sweet," katika mtandao wa Goodreads, ambao ni maarufu miongoni mwa wasoma vitabu. Humo wanaweka maoni yao kuhusu vitabu walivyosoma au vitabu wanavyopangia kusoma.

Kama ilivyo kawaida yangu katika blogu hii, ninamshukuru kwa kujipatia kitabu hiki, kukisoma, na kuwajuza walimwengu maoni yake. Amefanya hivyo kwa hiari yake, akijua kwamba kauli yake itasomwa na watu wengi. Namshukuru kwa hisani yake; amenifanyia kazi bila malipo wala kutegemea shukrani.

Maoni ya wasomaji yana manufaa makubwa. Kwanza yananiwezesha kufahamu kama ninafikisha ujumbe wangu na unaeleweka vipi. Kila msomaji anapotoa maoni, hutaja jambo fulani au mambo fulani yaliyomgusa kwa namna ya pekee. Wasomaji wanaweza kuwa wamekipenda kitabu hicho hicho, lakini kwa misingi au namna mbali mbali.

Pili, kuwepo kwa maoni ya wasomaji kunaniondolea jukumu la kukiongelea kitabu changu, kwa watu wanaokiulizia. Badala ya mimi kuwaelezea, ninawaelekeza watu wakasome maoni hayo, ambayo wasomaji wameyatoa kwa hiari yao, bila msukumo wa aina nyingine.

Siku nne zilizopita, kwa mfano, m-Tanzania moja aishiye Marekani, aliniandikia ujumbe binafsi katika Facebook akinielezea kuwa anatakiwa kuongea na waalimu kutoka Marekani katika kuwaandaa kwa safari ya Tanzania. Hiyo ni programu baina yao na walimu wa Tanzania kuhusu tamaduni na ufundishaji. Alihitaji pendekezo la kitabu kuhusu tamaduni.

Nilimtajia kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences, na baadaye nimemshauri kuwa ili ajiridhishe, aangalie maoni ya wasomaji kwenye mtandao wa Amazon na pia mtandao wa Goodreads. Kuna sehemu zingine pia ambapo maoni yamechapishwa, kama vile blogu, tovuti, na majarida.

Friday, May 5, 2017

Mwanahabari Amy Goodman Amehutubia Hapa Kwetu

Leo, mwanahabari na mwanaharakati maarufu Amy Goodman amehutubia chuoni Carleton hapa Northfield. Mada yake ilihusu "threats to freedom of the press and the importance of independent media," yaani mambo yanayotishia uhuru wa vyombo vya habari na umuhimu wa media zisizo chini ya mamlaka yoyote. Ninaamini tafsiri yangu inaweza kuboreshwa.

Amy Goodman ni maarufu kama mwendesha kipindi kiitwacho Democracy Now!, ambacho kinachambua masuala kwa mtazamo tofauti na ule wa watawala wakandamizi na propaganda zao za kurubuni watu na kuhalalisha hali iliyopo. Mtazamo wa Amy Goodman ni wa kichochezi kwa maslahi ya walalahoi, wavuja jasho, na wale wanaoonewa na kudhulumiwa. Ni mwana harakati ambaye hasiti kujitosa sehemu ambapo watu wanadhulumiwa ili kuwaunga mkono na kuwezesha sauti zao kusikika ulimwenguni.

Katika mhadhara wake wa leo, ameongelea zaidi hali ya Marekani, akiainisha madhaifu ya vyombo vya habari na media kwa ujumla. Alianza hotuba yake kwa kauli ya kusisimua na kufikirisha ya Thomas Jefferson, "were it left to me to decide whether we should have a government without newspapers or newspapers without a government, I should not hesitate a moment to prefer the latter," yaani "ingekuwa ni mamlaka yangu kuamua kama tuwe na serikali bila magazeti au magazeti bila serikali, nisingesita hata dakika moja kuchagua hilo la pili."

Baada ya hotuba yake, Amy alisaini nakala za kitabu chake, Democracy Now: Twenty Years of Covering the Movements Changing America. Wakati ananisainia, aliniuliza ninatoka wapi. Nilipomtajia Tanzania, alitabasamu, akasema "Julius Nyerere." Niliguswa, ingawa sikushangaa, kuwa Amy ni mmoja wa watu wa ughaibuni wanaomwenzi Mwalimu Nyerere. 

Saturday, April 29, 2017

Tamasha la Mataifa Limefana Rochester, Minnesota.

Leo tamasha la mataifa limefanyika mjini Rochester, Minnesota. Niliweka tangazo la tamasha hili katika blogu hii. Binti yangu Zawadi na mimi tulishiriki. Ni mwendo wa saa moja kutoka hapa Northfield ninapoishi.

Tulipanga vitabu vyangu na machapisho mengine mezani, tukatundika ukutani bendera ya Tanzania ambayo nilinunua siku zilizopita. Saa nne ilipotimia, ambayo ndiyo saa ya kufunguliwa tamasha, watu walianza kuja. Na hapo kwenye meza yetu tulianza kutembelewa na watu tangu dakika zile za mwanzo. Tuliongea nao, tukajibu masuali kuhusu vitabu hivyo na mambo mengine mengi, nao wakatueleza mambo mbali mbali.


