Kama ilivyo kawaida yake, Kipanya hakosi neno. Kwenye katuni hapa kushoto katoboa ukweli: Tanzania ni nchi ya mavuvuzela. Tukubaliane kwa hilo.
Tuesday, November 27, 2012
Tanzania: Nchi ya Mavuvuzela
Kama ilivyo kawaida yake, Kipanya hakosi neno. Kwenye katuni hapa kushoto katoboa ukweli: Tanzania ni nchi ya mavuvuzela. Tukubaliane kwa hilo.
Monday, November 26, 2012
Wanafunzi Wangu wa ki-Ingereza Muhula Huu
Wanafunzi wote wanaosoma hapa chuoni St. Olaf wanatakiwa kusoma somo hilo kama msingi wa masomo ya chuo. Kwa vile wanafunzi ni wengi, tunawagawa katika madarasa madogo, yasiyozidi wanafunzi 18 kila darasa. Uchache huu unamwezesha mwalimu kumsaidia kila mwanafunzi ipasavyo, kwa kuhakiki uandishi wake na kumpa mawaidha.
Ninapenda kufundisha masomo yote ninayofundisha. Ninawapenda wanafunzi. Lakini kwa vile mimi ni mwandishi, ninapenda kwa namna ya pekee kufundisha uandishi wa lugha ya ki-Ingereza.
Kutumia ki-Ingereza vizuri kabisa ni mtihani mkubwa, kama mwandishi maarufu Ernest Hemingway alivyokiri na kutukumbusha. Hata huku ughaibuni kwa wenye lugha hii, wengi hujiandikia tu na kuamini kuwa wameandika ki-Ingereza vizuri. Kukaa nao na kuwaonyesha njia nzuri ni bahati na baraka ambayo ninaifurahia.
Sunday, November 25, 2012
Rais Obama Anunua Vitabu
Jana Rais Obama aliripotiwa akinunua vitabu kwenye duka dogo, kwa lengo la kuchangia mapato ya wafanya biashara wadogo.
Alitanguzana na binti zake, akanunua vitabu 15 vya watoto, kwa ajili ya kuwagawia ndugu. Picha ionekanayo hapa ni ya J. Scott Applewhite, Associated Press.Niliposoma taarifa hii, nilijiuliza je, ni lini tumewahi kuwaona vigogo wa Bongo wakinunua vitabu? Ni lini umewahi kumwona kigogo wa Bongo akiwa na wanawe katika duka la vitabu? Pia nilikumbuka kuwa niliwahi kuuliza katika blogu hii kama unaweza kumpa m-Tanzania kitabu kama zawadi ya Krismasi au Idd el Fitri. Soma hapa.
Kama vigogo wa Bongo wangekuwa na utamaduni wa kuvithamini vitabu, wangeweza kuleta mabadiliko makubwa nchini. Wangeweza kuanzisha maktaba vijijini. Wangeweza kuanzisha klabu za usomaji wa vitabu.
Vigogo hao husafiri sana nje ya nchi. Kwenye viwanja vya ndege, iwe ni O'Hare, Schippol, Heathrow, Johannesburg, au Istanbul, kuna maduka ya vitabu. Vigogo hao wangeweza kununua vitabu kila wanaposafiri na kuvipeleka kwenye maktaba za mkoa, shule na vyuo. Hebu fikiria, ukimpelekea hata tu kamusi ya ki-Ingereza mwalimu wa shule kule Lindi au Kalenga, unakuwa umeleta mapinduzi fulani katika ufundishaji kwenye shule hiyo.
Sisemi tu kwa kujifurahisha au kuwalaumu wengine. Mimi mwenyewe nanunua sana vitabu, na hadi sasa ninavyo zaidi ya elfu tatu. Niliposoma Marekani, 1980-86 nilinunua vitabu vingi sana, nikarejea navyo Tanzania. Ingawa watu walinishangaa kwa kuleta vitabu badala ya gari, vitabu hivyo vimewafaidia wanafunzi na wasomi wengi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Baada ya kuja kufundisha Marekani, 1991, nimenunua vitabu vingi zaidi. Nikifanikiwa kuvisafirisha nitakaporudi Tanzania, itakuwa ni hazina kubwa kwa wapenda elimu. Ila sina hakika kama nitaweza kuvisafirisha, kwani ni vingi mno. Itabidi wa-Tanzania wafanye mchango waniletee hela za kusafirishia vitabu hivyo. Uwezo wanao sana, kama inavyothibitika katika michango ya sherehe mbali mbali. Vinginevyo huenda nikaamua kuviuza hapa hapa Marekani nipate hela za kununulia angalau bajaji. Itanisaidia baada ya kustaafu Tanzania.
