Monday, June 3, 2013

Tunaanza Kusoma "Midnight's Children, Kitabu cha Salman Rushdie

Wiki kadhaa zilizopita, niliezea katika blogu hii azma yangu ya kufundisha kitabu cha Salman Rushdie kiitwacho Midnight's Children.

Sasa wakati wa kufanya hivyo umefika. Leo ni siku ya kwanza ya muhula wa kipindi cha joto. Ni siku ya kwanza ya somo langu la Post-colonial Literature. Leo nimejitambulisha kwa wanafunzi na kuitambulisha kozi.

Nimeongelea maana ya Post-olonial literature na utata uliopo katika dhana hiyo, malumbano yanayoligubika dhana hiyo.

Nimetoa utangulizi kuhusu India, historia ya utamaduni wake na fasihi yake, nikianzia na tungo za kale za Mahabharata na Ramayana, nikalipitisha darasa hadi kwenye uandishi wa watu kama Kalidasa, Tagore, Raja Rao, Mulk Raj Anand, na R.K. Narayan. Niliwaelezea jinsi, kwenye miaka ya sitini hadi leo, wanawake wamejitokeza katika uandishi wa India na wanatoa mchango mkubwa.

Hayo yote yalikuwa ni sehemu ya  matayarisho ya kusoma na kujadili Midnight's Children. Nimewaelezea kiasi habari za mwandishi Salman Rushdie, maandishi yake, na zogo lililozuka duniani baada ya yeye kuchapisha kitabu cha Satanic Verses.

Hayo niliyowaeleza leo yatakuwa yanajitokeza tena na tena wakati wa kujadili kazi za fasihi. Nimefurahi kuwajulisha wanafunzi majina ya waandishi mbali mbali. Tutakaphotimisha majadiliano kuhusu Midnight's Children, tutasoma The Guide, riwaya ya R. K. Narayan, ambaye nimemtaja leo.

Baada ya hizo kazi za fasihi ya India, tutasoma kazi kadhaa za fasihi ya Afrika, ambazo ni Half of a Yellow Sun kilichoandikwa na Chimamanda Ngozi Adichie wa Nigeria na Unconfessed kilichoandikwa na Yvette Christianse wa Afrika Kusini.

Nimewaambia wanafunzi kuwa ni kawaida yangu kuweka katika kozi yangu baadhi ya vitabu ambavyo sijawahi kuvisoma. Ninapenda changamoto ya kuvisoma sambamba na wanafunzi.

No comments:

Tangazo la Maongezi Yangu Books on Central, Faribault

Kwa miaka mingi, nimeongea na hadhira mbali mbali hasa kuhusu tofauti za tamaduni. Matangazo huandaliwa na kusambazwaa kabla ya mikutano. Ka...