Baada ya nusu saa hivi, ilianza shughuli ya kupeperusha bendera. Watu walielekezwa zilipowekwa bendera ili wachukue bendera ya nchi yao na kujiunga katika maandamano wakiwa wamebeba bendera. Nilikwenda nikaikuta bendera ya Tanzania, nikaibeba katika maandamano.

Tuliendelea kuongea na watu wa mataifa mbali mbali hapo kwenye meza yetu, tukapata pia fursa ya kuzunguka kwenye meza za wengine, na kupiga picha. Kwa namna ya pekee ninakumbuka tulivyozungumza na mama mmoja Mmarekani, kuhusu tofauti za tamaduni akatueleza yaliyomkuta Japani. Mila na desturi alizozizoea Marekani ziliwashangaza wenyeji. Nasi tulimweleza yanayotokea pale wa-Afrika wanapokuwa na wa-Marekani, kama nilivyoelezea katika kitabu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences.

Ninakumbuka pia nilivyoongea na mama anayeonekana pichani hapa kushoto amevaa hijab. Nilikumbuka kuwa nilimwona katika tamasha mwaka jana, ila hatukufahamiana. Jana tulipata hiyo fursa, mezani pake, ambapo aliweka machapisho ya ki-Islam, kama vile The Message of the Qur'an cha Muhammad Asad, Who Speaks for Islam cha John L. Esposito na Dalia Mogahed, na Wisdom for Life & The Afterlife: A Selection of Prophet Mohammad's Sayings, ambavyo vyote ninavyo.

Nilimwambia kuwa mimi ni mwalimu katika chuo cha St. Olaf; nimetunga kozi, "Muslim Women Writers." na sababu za kuitunga. Naye alinielezea kuhusu kipindi anachoendesha kiitwacho Faith Talk Show, tukakubaliana nije kuhojiwa katika kipindi hicho siku zijazo.

Baada ya kurejea kutoka kwenye tamasha, nimeangalia mtandaoni, nikaona taarifa za mama huyu kama vile hii hapa. Ninawazia kumwalika darasani kwangu nitakapofundisha tena kozi yangu.

Muda wote wa tamasha kulikuwa na vikundi vya burudani jukwaani na pia vyakula vya nchi mbali mbali. Ninaleta hapa baadhi ya picha za tamasha.





Thursday, April 27, 2017

Bendera ya Tanzania Kupepea Rochester, Minnesota

Kwa mara ya kwanza bendera ya Tanzania itapeperushwa katika tamasha la kimataifa mjini Rochester, Minnesota, tarehe 29 mwezi huu. Hili ni tamasha linaloandaliwa na Rochester International Association (RIA) kila mwaka. Nimewahi kuelezea kuhusu tamasha hili katika blogu hii na blogu ya ki-Ingereza.

Napenda kuelezea mchakato uliowezesha bendera ya Tanzania kupewa hadhi hiyo. Mwaka jana wa-Kenya wawili, Olivia Njogu na Kennedy Ombaye, ambao ni wanabodi wa RIA, waliniambia kuwa wangependa nijiunge nao. Niliguswa na wazo lao, nikaafiki. Waliwasilisha ujumbe kwa mwenyekiti wa bodi, Brian Faloon, nami nikawasiliana naye kumthibitishia utayari wangu wa kujiunga. Wazo lilipitishwa na bodi, nami nikajiunga.

Wiki chache zilizopita, bodi ilianza kujadili mipango ya tamasha la kimataifa kwa mwaka huu. Wakati suala la bendera lilipojadiliwa, mwanabodi Olivia Njogu aliniambia kuwa iwepo bendera ya Tanzania. Kwa kuwa sikuelewa utaratibu wa bendera ukoje, Olivia na wanabodi wengine walinihakikishia kuwa sitahitaji kuileta bendera, bali wataipata kwa muuzaji. Nilifahamu kuwa utaratibu wa tamasha ni kuwa linapoanza, panakuwa na maandamano ya watu wakiwa wamebeba bendera za nchi mbali mbali.

Mwaka jana niliposhiriki tamasha hili, nilikuwa na bendera ya Tanzania, ambayo nilikuwa nimeinunua mwaka juzi, kama nilivyoelezea katika blogu hii. Lakini kwa kuwa nilikuwa bado mgeni katika tamasha hili, sikuwa nimefanya utaratibu wa kuijumlisha katika maandamano ya bendera. Niliitandaza kwenye meza yangu, kama inavyoonekana pichani hapa kushoto.

Ninawashukuru tena wa-Kenya kwa urafiki na ukarimu ambao wamenionyesha tangu nilipokwenda nchini kwao kufanya utafiti, kuanzia mwaka 1989, hadi miaka yote niliyoishi huku Marekani. Jambo hili nimekuwa nikilitaja katika blogu hii.

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...