Thursday, November 22, 2012
Kanisa Katoliki Mjini New Prague, Minnesota

Jana nilifika mjini New Prague hapa Minnesota, kwa shughuli binafsi. Nilishawahi kupita kwenye mji huu mara kadhaa, na kitu kimoja kilichonivutia tangu mwanzo ni kanisa Katoliki ambalo liko katikati ya mji, pembeni mwa barabara.Watu waliniambia tangu zamani kuwa kanisa hili lilijengwa na wahamiaji kutoka Czechoslovakia, na kwamba madirisha yake ya vioo (stained glass) yanavutia sana. Nilikuwa na hamu ya siku moja kwenda kusali hapo na pia kuangalia hayo madirisha. Mimi hupenda nyumba za ibada za dini mbali mbali kama nilivyoeleza hapa na hapa.
Jana, kwa vile nilikuwa mjini hapo, nilihakikisha nimepiga picha ya kanisa hilo, ingawaje ni kwa nje tu. Nilipata fursa ya kuona kuwa pembeni mwa kanisa kuna shule. Huu ni utamaduni wa kanisa Katoliki, kwamba panapojengwa kanisa, na huduma zingine ziwepo, hasa shule na hospitali. Nilivyoliangalia hilo kanisa na hiyo shule, nilikumbuka kijijini kwangu, kwani kule nako hali ni hiyo hiyo.
Monday, November 19, 2012
Kwa wa-Luteri wa Tungamalenga, Iringa
Nimewahi kutembelea Shepherd of the Valley kuongea na wanafunzi wa Chuo cha Gustavus Adolphus ambao walikuwa hapo kufanya maandalizi ya safari ya Tanzania, kama nilivyoelezea hapa.
Kwa miaka mingi kiasi nilifahamu kuhusu uhusiano baina ya Shepherd of the Valley na Tungamalenga. Kila ninapoliwazia kanisa la Shepherd of the Valley, au ninapoliona, naiwazia Tungamalenga, ingawa mimi si m-Luteri. Kwa vile liko pembeni mwa barabara, ninaliona kanisa hilo kila ninapoenda kutoa mihadhara katika Chuo cha Mazingira.
Sikuwahi kufika Tungamalenga, hadi mwaka jana, niliposafiri na wanafunzi wa ki-Marekani kutoka Iringa kwenda hifadhi ya Ruaha. Ghafla tulipita sehemu iitwayo Tungamalenga. Nilishtuka, kwa sababu sikuwa hata najua kama Tungamalenga iko katika njia hiyo, karibu kabisa na hifadhi ya Ruaha.
Picha inayoonekana hapa juu nilipiga tarehe 13 Novemba, nilipokuwa narudi kutoka kwenye Chuo cha Mazingira. Kwa miaka miwili au zaidi nilitaka niweke picha ya Shepherd of the Valley hapa katika blogu yangu, nikiwawazia wa-Luteri wa Tungamalenga.
Saturday, November 17, 2012
Mdau Wangu Mpya, Mhadhiri wa Mankato
Nimempata mdau mpya, mhadhiri katika chuo cha North Central, mjini Mankato, Minnesota. Natumia neno mdau au wadau kwa maana ya wasomaji wa vitabu vyangu ambao wanajitokeza na kujitambulisha kwangu. Nina kawaida ya kuwataja wadau hao katika hii blogu yangu, kama unavyoweza kusoma hapa na hapa.Leo napenda nimwongelee huyu mdau mpya, Mhadhiri Davis. Wiki kadhaa zilizopita, nilipigiwa simu na Profesa Scott Fee wa Chuo Kikuu cha Minnesota, Mankato, akisema kuwa wakati anapiga simu, yuko katika mazungumzo na Mhadhiri Becky Davis, wakiongelea kitabu changu cha Africans and Americans: Embracing Cultural Differences. Alinipa fursa nikasalimiana na Mhadhiri Davis, ambaye anaonekana pichani hapa kushoto.
Waalimu hao walikuwa katika maandalizi ya kupeleka wanafunzi Afrika Kusini. Pamoja na kuongelea upatikanaji rahisi wa nakala za kitabu hiki, walikuwa wananialika Mankato kuongea na wanafunzi. Bila kusita, niliupokea mwaliko wao. Falsafa yangu ni kuwa Mungu kanipa fursa ya kuelimika sio ili nimwage mbwembwe bali niwafaidie wanadamu.
Profesa Scott Fee tulifahamiana miaka kadhaa iliyopita, wakati anaandaa msafara wa wanafunzi wa kwenda Afrika Kusini. Katika maandalizi hayo, aliamua kutumia kitabu changu hicho. Kama sehemu ya maandalizi ya safari, alinialika chuoni kwake kuongea na wanafunzi kuhusu masuala ya tofauti za tamaduni, kama nilivyoelezea kitabuni. Nilienda, nikaongea na wanafunzi, ambao walikuwa wengi, kama ninavyokumbuka.
Baada ya kutajiwa jina la Mhadhiri Davis, niliingia mtandaoni kutafuta taarifa zake. Yeye ni mwandishi makini, kama ilivyoelezwa hapa. Nafurahi kuunganishwa na mwandishi mwenzagu, kwani kutakuwa na fursa ya kubadilishana mawazo na uzoefu.
Nashukuru kwamba kazi yangu ya kutafakari na kuandika kuhusu masuala ya tofauti za tamaduni inawagusa na kuwafaidia wengine. Insh'Allah, siku itakapowadia, nitaenda Mankato na kutoa mchango wa kiwango cha juu kwa kadiri ya uwezo wangu.
Tuesday, November 13, 2012
Kitabu cha Mazungumzo ya Nelson Mandela
Leo nimenunua kitabu cha Nelson Mandela, Conversations with Myself. Ingawa sijui nitakisoma lini, kutokana na utitiri wa vitabu vyangu, nimekinunua kutokana na umaarufu wa Mandela na kutokana na ukweli kwamba kumbukumbu zake na mawaidha yake ni hazina kubwa.
Idadi ya vitabu vinavyosimulia na kuchambua mchango wa Mandela vinaendelea kuchapishwa. Yeye mwenyewe pia amejitahidi kuandika. Kwa mfano, tulipokuwa vijana, tulikifahamu kitabu chake kiitwacho Long Walk to Freedom. Haikuwa rahisi mtu usikijue kitabu hiki, kwani kilichapishwa katika mfululizo maarufu wa vitabu vya shirika la Heinemann, ambalo tulilifahamu sana kutokana na vitabu vyake ambavyo tulikuwa tunavisoma.
Miaka ya karibuni, Mandela amejikakamua akaandaa kitabu cha hadithi, Nelson Mandela's Favorite African Folktales. Ni mkusanyiko wa hadithi za asili za ki-Afrika.
Kwa kuangalia juu juu, nimeona kuwa hiki kitabu cha Conversations with Myself ni mkusanyiko wa barua mbali mbali za Mandela na maandishi mengine ambayo yanatufunulia picha ya Mandela sio tu kama mwanasiasa na mpigania ukombozi maarufu bali kama binadamu. Ni kitabu kikubwa, kurasa 454. Nitakuwa nakisoma kidogo kidogo. Isipokuwa ni kimoja kati ya vitabu vya pekee kabisa katika maktaba yangu.
Idadi ya vitabu vinavyosimulia na kuchambua mchango wa Mandela vinaendelea kuchapishwa. Yeye mwenyewe pia amejitahidi kuandika. Kwa mfano, tulipokuwa vijana, tulikifahamu kitabu chake kiitwacho Long Walk to Freedom. Haikuwa rahisi mtu usikijue kitabu hiki, kwani kilichapishwa katika mfululizo maarufu wa vitabu vya shirika la Heinemann, ambalo tulilifahamu sana kutokana na vitabu vyake ambavyo tulikuwa tunavisoma.
Miaka ya karibuni, Mandela amejikakamua akaandaa kitabu cha hadithi, Nelson Mandela's Favorite African Folktales. Ni mkusanyiko wa hadithi za asili za ki-Afrika.
Kwa kuangalia juu juu, nimeona kuwa hiki kitabu cha Conversations with Myself ni mkusanyiko wa barua mbali mbali za Mandela na maandishi mengine ambayo yanatufunulia picha ya Mandela sio tu kama mwanasiasa na mpigania ukombozi maarufu bali kama binadamu. Ni kitabu kikubwa, kurasa 454. Nitakuwa nakisoma kidogo kidogo. Isipokuwa ni kimoja kati ya vitabu vya pekee kabisa katika maktaba yangu.
Subscribe to:
Posts (Atom)
Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault
Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...
-
Ukizunguka mitaani Dar es Salaam, utakuta matangazo mengi ya waganga wa kienyeji. Waganga hao wanatoka sehemu mbali mbali, kama vile Sumbaw...
-
Leo napenda kukitambulisha kwako mdau kitabu muhimu cha ki-Swahili, Tenzi Tatu za Kale . Nilinunua nakala yangu miaka kadhaa iliyopita katik...
-
Jina la Shaaban Robert ni maarufu miongoni mwa wa-Tanzania na wengine wa nchi zingine wanaokijua ki-Swahili. Lakini, tujiulize ni wa-Tanza...
